Habari za Punde

Umeme Juu Zanzibar kwa asilimia 20.

Shirika la umeme Zanzibar ZECO limeamua kuongeza bei ya kuuzia umeme kwa asilimi 20 kuanzia leo.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari, Waziri wa ardhi, maji, nishati na mazingira, Bi Salama Aboud Talib akitangaza mabadiliko ya bei hizo, amesema watumiaji wa majumbani wenye uwezo ambao wanatumia hadi uniti 50 sasa watanunua umeme kwa shilingi 79 kwa uniti  badala ya bei ya zamani ya shilingi 66.

Amesema watumiaji wanaozidi uniti 51 sasa watalipa shilingi 480 kwa uniti badala ya shilingi 400 walizokuwa wakilipia.

Aidha amesema watumiaji wa kawaida wa huduma za jamii ambao wanatumia uniti moja hadi 1,500 sasa watanunua uniti moja ya umeme kwa shilingi 266 badala ya shilingi 222.

Amesema watumiaji watakaozidi uniti 1,500 watalipia umeme kwa shilingi 288 badala ya bei ya zamani ya shilingi 240 kwa uniti,watumiaji wa viwanda vidogovidogo  watalipia shilingi 206 kwa uniti badala ya bei ya zamani ya shilingi 172.

Amesema kwa watumiaji wa viwanda vikubwa itakuwa shilingi 169 kwa uniti badala ya shilingi 141 na taa za njiani ambapo bei ya zamani ilikuwa shilingi 222 kwa uniti bei mpya kwa sasa itakuwa shilingi 266 kwa uniti.

Hata hivyo waziri huyo amesema serikali imezingatia mabadiliko hayo na hali ya maisha ya wananchi wake na sekta yengine ili kuepusha kuwabebesha mzigo mkubwa wa maisha.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.