Habari za Punde

Rais Dk Shein atoa salamu za mwaka mpya 2017

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  Mhe, Dk. Ali Mohamed Shein alipokuwa akitoa salamu za mwaka mpya wa 2017 kwa wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla, ambapo ameuombea kuwa mwaka wa mafanikio na amani, salamu hizo alizotoa leo katika  ukumbi wa Ukulu Mjini Unguja leo,[Picha na Ikulu.] 31 DISEMBA 2016.



STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
  Zanzibar                                31.12.2016
---
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa uchumi wa Zanzibar umezidi kumeimarika sambamba na Serikali kufanikiwa kuongeza kiwango cha makusanyo ya kodi ambapo kwa kipindi cha Januari hadi Novemba, mwaka 2016 jumla ya TZS bilioni 441.3 zimekusanywa kutoka vyanzo vya ndani.

Dk. Shein aliyasema hayo leo katika risala yake ya kuukaribisha mwaka mpya 2017 aliyoitoa kupitia vyombo vya habari, Ikulu mjini Zanzibar na kusisitiza kuwa hadi kufikia robo mwaka ya pili (April- Juni) mwaka 2016 uchumi umekua kwa kasi ya asilimia 6.2.

Katika maelezo yake, Dk. Shein alisema kuwa kwa kipindi kama mwaka 2015 Serikali ilikusanya TZS bilioni 336.6 ikimaanisha kwamba miezi kumi ya mwanzo ya mwaka 2016, mapato yameongezeka kwa TZS bilioni 104.7 sawa na ukuaji wa asilimia 31.1.

Alisema kuwa sambamba na mafanikio hayo, washirika wa maendeleo wamethamini kazi nzuri inayofanywa na Serikali ya kuwaletea maendeleo wananchi ambapo katika kuthibitisha imani yao kwa Zanzibar, Serikali imepokea jumla ya TZS bilioni 54.53 kutoka kwa Washirika wa Maendeleo kati ya Januari hadi Oktoba 2016.

Dk. Shein alisisitiza kuwa huo ndio ukweli halisi na hio ndiyo hali halisi ambayo ni vyema wananchi wakaifahamu kuwa ni nzuri kinyume na maelezo yanayotolewa na baadhi ya watu ambao hawana taarifa sahihi na takwimu za uhakika za Serikali.

Aidha, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kueleza mafanikio yaliopatikana katika sekta mbali mbali za maendeleo ikiwemo sekta ya afya kwa kuzinduliwa majengo ya wodi mpya ya watoto na wodi ya wazazi katika hospitali kuu ya Mnazi Mmoja pamoja na uzinduzi wa Hospitali ya Abdalla Mzee, Mkoani Pemba baada ya kujengwa upya kwa msaada wa Serikali ya China.

Akizungumzia juhudi zilizochukuliwa na Serikali kuwaenzi wazee, Dk. Shein alisema katika mwaka unaomaliza utekelezaji wa Pencheni ya Jamii ambapo kupitia Mpango huo, wazee wote waliofikia umri wa miaka 70 na kuendelea waliosajiliwa wameanza kupewa posho la TZS 20,000 kwa mwezi.

Kwa maelezo ya Dk. Shein kuanzia mwezi April 2016, utaratibu huo ulipoanza iadadi yao imeongezeka kutoka watu 21,263 waliosajiliwa mwaka 2015 hadi kufikia watu 26,603 mwezi wa Novemba, 2016 huku Serikali ikiangalia uwezekano wa kuwapa wawee kuzia miaka 65 kwa hapo baadae.

Dk. Shein alisema kuwa tukio mahususi katika mwaka unaomaliza lilikuwa ni kutiwa saini kwa Sheria Namba 6 ya Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia ya mwaka 2016 inayoipa Zanzibar uwezo wa kisheria wa kushughulikia utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi.

“ Hadi sasa mipango yetu katika suala hili inaendelea vizuri na tunaendelea na mazungumzo na wawekezaji mbali mbali wenye uwezo mkubwa na uzoefu wa masuala ya mafuta na gesi asilia ambao wana nia ya kuwekeza nchini kwetu”,alisema Dk. Shein.

Aidha, Dk. Shein alisisitiza kauli yake aliyoitoa Disemba 10, 2016 katika maadhimisho ya siku ya Maadili kwenye viwanja vya bustani ya Victoria ya kuwataka viongozi wa umma wanaohusika  kujaza fomu kwa kuzingatia maelekezo yaliotolewa kwenye fomu hio na waepuke kutoa taarifa zisizo za kweli kwani kufanya hivyo ni kitendo cha kuvunja maadili ya uongozi.

Sambamba na hayo, Dk. Shein alieleza juhudi zilizochukuliwa katika kukabiliana na tatizo la ukosefu wa ajira kama ilivyo kwa mataifa mengine duniani na kueleza kuwa katika mwaka 2017, Serikali itajitihidi kuwasaidia wajasiriamali kwa kuwapatia mikopo, masoko ya bidhaa zao na mafunzo na kukiendeleza kituo cha Wajasiriamali kilichopo Mbweni Zanzibar.

Akieleza juu ya amani na utulivu katika kusherehekea mwaka mpya unaoingia, Dk. Shein alisema kuwa Serikali haitosita kumchukulia hatua mtu yoyote au kikundi cha watu kitakachofanya vitendo vinavyohatarisha amani na usalama wa wananchi na mali zo pamoja na wageni wanaoitemebelea Zanzibar.

Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa wananchi wote kushirikiana katika kuvikomesha vitendo vya udhalilishaji kwani ni dhahiri kuwa ufumbuzi wa changamoto hizo unahitaji mchango wa kila mmoja na sio Serikali peke yake.

Pia, Dk. Shein  aliendelea kutoa wito kwa wananchi kwamba kila mmoja ajitahidi kushiriki katika maadhimisho ya miaka 53 ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar, yanayotanguliwa na shamra shamra mbali mbali za uzinduzi wa miradi wa miradi na uwekaji wa mawe ya msingi.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.