Habari za Punde

Makamba awabeba vijana Unguja UkuuNa Salum Vuai, MAELEZO

WAZIRI wa Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia mambo ya muungano Januari Makamba, ameyachangia mabaraza ya vijana Unguja Ukuu shilingi milioni tatu na kuyataka yaelewe kuwa mustakbali wa taifa la Tanzania umo mikononi mwao.

Makamba, alikuwa akizungumza na vijana wa shehia tatu za kijiji cha Unguja Ukuu wakati wa uzinduzi wa mabaraza ya vijana wa shehia hizo uliofanyika juzi katika uwanja wa mpira wa Tindini katika jimbo la Tunguu Wilaya ya Kati.

Mabaraza yaliyozinduliwa ni yale ya shehia za Kaepwani, Tindini na Kaebona.

Hata hivyo, Waziri huyo aliyepangwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi huo, aliwahutubia vijana hao kwa kuunganishwa na teknolojia ya mtandao akiwa mjini Dodoma ambako ametingwa na vikao vya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Makamba aliwataka vijana hao kutojiingiza katika siasa chafu zinazoweza kuwafarakanisha na kurudisha nyuma jitihada zao na za serikali katika kuleta maendeleo nchini.

Badala yake, aliwaeleza kuwa siasa nzuri ni zile zilizojikita katika kuwaunganisha watu, kuimarisha upendo, na kujenga taifa kwa lengo la kuwakomboa na umasikini.

Waziri huyo pia aliwashauri vijana kutoendekeza mihemko kwa kujiingiza kwenye vitendo viovu ikiwemo biashara au matumizi ya dawa za kulevya, uvutaji bangi, uasherati na uporaji, ambavyo alisema havina hatima njema kwao na kwa taifa.

Alieleza kuvutiwa kwake na ubunifu wa vijana hao katika kujishughulisha na miradi mbalimbali ya kuwaendeleza kimaisha na kuahidi kuendelea kuwaunga mkono ili kuhakikisha wanafikia malengo yao.

Mapema, Mwakilishi wa jimbo la Tunguu Simai Mohammed Said, na kwa niaba ya mbunge Khalifa Salum Suleiman, aliwapongeza vijana hao kwa kuitikia wito wa serikali kuunda mabaraza yao ambayo ndiyo njia inayoweza kuwainua.

Aliwahakikishia kuwa viongozi wa jimbo wako pamoja nao kwa kuwasafishia njia ya kutimiza mipango yote ya maendeleo wanayoipanga, huku akiwataka wasiyumbishwe  na watu wasiokuwa na nia njema, ambao wamelenga kuwarejesha nyuma.
Aidha aliyachangia mabaraza hayo kwa pamoja shilingi laki tano.

Katika risala yao, vijana wa mabaraza hayo walisema wamejidhatiti kuupiga vita umasikini kwa kuanzisha miradi mbalimbali ikiwemo ufugaji nyuki, kuku, mbuzi na ng’ombe, pamoja na kilimo ingawa wanakabiliwa na changamoto kadhaa za uhaba wa vitendea kazi walizoomba wasaidiwe kuzipatia ufumbuzi.


Hafla ya uzinduzi huo iliyopambwa kwa burudani za sarakasi, muziki, tenzi, ngongoti na maigizo, ilihudhuriwa pia na Mkuu wa Wilaya ya Kati Mashavu Sukwa Said, madiwani wa wadi za jimbo la Tunguu, masheha na wananchi mbalimbali.  

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.