Habari za Punde

Omar Ali Shehe atakiwa ajisalimishe mwenyewe Polisi

Na Salmin Juma – Pemba.
Jeshi la Polisi Zanzibar  linamtaka Ndg Omar Ali Shehe (Mkurugenzi wa uchaguzi wa CUF) kujisalimisha mara moja kwa kamanda wa Polisi wa Mkoa wa kusini Pemba  kwa mahojiano dhidi ya tuhuma nyingi zinazomkabili dhidi ya vitendo vya kihalifu vinavyoendelea Pemba.
Amri hiyo ya kuwataka kujisalimisha ilikua ikimuhusu pia  Hija Hassan Hija (aliekua mwakilishi wa jimbo la kiwani CUF) lakini tayari ameshapatikana leo hii.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa makao makuu ya Jeshi la Polisi Madungu  Mkoa wa Kusini Pemba leo Naibu Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Polisi Zanzibar Salum Muhammed Msangi amesema kua tangia tarehe 18/05/2016 kumejitokeza vitendo vya kihalifu katika  mkoa ya kaskazini Pemba maeneo ya Tumbe na Mtambwe  na kwa kusini maeneo ya  Ziwani, Chonga na Kiwani
Msangi amesema vitendo hivyo ni pamoja na uharibifu wa mali ikiwemo kukata mazao kama vile mikarafuu, migomba na kung’oa minazi, kubomoa na kuchoma moto nyumba, kuzuia watu wengine  kufanya ibada na mengineyo.
Aidha amesema uhalifu huo umeibuka mara tu baada ya ziara ya Katibu Mkuu wa chama cha wananchi CUF Seif Sharif Hamad hali ambayo inaonesha kua kuna maelezo maalum ya kufanyika hujuma hizo dhidi ya wafuasi wa CCM ambapo Ndg Omar Ali Shehe pamoja na  Hija Hassan Hija wanaonekana kuhusika.

“Hija Hassan Hija tayari tumeshampata, tunamtaka Omar Ali Shehe kujisalimisha  kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa kusini Pemba kwa mahojiano na asipofanya hivyo jeshi la polisi litamtafuta kwa namna yoyote ile, mahali popote duniani na kumtia mbaroni”alisema Msangi
Amefahamisha kua hadi sasa jumla ya matukio 21 ya uhalifu yametokea, 12 kati yao yamefanyika katika Mkoa wa Kaskazini huku 9 yakiwa yamefanyika katika Mkoa wa Kusini.
Amesema kufuatia hali hiyo jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama  vilianza operesheni ya kukabiliana na wahalifu hao ambapo hadi sasa  watuhumiwa 43 wameshakamatwa  na kati ya hao 16  wameshafikishwa mahkamani mkoa wa kaskazini Pemba.
Pia watuhumiwa wengine 53 walikamatwa  na kati yao 19 wameshafikishwa mahkamani mkoa wa kusini Pemba.
Kamanda Msangi amesema ingawa uhalifu huo unaonekana ni wa kawaida lakini uchunguzi wa jeshi hilo umeonesha kua vitendo hivyo vinahusishwa na uhasama wa  kisiasa ikizingatiwa kua waathirika wote wa matukio hayo ni wafuasi wa chama cha mapinduzi CCM.

Amesema pamoja na jeshi la Polisi kuendelea na uchunguzi wa matukio hayo bado linatoa onyo kwa wale wote wanaojihusisha na vitendo hivyo ikiwa ni pamoja na  wale wanaotoa maelekezo  na kuhamasisha utendeji wa uhalifu huwo, jeshi la polisi linawataka kuacha maramoja vitendo hivyo kwani operation dhidi yao  itakua endelevu na yakudumu hadi pale wahalidu wote watakapotii sheria bila ya kushurutishwa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.