Habari za Punde

SMZ:Hakuna Ubaguzi katika Nafasi za Kazi

Na Salmin Juma Pemba.
Serikali ya Mapindunzi ya Zanzibar imesema hakuna upendeleo katika kutoa nafasi za ajira za Idara za Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania,ikiwemo Jeshi la Wananchi na Polisi bali zinatolewa kulingana na sifa ya muombaji.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais Zanzibar Mhe Mohammed Aboud Mohammed ameyasema hayo jana alipokuwa akijibu suali aliloulizwa na waandishi wa habari kwenye mkutano wake na vyombo vya habari uliofanyika chake chake kisiwani Pemba.

Katika suali lake mwandishi wa habari Suleiman Rashid Omar alitaka kujua Serikali inachukua hatua gani kuondoa upendeleo katika kutoa ajira kwa idara za muungano ambazo wananchi kisiwani Pemba wanadai kwamba nafasi zinazoletwa zinaporwa na kupewa vijana wanaotoka unguja.

Waziri Aboud alisema serikali ya jamuhuri ya muungano imekua ikitoa nafasi za ajira katika idara zake kwa mikoa yote ya Zanzibar, kila mkoa kufikisha majina ya vijana ambao ni wakaazi wa mkoa huo na sio vyenginevyo.

Alifahamisha kua, ajira zinazotangazwa ni chache na wanaojitokeza kuomba ni wengi hivyo kunakuwako na uchambuzi wa kina katika kufanya maamuzi ya kuchagua vijana wa kujiunga na idara hizo kwa kufikia vielelezo vya kila mmoja.

Aidha Waziri Aboud alikiri kuwepo na idadi kubwa ya vijana wasio kuwa na ajira unguja na pemba na kufahamisha kwamba serikali imeanza kuchukua hatua za makusudi kulitafutia ufumbuzi swala hilo.

Alieleza kuwa miongoni mwa mikakati hiyo iliyoandaliwa na serikali na ambayo  imeanza kutekelezwa ni kuahamasisha wawekezaji kuekeza katika sekta ya kilimo ,uvuvi na utalii ili  vijana waweze kupata ajira na kupunguza ukali wa maisha katika familia zao.

Aliongeza kuwa kupitishwa kwa sheria mpya ya mafuta na gesi itafungua milango kwa wawekezaji kuwekeza mitaji yao na hivyo kutoa fursa kwa vijana kupata ajira pamoja na kupatikana soko la bidhaa la wajasiriamali wadogo  wadogo.

“kupitishwa kwa sheria mpya ya mafuta na gesi kutafungua milango ya uwekezaji pamoja na kuzalisha ajira kwa vijana na kutanuka soko la bidhaa za wajasiriamali wadogo wadogo  na wakati “alieleza.

Hivyo alisisitiza kuwa serikali imepanga kuziendeleza fursa ambazo bado hazijatumika kwa maslahi ya taifa kwa kuziboresha ili zilete tija kwa umma na taifa kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.