Habari za Punde

WanaCCM Z'bar watarajiwa makubwa kukabidhiwa kwa uenyekiti Dkt John Magufuli

TAKDIR ALI - MAELEZO ZANZIBAR.                              .

WANACHAMA wa chama cha Mapinduzi Zanzibar wamesema kukabidhiwa kwa uwenyekiti Dkt. John Pombe Magufuli kunawapa matumaini makubwa ya mabadiliko katika uwajibikaji.

Wamesema kitendo cha Dkt Magufuli kuwaajibisha wanaofanya ubadhirifu wa mali ya Umma Serikalini kitaweza kuleta maendeleo ya haraka kwa nchini na kufanyakazi kwa uadilifu.

Akizungumza na Mwandishi wa habari hizi Mwasisi wa Maskani ya Kisonge Suleiman Omar Seleganzi amesema kitendo hicho kinaleta  matumaini makubwa kwa WanaCCM, Wananchi na Wapenda maendeleo nchini.

Seleganzi amesema Dkt.Magufuli ni kiongozi muadilifu, mpenda maendeleo ambae ni mchapa kazi na mwenye nia njema ya kuwatetea Wananchi wa Tanzania hususan wa kipato cha chini kwa kusimamia ipasavyo ilani ya chama cha Mapinduzi.

“Tumepata matumaini makubwa ya kupata Maendeleo Dkt. Magufuli hasa kwa kuwaajibisha wafanyakazi wabadhirifu wa mali ya umma,” alisema Mwasisi huyo wa Kisonge Seleganzi.

Amesema kitendo cha kupunguza Mshahara wake na baadhi ya watendaji wa Serikali na kuwaajibisha wale wote wanaofanya ubadhirifu kwa kutumia vibaya madaraka yao ni dalili tosha ya kuleta mabadiliko nchini.

Kwa upande wake Mwanachama mkongwe wa CCM Maskani ya Kizota Adil Ali Adil amempongeza Dkt. Magufuli kwa kukabidhiwa nafasi hiyo sambamba na juhudi zake za kupambana na Rushwa pamoja na kujali Wananchi wa makundi yote ikiwemo wanawake na Watu wenye ulemavu kwa kuwapa nafasi mbali mbali za Uongozi.

“Pia tunampongeza kwa kusimamia vizuri Taasisi za serikali ikiwa ni pamoja na kuwaondosha watendaji wazembe wenye kujali maslahi yao binafsi na familia zao,” amepongeza Kada huyo

Amesema Mwenyekiti anaemaliza muda wake Dkt Jakaya Mrisho amefanya kazi nzuri ambayo Dkt. Makufuli anapaswa kuiendeleza zaidi ili kuongeza kasi ya Maendeleo na kufikia Tanzania ya Viwanda.
“Dkt Kikwete amepeleka jahazi vizuri lakini tunatumai Magufuli azidi kasi mara dufu”Alisema Mwanachama huyo wa Maskani ya Kizota.
Nae Suhaila Masoud Muhammed kutoka Maskani ya Kisonge amemuomba Dkt. Magufuli kuendelea kutetea maslahi ya Wanawake kwa kuwaamini na kuwapa nafasi za Uongozi katika Serikali yake.
“Wanawake wanaweza kuongoza bila wasiwasi wowote jambo ambalo Magufuli ameamua kulioneshea mfano kwa kuwaopa Wanawake nafasi za Uongozi,” alisema mkereketwa huyo wa CCM Maskani ya Kisonge.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Taifa Abrahmani Kinana amesema Maandalizi ya Mkutano Mkuu wa Chama hicho, unaotarajiwa kufanyika Jumamosi tarehe 23 mwezi huu huko Dodoma kwa kumchagua Rais Magufuli kuwa Mwenyekiti kwa kipindi cha miaka mitano ijayo kuchukuwa nafasi ya Rais Mstaafu Jakaya Kikwete yamekamilika

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.