Habari za Punde

Migomo ya kisiasa Pemba yashusha presha ya wananchi

  • Kisiwapanza, Mgelema bado kuna majipu
  • Mazishi, misiba, harusi, usafiri huria kwa wote

Na Haji Nassor, Pemba
MIGOMO ya kisiasa ilioripotiwa kuanza na kushika kasi mwanzoni mwa mwaka huu kisiwani Pemba, kwa wananchi kutoshirikiana katika shughuli za kila siku, imeripotiwa kutoweka katika maeneo kadhaa kisiwani humo, na kurudi katika uasili wa kushirikiana.
Hali hiyo kwa sasa imeanza kuwa historia katika maeneo hasa ya Mkoa wa kaskazini Pemba, ambako ndiko migomo hiyo ilikokuwa imeota mizizi, iliosababishwa na siuntafahamu ya kisiasa.
Uchunguuzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi, umebaini kuwa kwa sasa wanachama wa chama mapinduzi waliokuwa wahanga wa migomo hiyo, wanaruhusiwa kushiriki katika shughuli za wasiokuwa wanachama wenzao.
Imebainika kuwa, kwa sasa hakuna harusi, msiba wala gari za abiria zinazowabaugua wananchi kwa itikadi za vyama vyao, kama ilivyokuwa miezi sita iliopita.
Mwandishi wa habari hizi, amebaini kuwa gari za abiria zinawabeba wananchi wa aina zote, bila ya kujali itikadi vya vyama wanavyoshabikia, jambo ambalo awali wapo walioshushwa kwenye gari kwa sababu za vyama vyao.
Katibu wa siasa na uenezi wa CCM wilaya ya Micheweni Pemba Maryam Omar Ali, amethibitisha kuwa wanachama wake, sasa hawabaguliwi kwenye shughuli za kijamii.
“Mbona migomo ya kisiasa kwetu kwenye vijiji vingi hasa  cha Kwale, mambo poa, CCM akienda harusi ya CUF wala haulizwi ilikuwaje’’.alisema.
Katibu huyo alisema, hali ilivyokuwa kuanzia mwezi Januari hadi mwezi Mei, ya kubaguana na kupewa majina mabaya, sasa hali afadhali, ingawa kijiji cha Kilindini utulivu wa moja kwa moja haupo.
Katibu Mkuu wa chama cha wenye dalala na usafirishaji mkoa wa Kusini Pemba, PESTA, Hafidh Mbaraka Salim, alisema kwa miezi minne sasa, hajapokea taarifa ya madereva kuwabagua wananchi, kwa sababu ya vyama vyao.
“Hata hapo mwanzo kwa kweli madereva hawakuwasusia wananchi, bali wamiliki wa gari wakitaka leta shinda, lakini kwa sasa hakuna hata harufu ya migomo ya kisiasa kwenye usafiri’’,alifafanua.
Mkuu wa Mkoa wa kaskazini Pemba Omar Khamis Othman, alisema hali ya kususiana kwa wananchi kwa sababu ya vyama vyao, imetoweke ndani ya mkoa wake.
“Ilikua, hukai robo au nusu sasa, wasikia mwananchi hakuchukuliwa kwenye gari, nyumba imetiwa moto, mchele hakuuziwa, maiti imesusiwa, lakini sasa twashukuru’’,alieleza.
Katibu wa CUF wilaya ya Chakechake Saleh Nassor Juma, amesema matukio yaliokuwa yakihusishwa na wananchama wao, yamepungua maana wafanyaji walikuwa wakijulikana.
“Hivi sasa pamoja na kwamba serikali iliopo sio ile ya umoja wa kitaifa, lakini hali ndani ya siasa sio nzuri, lakini matukio ya kususiana yamepungua’’,alifafanua.
Katibu huyo amelalamikia tendo la baadhi ya viongozi wake kuendelea kutakiwa kuripoti kituo cha Polisi, kutoka kila siku sasa kuripoti kila wiki.
Uchunguuzi umebaini kuwa, sasa wananchi wote wanaendelea kushirikiana vyema katika kazi na shughuli za kila siku za kijamii kama vile harusi, misiba, ugonjwa na usafiri ambazo zilitoweka kwa miezi kadhaa.
Mwanachama wa CCM na mfanyabiashara wa duka la chakula shehia ya Wara Siti Rashid Salim, alisema aliathirika na migomo hiyo, ingawa kwa sasa hali imeanza kurejea kama kawaida.
“Kabla ya kugomewa nilikuwa nikuza shilingi 150, 000 kwa siku, lakini nilipogomea nikiuza shilingi 10,000, lakini sasa afadhali nafikia shilingi 20,000”,alifafanua.
Nae Aisha Makame Nahoda, alisema hasau alivyofunga biashara yake ya uji na maandazi, kwa sababu ya kugomewa baada ya kushiriki uchaguzi wa marudio.
“Sasa uji wangu nauza kama kawaida, hapa hapana hadithi ya migomo, sasa ni kushughulika na maisha tu, siasa mpaka mwaka 2020’’,alisema.
Sheha wa shehia ya Mgelema wilaya ya Chakechake Omar Idd, amesema kwenye shehia yake bado baadhi ya familia hazijachana kususiana moja kwa moja.
“Sasa migomo ya kisiasa iliopo ni baina ya ndugu na ndugu, lakini ile ya jumla jumla imepungua, maana CCM na CUF wafanyiana shughuli zao kama za harusi”,alifafanua.
Ingawa mwananchi mmoja ambae hakutaka jina lake lichapishwe gazeti, mkaazi a shehia hiyo, alisema hali mbaya ya kisiasa kijijini kwao, ndio kwanza imeibuka upya na hasa baada ya vijana kadhaa kufikishwa Polisi kwa tuhuma za kukata mikarafuu.
“Mbona Mgelema sisi tokea mwanzo hatukuathiriwa na migomo ya kisasa, lakini baada ya watu wasiofahamika kukata mikarafuu ya Mhe: Said Soud, ndio ilioibua siuntafahamu baada ya kulala Polisi vijana wetu’’,alisema.
Aidha sheha wa shehia ya Kanganani Fakih Omar Yussuf, ambayo shehia yake ilikumbwa na janga la nyumba mbili za wananchi kuchoma moto mwezi Machi mwaka huu, alisema hali sasa imetulia.
“Hakuna tena migomo ya kisiasa wala suala la kukatiana vipando, kama ilivyokuwa baada ya uchaguzi wa marudio Machi 20 mwaka huu, shehia imetulia’’,alifafanua.
Sheha wa shehia ya Kojani wilaya ya Wete, Hamad Ali Bwakame, alisema migomo iliokuwepo kwenye shehia yake haikuwa ya harusi na misiba, bali ilihusiana na kuvuushwa kwa vidua, ambapo kwa sasa imerejea vyema.
“Sasa hakuna mwanaccm anaebaguliwa kwa kupanda mtumbwi, wananchi wameshazika tofauti zao na shughuli zinaendelea kama kawaida’’, alifafanua.
Nae sheha wa shehia ya Kisiwa Panza wilaya ya Mkoani Chumu Abdalla Abdalla, alisema ndani ya shehia yake bado migomo ya kisiasa ipo kama kawaida, hasa kwenye usafiri wa mitumbwi.
“Mimi mwenyewe juzi nilishushwa kwenye mtumbwi, wakati naenda Mkoani kikazi, lakini hata kwenye harusi ukibainika wewe ni CCM, wengine wanakutenga, hivyo hali bado’’,alifafanua.
Mwenyekiti wa CUF wilaya ya Mkoani Rashid Saleh Mohamed, alisema taarifa ya Kisiwa Panza, kwamba CUF hawawavuushi wana CCM, anaifahamu vyema ingawa alisema hilo ni zaidi ya siasa.
“Kuna maneneo walisema kwamba, wakipanda mitumbwi watajiangusha ili, kisha akamatwe nahoza na ndio maana wanaogopa kuwachukua CCM’’,alisema .
Aidha Mwenyekiti huyo alisema kuendelea kushikiliwa kwa madau mawili na mashuwa moja ya wananchi wa Kisiwa Panza na uongozi wa wilaya, kunachangia wananchi hao kushindwa kuelewana.
Mwanachama wa CUF Saada Khalfan Juma wa kijiji cha Chanjamjawiri wilaya ya Chakechake, alisema migomo imeondoka, maana ilikuwa ni hatua moja kwao kuonyesha kutoridhishwa kwa kuchezewa kwa demokrasia.
“Suala la miogomo ama kutoshirikiana na wanaccm, ni hatua moja, ya pili viongozi wa chama changu wanaendelea kusaka haki yetu’’,alisema.
Nae Biubwa Hassan Mwalimu (CUF) alisema, suala la kutoshirikiana na wafuasi wa vyama vyengine kwa wakati huo, lilikuwa ni agizo la baraza kuu la chama chao.
Mwanachama wa CCM, Asha Sineni Mjaka wa kijiji cha Uwandani, alisema yeye binafsi ameshashiriki harusi na misiba ya wafuasi wa CUF, bila ya kusumbuliwa.
“Hata juzi mimi nilialikwa harusi na jirani yangu ambae ni CUF na nikashiriki mwanzo mwisho, ni ishara sasa migomi imezikwa Pemba’’,alifafanua.
Nae Kamanda wa Polisi Mkoa wa kaskazini Pemba Haji Khamis Haji, alikiri kutoweka kwa matendo ya migomo na kuharibu vipando, kama ilivyoku hapo kabla.
Alieleza kuwa miezi sita iliopita, jeshi lake lilikuwa na kazi saa 24 kusaka wahalifu wa matukio mbali mbali, ambapo kwa sasa mkoa uko shuwari.
“Sasa hali imetuliwa, na nadhani ni kule kushikiliwa kwa wathumiwa na tayari wananchi wamepata taaluma, juu ya athari za kufanya uhalifu na kugomeana, kama walivyoeleza baadhi ya viongozi”,alifafanua.
Mwananchi Hassan Kombo Juma wa Mkoani, alisema hata wao kwa sasa wanafanya shughuli zao za kujieletea maendeleo hasa wao wanafanya kazi nyakati za usiku.
“Mimi nafanyakazi bekari ya mikate, lakini kipindi kile cha mshike mshike, nilikuwa kazini naenda mchana tu kwa kuogopa kuingizwa kwenye wahalifu, lakini sasa shuwari’’,alifafanua.
Katika kipindi cha mwezi wa Machi hadi Mei mwaka huu, Jeshi la Polisi kisiwani Pemba, liliripoti matukio 21 ya uhalifu, ikiwemo kuchoma nyumba moto, kukatwa mikarafu 430, huku watuhumiwa 26 wanaokabiliwa na tuhuma hizo walifikishwa mahakamani.

Hali ya siuntafahamu baina ya baadhi ya wafuasi vyama vya CCM na CUF, iliibuka tokea mwezi Oktoba mwaka jana, baada ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar ‘ZEC’ kuyafuta matokeo ya uchaguzi mkuu, kwa sababu za kutawaliwa na ghilba.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.