Habari za Punde

Ahukumiwa miaka 6 jela kwa shambulio la aibu

Na Salmin Juma, Pemba

MAHAKAMA ya Mkoa Wete imemhukumu kwenda chuo cha Mafunzo kwa kipindi cha miaka sita (6) Muslih Mserembwe Omar (55)  mkaazi wa Kidutani Shehia ya Gando baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la shambulio la aibu .

Mzee huyo  amepatikana na hatia hiyo kufuatia kitendo cha kumvua nguo ya ndani msichana mwenye umri wa miaka kumi na mbili (12) jina linahifadhiwa jambo ambalo ni kinyume na sheria chini ya kifungu cha 131 (1) cha sheria namba 6 ya mwaka  2004 .
Mbele ya Hakimu wa mahakama hiyo Makame Mshamba Simgeni , mwendesha mashtaka kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa mashtaka wa Serikali Ali Bilali ameiambia mahakama kuwa Mserembwe ametenda kosa hilo Novemba 26 mwaka 2013  sheria za Zanzibar .

Amesema siku ya tukio huko Kidutani Gando , majira ya saa 12:15 za asubuhi , bila ya halali na kwa njia ya aibu Mserembwe alipatikana na kosa hilo na kumfanyia kitendo cha aibu msichana huyo kwa kutekeleza tendo la kumvua nguo ya ndani .

Awali Mserembwe alifikishwa katika mahakama hiyo akikabiliwa na makosa mawili tofauti , ambapo kosa la kwanza ni la shambulio na aibu , huku kosa la pili ni kutorosha msichana mwenye umri wa miaka 12 kinyume na kifungu cha 130 (a) cha sheria namba 6 ya mwaka 2004 sheria za Zanzibar.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka iliyowasilishwa mahakama hapo ilisema kwamba siku ya tukio , mtuhumiwa alimtorosha msichana huyo kutoka nyumbani kwa wazazi wake na kumpeleka nyumbani kwake hali akijua kwamba ni kosa kisheria .

Akisoma hukumu kwa mshtakiwa iliyochukua muda wa dakika 60 , hakimu wa mahakama hiyo Makame Mshamba Simgeni , alimtia hatiani kwa kosa la kwanza la shaambulio  la aibu huku akimwachia huru kwa kosa la pili la kutorosha .

Mbali na hukumu hiyo , pia mahakama imemtaka Mserembwe kulipa faini ya shilingi laki tano (500,000) ambazo zitakwenda kwenye mfuko wa Serikali pamoja na kulipa fidia ya shilingi laki nne (400,000) kwa mwathirika .

1 comment:

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.