Habari za Punde

Timu za Kaskazini Kuzindua Msimu Mpya wa Ligi.

Msimu mpya wa ligi kuu ya soka Zanzibar unatarajiwa kuanza rasmi Oktoba 2 mwaka huu wa 2016 huku vilabu 36 vikishiriki ligi hiyo kwa mgawanyo sawa wa timu 18 kwa visiwa viwili vya Unguja na Pemba.


Kamati inayosimamia mashindano ya Chama cha mpira wa miguu Zanzibar chini imekaa na vilabu 18 vya Unguja kujadili hali halisi ya ligi hiyo.

Katika kikao hicho viongozi wa vilabu pamoja na ZFA kulitolewa maamuzi ya kuanza msimu mpya wa ligi kwa kutumia viwanja viwili.

Kwa mujibu wa ratiba ambayo itatolewa rasmi Alhamis ya wiki hii timu ya Mundu ndiyo itakayofungua pazia la ligi hiyo kwa kucheza na jirani zao Kimbunga wote kutoka wilaya ya Kaskazini A kisiwani Unguja.

Pambano hilo litachezwa majira ya saa nane mchana uwanjani Amaan huku pia Sikh hiyo ya Oktoba 2 kukiwa na michezo mengine miwili.

Mara baada ya pambano hilo Zimamoto ambao ni mabingwa wapya wa ligi hiyo watawaalika mabaharia weusi, Black Sailor wakati wa saa kumi huku kwenye dimba la Ngome Fuoni timu ya Kijichi itapambana na JKU.

Kwa upande mwengine kikao hicho kimeamua pambano la ngao ya hisani ambalo huashiria kuanza kwa msimu mpya wa ligi kuchezwa September 26 kati ya Zimamoto dhidi ya timu ya Chwaka.

Hata hivyo endapo timu ya Chwaka itashindwa kuchuana na Zimamoto fursa hiyo itaangukia kwa timu ya Taifa ya Jang'ombe ambayo ilishika nafasi ya pili kwenye msimamo wa kupanda daraja.

Ligi hiyo inaingia kwenye mchakato wake huku bado chama cha soka Zanzibar kikihaha kutafuta udhamini wa kuvisaidia vilabu vyake.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.