Habari za Punde

Dk Shein: Zanzibar Inakaribisha Uwekezaji Utakaosaidia Kuinua Uchumi na Kuimarisha Ustawi wa Watu Wake.

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
    Zanzibar                                                                                            20 Julai, 2016
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema Zanzibar iko tayari kushirikiana na wawekezaji wote ambao uwekezaji wao utasaidia kuinua uchumi wake na kuimarisha ustawi wa wananchi wake.

Akizungumza na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Huawei Technologies Tanzania Cooperation Limited Bwana Bruce Zhang, Ikulu leo, Dk. Shein amesema kuwa wawekezaji wanakaribishwa Zanzibar kuwekeza katika sekta zote za uchumi na kijamii.

“wawekezaji wakiwemo kampuni ya Huawei wanayo fursa ya kuwekeza katika maeneo mbalimbali ya uwekezaji katika sekta zote ikiwemo nishati, tekinolojia ya habari na mawasiliano, viwanda, uvuvi na kadhalika” Dk. Shein alimueleza bwana Zhang.   
Alifafanua kuwa wawekezaji wanaweza kuwekeza wakiwa wao wenyewe au hata kwa kushirikiana na serikali kwa kuingia ubia lakini akabainisha kuwa miradi ya ubia ni ile ambayo ni ya kipaumbele tu kwa serikali.

“miradi ya pamoja tunaikaribisha na tuko tayari kushirikiana na makampuni ya uwekezaji kuendesha miradi ya pamoja kwa hivyo milango iko wazi kwa hilo ikiwemo kwa Kampuni ya Huawei” Dk. Shein alisema.

Dk. Shein alimueleza Mkurugenzi Mtendaji huyo ambaye alikuwa amefuatana na Mkurugenzi wa Kampuni hiyo anayefanyia kazi zake Zanzibar bwana Peter Jiang kuwa amefurahishwa na dhamira ya kampuni hiyo ya kuendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

“taarifa ya dhamira ya Kampuni yenu kushirikiana na serikali katika sekta mbalimbali zikiwemo afya, elimu na uendelezaji wa Programu ya Miji Salama imenifurahisha na kunitia moyo” Dk. Shein alieleza.

Dk. Shein alimueleza Bwana Zhang kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwa ilianzisha Programu ya Miji Salama miaka miwili na nusu iliyopita na utekelezaji wake unaendelea vyema hivyo kujitokeza kwa Huawei kuunga mkono progamu hiyo hizo ni habari njema kwa serikali na wananchi wa Zanzibar.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein alieleza pia kuwa Zanzibar inathamini sana ushirikiano wake na Jamhuri ya Watu wa China na kwamba kuwepo kwa makampuni ya kichina humu nchini ni moja kati ya matokeo ya ushirikiano huo.  

Kwa upande wake Mkurungenzi Mtendaji huyo wa Huawei alimueleza Mheshimiwa Rais kuwa Kampuni yake inatarajia kuongeza uwepo wake Zanzibar kwa kupanua shughuli zake ikiwemo kuongeza huduma kwa jamii ikiwa ni pamoja kusaidia sekta ya elimu, afya na kuendeleza dhana ya miji salama.

“Kampuni yetu sasa inaaminiwa nchini China na nchi za nje hivyo shughuli zetu zimekuwa zikipanuka mwaka hadi mwaka kote ulimwenguni ikiwemo nchini Tanzania” Bwana Zhang alisema.

Alibainisha kuwa kampuni yake imepata mafaniko makubwa nchini Tanzania na hiyo imetokana na kampuni hiyo  kuwa na mahusiano mazuri naSerikali na sekta binafsi.

Alifafanua kuwa hivi sasa kampuni yake inatoa huduma kwa makampuni yote makubwa ya simu humu nchini kitu ambacho kinathibitisha ubora na umahiri wa huduma za kampuni yake.

Bwana Zhang alieleza kuwa kadri inavyowezekana kampuni yake inatilia mkazo kuwaendeleza vijana wa kitanzania katika shughuli zake ili kuwapatia ujuzi na utalaamu waweze kufanyakazi wakiwa wataalamu bora.  

Mazungumzo hayo yalihudhuriwa pia na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Issa Haji Ussi Gavu na Mshauri wa Rais Ushirikiano wa Kimataifa, Uchumi na Uwekezaji Balozi Mohamed Ramia Abdiwawa.    

Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.