Habari za Punde

Watoto 541 Hawakufanya Mitihani yao ya Darasa la Nne.

Na salmin Juma. Pemba. 

MITIHANI ya darasa la nne iliyofanyika hivi karibuni visiwani hapa imegeuka na  kuwa kaa la moto kwa walimu wakuu pamoja na wajumbe wa kamati za skuli Wilaya ya Micheweni baada ya kubainika kuwepo wanafunzi 541 hawakufanya mitihani hiyo .

Wanafunzi   waliotarajiwa kufanya mitihani hiyo  katika skuli 19 za msingi zilizomo katika  Wilaya  hiyo  ni 2728 ambapo kati ya hao wanawake ni 1415 na wanaume ni 1313, lakini  ni wanafunzi 2187 ndio waliofanya mitihani iliyofanyika Novemba  16-17 mwaka huu .

Hali hiyo imemfanya Mkuu wa Wilaya hiyo Abeid Juma Ali kutoa wito kwa walimu wakuu wa skuli za msingi  na kamati zao za skuli kufanya uchunguzi wa kina na kuwasilisha taarifa Ofisi ya Elimu Wilaya  kubainisha walipo wanafunzi hao pamoja na sababu zilizosababisha wasifanye mitihani hiyo.

Akizungumza na walimu wakuu na wenyeviti wa kamati zao za skuli katika ukumbi wa skuli ya Chwaka Tumbe , alisema Serikali ya Wilaya imesikitishwa  kwani  wanafunzi hao wamekosa haki yao ya msingi .

Mkuu huyo wa Wilaya ameahidi kuchukua hatua kwa yoyote atakaye bainika kuhusika na utoro huo ikiwa ni pamoja na kumuwajibisha kwa mujibu wa sheria za nchi .

Alisema   serikali inatumia fedha nyingi kuandaa mitihani hiyo na hivyo kitendo cha baadhi ya wanafunzi kushindwa kwenda kufanya mitihani ni kuisababishia harasa kwa kuwa mithani hiyo iliandaliwa kulingana na idadi ya wanafunzi waliosajiliwa .

“Serikali ya Wilaya imeshtushwa sana na taarifa hizi kwani idadi ya wanafunzi 541 , nimemwagiza Afisa Elimu Wilaya kwa kushirikiana na walimu wakuu kuwalisha taarifa sahihi pamoja na sababu zilizosababisha wanafunzi hao kutofana mirihani hiyo ”alisema .

Alifahamisha walimu wanajukumu lako , wazazi nao wanajukumu na serikali nayo inajukumu lake , hivyo kunahitajika ushirikiano wa  pamoja  ili kudhibiti suala la utoro pamoja na kuboresha kiwango cha elimu hapa nchini .

Naye Afisa Elimu na Mafunzo ya Amali Wilaya hiyo Mbwana Shaame alisema , wizara imekuwa ikifanya ziara za mara kwa mara katika skuli kuhamasisha maendeleo ya elimu kwa wanafunzi na kuongeza wanaostahili kubeba lawama ni wazazi .

Alisema kuwa baadhi ya wazazi hawana utamaduni wa kufuatilia maendeleo ya watoto wao skuli na kwa wazazi wa aina hiyo ni vigumu kuweza kuwahimiza watoto wao kwenda skuli .

“Walimu wanafanya kazi kubwa kuwahamasisha wanafunzi kuhudhuria masomo  lakini kikwazo kikubwa ni kwa baadhi ya wazazi kutokuwa na utamaduni wa kufuatilia maendeleo ya watoto wao  ”alifahamisha. 

Aidha Mbwana alisema Skuli ya Msingi Micheweni ambayo ipo centre ya Wilaya inaongoza kwa utoro wa wanafunzi ambapo jumla ya wanafunzi 122 kati ya 300 hawakufanya mitihani hiyo ikifuatiwa na Tumbe iliyokuwa na wanafunzi 287 huku 80 hawakufanya mitihani .

Mmoja wa wadau wa elimu katika wilaya hiyo alisema kwamba walimu hawapaswi kulauminiw akwani wamefanya kazi ya ziada kuwahamasisha wanafunzi kuhudhuria mitihani hiyo .

 Vipo viashiria ambavyo vinaweza kuwa ni sababu ambayo inapelekea ongezeko la utoro wa wanafunzi katika Wilaya hiyo miongoni wa sababu hizo ni uchimbaji wa mawe , upazaji wa samaki bandarini , kilimo cha mwani pamoja na biashara ndogo ndogo .

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.