Habari za Punde

Hii ni michezo ya kiislamu au ya kuudhalilisha Uislamu?

Na mwandishi wetu

Katika miaka ya hivi karibuni kumekua na mapinduzi yanayoendelea kukua kwa kasi ya ajabu katika uandaaji na utengenzaji wa filamu au hata maigizo yanayoitwa ya kiisilamu.

Katika filamu hizo kumekua na juhudi za makusudi kufikisha ujumbe wenye  kuaendana na mazingira ya kiisilamu ikiwa lengo lao kuu ni kuwafundisha wanajamii juu ya yale yatendekayo kinyume na dhana ama fikra ya kiisilamu inavyotaka, hakika ya hilo ni jambo jema ila sijui kwakua simweledi wa kupitiliza kama walivyowengine nahisi hata kama nia ni njema, lakini tatizo kati yake linaweza kuzaliwa tena likapiliza faida inayotarajiwa.

Kwakua si mweledi kama nilivyokwishatangulia kusema huko juu, hivyo sitaogelea sana katika mawanda ya lugha bali naandika japo tu kidgo ilhali  nami niwe miongoni mwa waliyozungumza juu ya kadhia hii.

Hivyo napenda kukutanabahisha mapema, katika maelezo haya mafupi utakayoyasoma sitaraji kama utapata ufasaha wa kiswahili sanifu katika lugha ama utapata mtiririko maalum wa kupangilia vina, maneno na  tungo ila utapata kujua nini nakusudia, nikiamini ninachokiandika kinafahamika, nimesema hayo kwakua sijajikita zaidi kuandika katika mtindo wa kuridhisha wanafasihi.

Sasa nikiingia mojamoja kwamoja katika hoja ambayo ni hizi filamu zinazoitwa za dini ya kiisilamu lengo lao ni kufunza lakini vipi utafunza, leo hii anaonekana mwanamke aliyejinasibisha na uisilamu anacheza (kuigiza) kama mama wa kiisilamu katika filamu hizo lakini mtazame uisilamu wake katika filamu hiyo  ni kwenye maneno tu ayatamkayo na si kwengineko, kama vile kivazi, mwendo na hata maumbile.

Nakusudia kusema, mama huyo wa kiisilamu anefunza umma katika kioo cha runinga anaonekana amepara nyusi zake zote na hana zaidi ya kope la wanja ilililotanda jichoni, jee huu ndio uisilamu au uisilamu ni kauli tu? 

Nimeamua kuandika haya kwa mtindo wa kuuliza najua karne hii ya 21 imeshamiri magwiji na wataalamu katika tasnia ya filamu(za kiisilamu) naomba nipatiwe majibu pengine nitafaidi mie na wengineo.

Tasnia hii ya filamu kipindi hiki imekua zaidi kule kwa wenzetu Tanzaniabara, naweza kusema humalizi nyumba saba mpaka nane basi moja itakua na msanii ndani ambae baadae anatarajiwa kucheza filamu za dini tena ya kiisilamu.

Kubwa jengine la kushangaza na kushtusha, wasanii wetu wa sasa tumekua tukiwaona leo anaigiza filamu za kiisilamu kesho nyimbo keshokutwa vichekesho , si vibaya lakini jamii hasa vijana unawafunza nini.

Umeamua unaekti filamu za dini basi fanya dini usichanganye watu watashindwa kutambua wafuate wapi,utawachanganya wafuasi wako mwisho watakorogeka na hatimae jamii itayachukulia haya kama ni utani na hakuna llte la maana na ndio kama muda huu sasa.

Napenda nilieleze hili kiunagaubaga ingawa nitarudia ya awali lakini yanahaki ili nieleweke kile nilichokikusudia na  sitotaja jina la muhusika wenyewe lakini mazingira yapo wazi utaelewa tu, Tanzania yetu ni ya vichekesho sana eti unamuona mtu anacheza filamu ya dini hivyohivyo kidogo lakini tutasema ndio ameshajisitiri, watoto, vijana na wazee wanainua mikono juu kwa alivyocheza vizuri na kusikitisha umma pale alipoonesha huruma na mapenzi juu ya kitu fulani lakini miezi miwili baadae yule tuliyemuona aliyejisitiri katika filamu ya dini tunamuona tena kwengineko katika hizo za kawaida, mithili ya mnyama porini, kivazi hakitambuliki, manyewele timutimu pengine mkononi anachupa la pombe akilibwiya, umekubali kua msanii lakini jamii ikufahamu vipi, wale waliokuona umesitirika awali wakuseme vipi, ni ipi nafasi ya dini katika maigizo yako, wajuzi wa mambo twambieni  hapa si kuucheza shere uislamu ?

Tuachane nako uko tutazame hili, hata kama ni kuigiza lakini usilamu hauwezi kuhalalisha jambo ambalo ni haramu pasipo na udharura wa lazima, eti leo unalala na mwanamke kitanda kimoja kwa kuigiza tu, wengine hushikana shikana kitandani na kupapasana kisa kuigiza tu, weledi twambieni hapa vipi ?

Hakuna jambo baya sana katika usilamu kama mwanamke kuonekaana nywele zake, tazama leo fialmu hizo za kiisilamu si nywele tu utaona mpaka visivyoonwa (maziwa)

Suala nauliza, wakati filamu hizo zikitengenezwa haziwi na waongozaji (directors) na wasaidizi wake?

Kwa mtindo wa filamu hizi zinavyoonekana kanakwamba msimamizi wake hahusiki kabisa na uisilamu (pengine si waisilamu)

Kwa upande wangu naunga mkono hoja ya maudhui ipatikanayo katika filamu hizi lakini siridhishwi kabisa hata kidogo katika utengenezaji wa filamu hizo hasa muonekano halisi wa wachezaji, ni lazima kuzingatiwe maadili na muonekano wa wachezaji ili kuleta uhalisia wa dini la si hivyo hakuna jengine litakalopatikana zaidi ya kuukafishu uisilamu na ndio linaloonekana tu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.