Habari za Punde

Tamko la chama cha Wanasheria kulaani kauli ya Jeshi la Polisi kwa mawakili wa utetezi kesi za Jinai

Na  Khadija Khamis  - Maelezo  Zanzibar    01/07/2016.

CHAMA CHA WANASHERIA  Zanzibar (Zanzibar law society)  kimelaani  taarifa za onyo zilizotolewa na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Zanzibar ,Naibu Mkurugenzi Salum Msangi kuhusiana na wanasheria wanaojitokeza kuwatetea watuhumiwa wa uhalifu  na kuwataka waache mara moja akibainika watanganishwa na watuhumiwa hao .

Hayo yameelezwa leo  na Rais wa Wanachama cha Wanasheria Zanzibar {Zanzibar  Law Society) Omar Said Shaaban huko katika Ukumbi wa  Wanasheria Kwamchina Mwanzo wakati akizungumza na waandishi wa vyombo mbali mbali  vya habari .kuhusiana  na kushtushwa na taarifa hizo.

Alisema Chama cha Wanasheria kimetafakari kauli  hiyo na kuona Naibu Kamishna Msangi wa Jeshi la Polisi wanakosoa na kuchukizwa na sheria inayotambua kuwepo kwa wanasheria na kazi zao .

Aidha  alisema  Naibu huyo  na Jeshi la Polisi amechukizwa na Kukosoa utaratibu wa sheria unaompa mamlaka Jaji Mkuu wa Zanzibar kuteua wakili wa kuwawakilisha  watuhumiwa wa kesi za jinai hasa zile za mauaji .

Alieleza kuwa Naibu Kamishna na Jeshi la Polisi hawaamini ,hawajui au wanapuuza uwepo wa mawakili wa utetezi kama nguzo muhimu katika mfumo wa utoaji  haki katika mwenendo wa makosa ya jinai .

Alifahamisha kuwa Naibu huyo na Jeshi la Polisi  hawafahamu kuwa nani mwenye mamlaka ya kuamua wa kuunganishwa kwenye kesi ya jinai ni Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar pekee.

Alisisitiza kwamba kuwepo kwa fani ya wanasheria na kazi zao ni kuwepo kwa mujibu wa sheria ya wafanyakazi za sheria sura 28 ya sheria ya Zanzibar .

Omar alisema Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 imeeleza kuwa mtu alieshtakiwa kwa kosa la jinai hatatendewa kama mtu mwenye kosa hilo mpaka itakapothibitika kuwa anayo hatia ya kutenda kosa hilo.

Aidha  Wanasheria hao wameiomba Serikali kutoa tamko la kukerwa na kutokubaliana  na kauli hiyo ya Naibu Kamishna  wa Polisi  Salum Msangi na kuwahakikishia mawakili  hao uhuru na usalama wao wanapotekeleza majukumu yao kwa mujibu wa katiba na sheria ya Zanzibar .





1 comment:

  1. kiukweli nchi yetu inaendeshwa kidicteta sasa

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.