Habari za Punde

Ziara ya Waziri Mhagama Bagamoyo.

Na Daudi Manongi. Maelezo Dae es Salaam.
Bagamoyo
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera,Bunge,Kazi,Vijana,Ajira na Walemavu Mhe.Jenista Mhagama amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Bw.Majid Mwanga kuhakikisha ana tatua mgogoro wa  ujenzi wa barabara ya Kiwangwa-Mabohelo  yenye urefu wa kilomita 15 na kumalizika mwishoni mwa mwezi huu.

Ameyasema hayo jana Wilayani  wakati alipotembelea  miradi inayotekelezwa na Halmashauri  ya Wilaya ya Chalinze na Bagamoyo  kwa ufadhili wa Programu ya  Miundombinu ya  Masoko, Uongezaji Thamani na Huduma za Kifedha Vijijini(MIVARF)  inayosimamiwa na chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

“Serikali ya Awamu ya Tano ina lengo kubwa la kuwasaidia wananchi hususani wakulima ili wafikiwe na miundombinu ili kupambana na umaskini na kuboresha masuala ya masoko yao na hivyo kuwaongezea kipato”, Alisema Mhagama.

Aidha Mhe. Mhagama alisema kuwa asili ya miradi ya ufadhili wa Programu ya Miundombinu ya  Masoko, Uongezaji Thamani na Huduma za Kifedha Vijijini (MIVARF) iliyo  chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu haina fidia hivyo  anashangaa kuona ni kwanini ujenzi vipande hivyo vitatu vya barabara vinachelewa kukamilika hadi kufikia leo.

Ameongeza kuwa pesa za kumalizia mradi huo zipo na kusema kuwa tatizo kubwa lililopo ni kukosekana kwa mawasiliano kati ya Halmshauri za Bagamoyo na Chalinze na kuwaagiza Viongozi wa Halmashauri hizo chini na kumaliza mgogoro huu mara moja ili  wananchi wafanikishe lengo kuu la mradi huo ambao ni umwagiliaji.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Chalinze Mhe.Ridhiwani Kikwete alisema kuwa tatizo kubwa  linalofanya mradi huo kutokamilika ni kutoshirikishwa kwa wananchi  na kuitaka halmashauri ya Bagamoyo kukaa pamoja na wao ili kupata ufumbuzi wa kudumu.


Naye Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Bw.Majid Hemed Mwanga aliahidi kulipatia ufumbuzi tatizo la mgogoro huo ndani ya muda alioagizwa  kwa kuwashirikisha madiwani wote.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.