Habari za Punde


Na Othman Khamis OMPR 


Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeithibitishia Kampuni ya Kimataifa inayotoa huduma  za Kijamii { Avic international } ya Nchini Jamuhuri ya Watu wa China kuipa msukumo na ushirikiano wa karibu katika azma yake  iliyokusudia ya kutoa huduma  Visiwani Zanzibar.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alitoa uthibitisho huo wakati wa mazungumzo yake na Uongozi wa Kampuni hiyo kwenye Makao Makuu yake Mjini Beijing Nchini China.

Balozi Seif anayeuongoza Ujumbe wa Viongozi Wanne wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar akimalizia ziara yake  ya siku Tano Nchini China alisema Avic International imeonyesha  muelekeo mzuri wa kutaka kusaidia Maendeleo ya Wananchi wa Zanzibar hasa kwenye kundi kubwa la Vijana.

Alisema mipango ya Kampuni hiyo katika kushirikiana na Mamlaka ya Maji Zanzibar kwenye uimarishaji wa  mbiundombinu ya huduma za Maji  Mfenesini na Dimani, kuvipa msukumo Vituo vya Amali, huduma za Viwanja vya Ndege pamoja na usambazaji wa vifaa vya Electron ni dalili za wazi zinazoonyeshwa na Avic kukusudia  kustawisha Maendeleo ya Watu wa Zanzibar.

Balozi Seif alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hivi sasa imejikita katika kuvijengea uwezo wa vifaa na Walimu vituo vyake ilivyoanzisha Unguja na Pemba ili kuwapa fursa Vijana kujipatia Taaluma zitakazowawezesha hapo baadaye kujitafutia riziki kwa kujiajiri wenyewe.

Aliueleza Uongozi wa Kampuni hiyo ya Avic kwamba Zanzibar imekuwa ikizalisha  kundi kubwa la Vijana wanaomalioza masomo yao ya Sekondari ambao kutokana na ufinyu wa ajira Serikalini ni vyema ukawepo utaratibu mzuri wa kuandaa waingie kukabiliana salama na maisha yao ya baadaye.

Mapema Makamu wa Rais wa Kampuni ya Avic International Bwana Liu Jun alimueleza Balozi Seif kwamba Kampuni yao tayari imeshafunga mkataba na Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji, Nishati na Mazingira kwa ajili ya kuendesha miradi ya maji katika Vijiji vya Dimani na Mfenesini.

Bwana Liu alisema juhudi zitaendelea kufanywa na Kampuni hiyo katika kuona vituo vya Amali Zanzibar vinapatiwa nyenzo na kuimarishwa kwa lengo la kuwajengea uwezo Vijana wanaomaliza masomo kuata tyaaluma itakayoweza kuwasaidia katika kujiajiri wenyewe.

Alisema kwa vile Kamuni yao imejikita pia kutoa huduma za vifaa vya Kilimo kama Matrekta, Uongozi wao unaandaa mapendekezo yatakayowasilishwa katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa hatua ya kupata kibali kitakachowaruhusu kutoa huduma  ya kusambaza Visiwani Zanzibar.

Bwana Liu Alimueleza Balozi Seif kwamba wataalamu wa Kamuni hiyo tayari wameshafanya utafiti na kugundua  kwamba Zanzibar  bado ina upungufu wa vifaa vya Kilimo ambavyo Taasisi yake inaweza kusaidia kuunguza tatizo hilo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.