Habari za Punde

ZSTC Kupata Cheti Cha Karafuu za Kilimo Hai,Kuuza Katika Soko la Ulaya

Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la ZSTC DR. Said Seif Mzee kushoto na Mwakilishi wa Kampuni ya Ganefryd Bw. Palle Christensen wakitia saini mkataba wa makubaliano ya mashirikiano baina ya taasisi mbili hizo.
Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la ZSTC DR. Said Seif Mzee kushoto na Mwakilishi wa Kampuni ya Ganefryd Bw. Palle Christensen wakikabiziana mkataba wa makubaliano ya mashirikiano baina ya taasisi mbili hizo.

Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC) na Kampuni ya Ganefryd ya Denmark zimetiliana saini mkataba wa makubaliano ya uendelezaji wa Kilimo Hai cha zao Karafuu Zanzibar (Organic Cloves).

Mkataba huo uliosainiwa na Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la ZSTC Dkt. Said Seif Mzee na Mwakilishi wa Ganefryd Bw. Palle Christensen utaliwezesha Shirika la ZSTC kupata cheti cha utambulisho wa Karafuu za Kilimo Hai Zanzibar kuuzwa katika soko la Ulaya.

Akitoa ufafanuzi kwa Waandishi wa Habari juu ya mkataba huo, Dkt. Said alisema makubaliano hayo yataliwezesha Shirika la ZSTC kupata cheti cha utambulisho na kuuza karafuu za Kilimo Hai katika soko la Ulaya.

Dkt. Said alisema kuwa mpango huo utasaidia kutanua wigo wa soko kwa bidhaa za Zanzibar ambapo Wakulima wa Karafuu watanufaika zaidi kwa vile bei ya Karafuu ya Kilimo Hai ipo juu zaidi ukilinganisha na Karafuu za kawaida.

“Tukiwa tunasaini mkataba huu ambao tunaamini utaleta faida kubwa kwa karafuu za kilimo Hai za Zanzibar, tutawahimiza zaidi Wakulima wazalishe Karafuu za Kilimo Hai kwa wingi kwani soko la bidhaa hii kwa nchi za Ulaya ni kubwa”, alisema Dk. Said.
Nae Mwakilishi wa kampuni ya Ganefryd Bw. Christensen alisema ameridhishwa na namna ya Shirika la ZSTC linavyohudumia mazao ya Kilimo Hai na kuahidi kuwa kampuni yake itahakikisha ZSTC inapata cheti cha Karafuu za Kilimo Hai kutoka katika nchi za Ulaya na kuingiza zao hilo katika soko la nchi hizo.

Makubaliano hayo yamekuja wakati ambao Shirika la ZSTC tayari lishapata cheti cha utambulisho cha Karafuu za Kilimo Hai kwa nchi za Afrika Mashariki.

Aidha Serikali pia ipo katika hatua nzuri ya kukamilisha mpango wa kuzifanyia Utambulisho maalum (BRANDING) karafuu za Zanzibar ambapo kukamilika kwa mpango huo kutaongeza thamani na tija ya zao la Karafuu kwa Wakulima na Serikali.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.