Habari za Punde

Wafanyabiashara za Hoteli Pemba Watakiwa Kudhamini Bidhaa za Ndani, - Katibu Mkuu Kilimo.

Na Salmin Juma Pemba.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo , Maliasili , Mifugo na Uvuvi Zanzibar Mh Juma Ali Juma amewataka wamiliki wa mahotel ya kitali na wafanyabiashara wengine kisiwani Pemba kununua bidhaa zinazozalishwa na wajasiriamali nchini.

Amesema ndani ya zanzibar kuna wajasiriamali mbalimbali wanaojali na kuthamini kazi zao ambao huzalisha bidhaa madhubuti, nzuri na za kuaminika ikiwamo wazalishaji wa bidhaa ya mayai.

Katika kutilia mkazo suala hilo amesema kisiwa cha Pemba ni moja kati ya maeneo mazuri ambayo bidhaa ya mayai huzalishwa kwa wingi na ni yenye ubora wa kuaminika, amesema sivyema kwa wafanya biashara kanunua mayai kutoka nje wakati Pemba yapo ya kutosha na mazuri katika matumizi.

Kauli hiyo ameitoa wakati wa ziara ya kutembelea wafugaji wa kuku katika shehia ya Ziwani wilaya ya chake na kuona hali ya mrundikano wa mayai kwa wingi yaliokosa soko kwa wafugaji hao.

Amesema wizara itaandaa utaratibu maalum ili kuhakikisha mayai kutoka nje ya Pemba wanayazuia ili wafugaji kisiwani pemba waweze kupata soko lao la ndani.

Aidha katibu mkuu amewataka wafugaji hao wa kuku kutovunjika moyo bali waendelee na kazi ya kuzalisha mayai kwa wingi kwani Serikali inathamini juhudi na mchango wao katika mapambano dhidi ya adui maskini.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Chake Chake Salama Mbarouk Khatib kwa niaba ya wezake amesema kwamba Serikali za Wilaya zitahakikisha zinashirikiana na Wizara hiyo ili kuona kwamba mayai yote yanayozalishwa na wafugaji kisiwani pemba yanauzwa.

Mmoja wa wafugaji Soud Ali Said akizungumza kwa niaba ya wafugaji wenzake alimwambia Katibu mkuu kuwa ukosefu wa soko umepelekea pia mifugo yao kuathirika na maradhi na njaa kutokana na wafugaja kukosa fedha za kununulia mahitaji hayo .

Hata hivyo katika ziara hiyo zaidi ya trea mia tisa za mayai zimeweza kununuliwa na wizara ya kilimo Maliasili ,Mifungo na Uvuvi zanzibar kwa lengo la kuasaidia wafugaji hao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.