Habari za Punde

Marehemu Seif Hassan Mohamed “albajun’ameacha pengo kubwa

Na mwandishi wetu , PEMBA
MAMIA ya wananchi Kisiwani Pemba, wakiongozwa na mkuu wa wilaya ya Mkoani Hemed Suleiman Abdall, Mameneja wa redio Jamii za Mkoani na Micheweni kisiwani humo, wameshiriki katika mazishi ya mwandishi wa habari na mtangazaji wa redio Jamii Mkoani, Seif Hassan Mohamed, aliyefariki dunia usiku wa kuamikia jana.
Mwanahabari huyo amefikwa na mauti hayo Mkoani mjini, baada ya kupata ajali, wakati akiendesha vespa, na kugonga gari iliokuwa imewekwa pembezoni mwa barabara.
Marehemu alizikwa kijijini kwao Stahabu Mkanyageni Wilaya ya Mkoani Pemba, baada ya kusaliwa msikiti wa Kibigilini Mkoani na Mkanyageni wilaya ya Mkoani.
Seif Hassan ambaye hadi anakumbwa na umauti, alikuwa ni mkuu wa vipindi Redio Jamii Mkoani, pia alikuwa ni mwanafunzi wa Chuo cha Uandishi wa habari (TSJ) tawi la Pemba mwaka wa mwisho ngazi ya diploma.
Akizungumza na waandishi wa habari, mara baada ya kukamilisha taratibu za mazishi, kaka wa marehemu Mohamed Hassan Mohamed ‘shidadi’ alisema kifo cha marehemu ndugu yake, ni pengo kubwa katika familia yao.
Alisema kuwa marehemu alikuwa ni kiungo muhimu sio tu ndani ya familia yao, bali hata kwa majirani,  kutokana na umahiri wake wa kujituma na kuisaidia watu katika mambo mbali mbali.
“Kuondokewa na ndugu yangu, kumeacha pengo kubwa sana kwetu, alikuwa mtu muhimu kila mtu alikuwa anampenda, hata ukiangalia zaidi watoto, ambao alikuwa nao karibu, lakini ndio wakati wamefika, na ndio mipango ya Mwenyezi Mungu”,alisema.
Afisa Mipango wa Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar ZLSC tawi la Pemba Khalfan Amour Mohamed, alisema mwandishi na mtangazaji huyo, alikuwa akikitumia sana kituo chao, ili kujifunza na kutengeneza vipindi vya sheria.
Nae Mkuu wa Wilaya ya Mkoani Hemed Suleima Abdalla, alimtaja marehemu Seif kuwa, alikuwa ni kiungo muhimu sio tu kwenye fani ya habari pekee, bali hata katika jamii.
“Marehemu alikuwa ni mtu wa watu hapa Mkoani na nje, kwake yeye mkubwa na mdogo alikuwa ni wake, kuondoka kwake hakuna aliyeweza kufikiria, kwa kweli pengo lake lipo na vigumu kuzibika kwa haraka”.alisema.
Meneja wa Radio Jamii Mkoani, Ali Abass Omar alisema kuondokewa kwa mkuu wake wa vipindi, kutachukuwa muda mrefu, kuzibika kwa pengo hilo hasa katika kipindi chake cha ‘meza ya habari’.
“Vipindi vyake kwa sasa kupatikana mtu wa kuweza kuviziba ni pengo kubwa sana, itachukuwa muda mkubwa kuzibika. Lakini hayo ni mipango ya Mungu mwenyewe hayo”,alsiema.
Kwa upande wake Meneja wa Redio Jamii Micheweni Ali Massoud Kombo, alisema marehemu Seif alikuwa ni mtetezi mkubwa kwa redio za jamii nne za Zanzibar hata za Tanzania nzima.
“Huyu alikuwa akizitetea sana Radio za jamii zote, katika vikao mbali mbali kuhakikisha redio hizi zinadumu kwa muda mrefu na kupata mafanikio, kuondoka kwake kumetuachia majonzi mengi sisi viongozi wa radio za Jamii”,alisema.
Mwenyekiti wa bodi ya Raido Jamii Mkoani mwalim Hamdu Hassan Bakari, alisema kuondokewa na Seif ameacha pengo kubwa kwao, huku akiwataka vijana waliobakia kuvaa viatu vya marehemu katika ufanyaji wake wa kazi.
Kwa upande wao wafanyakazi wa Radio Jamii Mkoani, Shaib Kifaya Omar, Rahma Juma, Amina Masoud pamoja na Khatib Juma Nahoda, walisema marehemu alikuwa ni mtendaji mkubwa katika radio yao, pamoja na umahiri wake huku akiwasihi wafanyakazi wenzake kutumia uweledi.
“Marehemu alikuwa ni mtendaji mkubwa kwetu, tukiendeleze kituo chetu kwa pamoja, ili kituo kiweze kusonga mbele zaidi na daima akituhimiza kazi”, walisema.
Mkuu wa chuo cha TSJ Pemba Suleiman Rashid Omar, amesema marehemu alishaonyesha kufika mbalia kwenye sekta ya habari tokea alipokuwa akisoma habari chuoni hapo ngazia chetu.
Hata hivyo Afisa Mdhamini wizara ya habari, utamaduni, utalii na Michezo Pemba Khatib Juma Mjaja, aliiomba familia ya marehemu kuwa wastahamilivu katika kipindi hichi kigumu.

Marehemu Seif Hassan Mohamed “albajun’ alizaliwa mwaka 1993 Wilaya ya Mkoani, na kupata elimu yake ya msingi skuli ya Ng’ombeni na elimu ya sekondari skuli ya Uweleni Mkoani, marehemu hadi anafikwa na mauti alikuwa ni Mwanafunzi wa Chuo cha Uandishi wa habari Time School and Journalism Chake Chake Pemba mwaka wa mwisho na msemaji mkuu wa redio Jamii za Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.