Habari za Punde

Hotuba ya Rais Dk Shein katika sherehe za maadhimisho ya miaka 53 ya Mapinduzi ya zanzibar

HOTUBA YA RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA
BARAZA LA MAPINDUZI, MHE. DK. ALI MOHAMED SHEIN,
KATIKA SHEREHE ZA MAADHIMISHO YA MIAKA 53 YA
MAPINDUZI YA ZANZIBAR, AMAAN STADIUM
TAREHE 12 JANUARI, 2017

Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan;
Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,

Mheshimiwa Majaliwa Kassim Majaliwa;
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,

Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi;
Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar,

Mheshimiwa Ali Hassan Mwinyi;
Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
wa Awamu  ya Pili,

Mheshimiwa  Benjamin Wiliam Mkapa;
Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
wa Awamu  ya Tatu,

Mheshimiwa Dk. Jakaya Mrisho Kikwete;
Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
wa Awamu ya Nne,

Mheshimiwa Dk. Salmin Amour Juma;
Rais Mstaafu wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi,


Mheshimiwa Dk. Amani Abeid Karume;
Rais Mstaafu wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi,

Waheshimiwa Viongozi Wakuu Wastaafu Mliohudhuria,

Waheshimiwa Mawaziri wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,

Mheshimiwa Job Ndugai;
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,

Mheshimiwa Zubeir Ali Maulid;
Spika wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar,

Mheshimiwa Othman Chande Mohamed;
Jaji Mkuu  wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,

Mheshimiwa Omar Othman Makungu;
Jaji Mkuu wa Zanzibar,

Waheshimiwa Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa,

Mheshimiwa Ayoub Mohamed Mahmoud;
Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi,

Waheshimiwa Viongozi mbali mbali wa Serikali na Vyama vya
Siasa Mliohudhuria,

Ndugu Wananchi,

Mabibi na Mabwana,

Assalaam Alaikum,

Tuna wajibu mkubwa wa kutanguliza shukurani zetu kwa Mola wetu; Subhanahu Wataala; Muumba wa Mbingu na Ardhi kwa kutujaalia neema ya uhai na uzima, tukaweza kuifikia siku hii ya tarehe 12 Januari, 2017.  Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kuwa pamoja katika  kilele cha Maadhimisho ya miaka 53 ya Mapinduzi  Matukufu ya Zanzibar ya tarehe 12 Januari , 1964.

Kwa niaba ya wananchi wa Zanzibar, natoa shukrani zangu za dhati kwako Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  kwa niaba ya Mheshimiwa Dk. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuungana nasi katika sherehe zetu adhimu na muhimu.  Vile vile, natoa shukrani kwa viongozi wote wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, waliopo madarakani na waliostaafu, Mabalozi wa nchi mbali mbali, Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa, Viongozi wa dini na vyama vya siasa na wananchi wote kwa kuhudhuria kwenu kwenye sherehe hizi.

Mahudhurio yenu makubwa yanatuthibitishia kuwa Mapinduzi yetu yanaheshimika na yanapewa taadhima kubwa ndani na nje ya nchi yetu. Nasema ahsanteni sana kwa mahudhurio yenu.

Ndugu Wananchi,
Leo ni siku muhimu sana katika historia ya wananchi wa Zanzibar, ambapo miaka 53 iliyopita tuliikata minyororo ya utawala wa Kisultani na ukoloni wa Kiingereza uliodumu kwa takriban miaka 132.  Wananchi walikataa kwa vitendo kudharauliwa, kunyanyaswa, kubaguliwa na kutokuheshimiwa katika nchi yao. Chama cha Afro-Shirazi, kiliongoza vuguvugu la kuikomboa Zanzibar, dhidi ya madhila ya wakoloni, mabwanyenye na mabepari. Wananchi walitendewa madhila,walinyanyaswa na walinyimwa haki  kwenye mambo yote muhimu katika maisha yao.

Ndugu Wananchi,
Tunapoadhimisha miaka 53 ya Mapinduzi, tunawakumbuka na kuwashukuru wazee wetu Waasisi wa Chama cha Afro-Shirazi walioongozwa na Rais wake wa Kwanza, Marehemu Mzee Abeid Amani Karume. Daima hatutowasahau kutokana na  ushujaa wao na ushindi wa jitihada zao za kupigania haki, kuleta usawa na maelewano na kuondoa  pingamizi zote walizokuwa wakizipata wananchi wa Unguja na Pemba.  Ni ukweli ulio wazi kwamba Mapinduzi ndiyo yaliyowainua wanyonge, yameleta uhuru wa kweli na yamesimamisha utawala wao katika misingi ya usawa na haki.   Ni kutokana na Mapinduzi, ndipo Wafanyakazi na Wakulima wa Zanzibar walipoirudisha heshima yao na ubinadamu wao katika nchi yao.

Namuomba Mwenyezi Mungu amrehemu Jemadari wa Mapinduzi yetu Matukufu ya tarehe 12 Januari, 1964, Marehemu Mzee Abeid Amani Karume pamoja na waasisi wengine wa Mapinduzi hayo waliotangulia mbele ya haki na awape afya njema na umri mrefu, wale wote ambao bado wapo hai. Siku zote tutawakumbuka, tutawaenzi na tutawaombea dua kwa kujitoa muhanga kwa ajili ya kutukomboa.  Hivi sasa, tupo huru na tunasherehekea miaka 53 ya Mapinduzi yetu tukiwa na mafanikio makubwa.  Tunaahidi kuendelea kuyadumisha na kuyaendeleza malengo ya Mapinduzi yetu Matukufu ya Mwaka 1964. 
Ndugu Wananchi,
Leo tunafikia kilele cha Maadhimisho ya Sherehe za Miaka 53 ya Mapinduzi ya tarehe 12 Januari, 1964 tukiwa na furaha kubwa na kusherehekea kwa vifijo na hoi hoi, kama tunavyojionea wenyewe hapa uwanja wa Amaan. 

Katika kipindi hiki cha miaka 53 ya Mapinduzi,  tunasherehekea kuwepo kwa hali ya amani, umoja, mshikamano na maendeleo makubwa yaliyopatikana.  Kwa hivyo, tuna wajibu mkubwa wa kuuenzi na kuuendeleza umoja na mshikamano wetu ambao ndio siri kubwa ya kuendelea kuwepo kwa hali ya amani na utulivu yenye kuimarisha maendeleo yetu. 

Ndugu Wananchi,
Nafarijika sana kuona wananchi wa Zanzibar wameungana na Serikali yao katika kipindi cha miaka 53 kwa kuyatekeleza malengo ya Mapinduzi yetu na kupatikana mafanikio makubwa ya maendeleo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii. Katika  kipindi chote hicho, Serikali ilipanga mipango yake na iliitekeleza kwa mafanikio makubwa, bila ya kuingiliwa na nchi ye yote.

Yapo mambo mbali mbali yanayotekelezwa, ambayo yanaelezea mafanikio yaliyopatikana ikiwemo miradi 51 iliyozinduliwa na kuwekewa mawe ya msingi katika shamra shamra za maadhimisho haya. Ni haki ya kila mmoja wetu kujivunia mafanikio hayo na kuyaendeleza kwa manufaa yetu na wale watakaokuja baadae.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Awamu ya Saba, imeingia madarakani katika kipindi cha pili, baada ya Chama cha Mapinduzi kupata ushindi mkubwa wa asilimia 91.4, wa kura za Rais, ushindi wa majimbo yote 54 ya Baraza la Wawakilishi na ushindi wa viti vyote vya Madiwani; kwenye Uchaguzi wa marudio wa tarehe 20 Machi, 2016.  Uchaguzi huo ulirudiwa baada ya ule wa tarehe 25 Oktoba, 2015, kufutwa pamoja na matokeo yake na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya 1984 na Sheria ya Uchaguzi Namba 11 ya 1984.

Ndugu Wananchi,
Katika mwaka wa kwanza wa kipindi hiki cha pili, 2015/2016, cha Awamu ya Saba, Serikali imeanza vizuri utekelezaji wa Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, MKUZA III na Dira ya Maendeleo 2020 na kupata mafanikio ya kuridhisha katika kuuimarisha uchumi wetu, huduma za jamii na nyenginezo.

Katika kipindi hiki, pato halisi la Taifa lilikua kwa kiwango cha wastani wa asilimia 6.6.  Kadhalika, pato la mtu binafsi limefikia wastani wa TZS 1,632,000 sawa na USD 817 kwa mwaka 2015.   Katika mwaka 2016, kasi ya mfumko wa bei za bidhaa na huduma ilifikia asilimia 6.7 ambapo kasi hiyo ilikuwa asilimia 5.7 katika mwaka 2015.  Mfumko wa bei bado umedhibitiwa katika kiwango cha tarakimu moja.Ndugu Wananchi,
Mafanikio tunayoyaona, ya kuimarika kwa huduma mbali mbali, yametokana na juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya ukusanyaji wa mapato.  Kwa kipindi cha Januari hadi Novemba 2016, mapato yaliyokusanywa kutokana na vyanzo vya ndani, yameongezeka kutoka TZS  bilioni 336.6 mwaka 2015 hadi  TZS bilioni 441.3 mwaka 2016.  Hili ni ongezeko la TZS bilioni 104.7, sawa na asilimia 31.1.  Kadhalika, katika kipindi hiki, Serikali imepokea jumla ya TZS bilioni 54.53 kutoka kwa Washirika wetu wa Maendeleo, kuanzia mwezi wa Januari hadi Oktoba, 2016.

Natoa pongezi kwa Bodi ya Mapato ya Zanzibar (ZRB) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kazi nzuri waliyoifanya na nawahimiza waendelee na juhudi hizi, ili mapato yanayokusanywa kwa kila mwaka yazidi kuongezeka kwa kiwango kikubwa zaidi.

Ndugu Wananchi,
Kwa upande wa matumizi, Serikali imetumia jumla ya TZS bilioni 436.6 kwa kipindi cha Januari hadi Oktoba 2016. Kwa jumla, katika kipindi hicho, Mapato ya Serikali yalipindukia matumizi kwa jumla ya TZS bilioni 4.7, sawa na ongezeko la asilimia 1.08. Haya ni mafanikio makubwa katika usimamizi wa fedha za umma. Jitihada za kudhibiti matumizi zilizochukuliwa na Serikali, zimefanikiwa. Serikali itaendelea kuyadhibiti matumizi ambayo si ya lazima na kwa hivyo, fedha za Serikali zitaendelea kutumiwa katika kuwahudumia wananchi kwa mambo muhimu ya maendeleo yao.

Katika kipindi hiki, Serikali iliidhinisha jumla ya miradi 51 ya uwekezaji, yenye thamani ya USD milioni 497.92. Katika miradi hiyo, asilimia 53 ni miradi inayomilikiwa na wawekezaji wazalendo. Miradi hii inatarajiwa kutoa ajira zipatazo 2,658 na hivyo inakwenda sambamba na azma ya Serikali yetu ya kupunguza tatizo la ajira, na hatimae  kupunguza umaskini.

Ndugu  Wananchi,
Katika   kipindi hiki, Serikali  imeendelea  kuimarisha  sekta ya biashara ambayo ni muhimu kwa maisha na uchumi wetu.  Juhudi hizo zimeiwezesha Serikali kuongeza thamani ya bidhaa zilizosafirishwa nje ya nchi.  Jumla ya bidhaa zenye thamani ya  TZS   bilioni 94.94  zilisafirishwa nje ya nchi katika mwaka 2016, ikilinganishwa na  bidhaa zenye thamani ya TZS bilioni  45. 71, zilizosafirishwa mwaka 2015 . Ongezeko hilo ni sawa na  asilimia 99. Vile vile, jumla ya bidhaa zenye thamani TZS bilioni 167.09 ziliingizwa nchini katika mwaka 2016, ikilinganishwa na bidhaa zenye thamani ya TZS bilioni 156.94, zilizoingizwa nchini mwaka 2015.  Ongezeko hili ni sawa  na asilimia 7.  Serikali inaendeleza juhudi katika kuongeza usafirishaji wa bidhaa na kuimarisha kilimo ili kupunguza nakisi ya biashara  iliyopo.

Biashara kati ya Zanzibar na Tanzania Bara inaendelea vizuri  na ambapo bidhaa zenye thamani ya TZS bilioni 63.13 zilisafirishwa kwenda Tanzania Bara na bidhaa zenye thamani ya TZS bilioni 118.66 zilisafirishwa kutoka Tanzania Bara kuja Zanzibar, katika mwaka 2016. 

Katika kuhakikisha kwamba bidhaa zinazoingizwa zinakidhi viwango vinavyotakiwa,  Serikali kupitia  Shirika la Viwango la Zanzibar (ZBS), imeanzisha mfumo wa ukaguzi wa bidhaa kwa lengo  la kumlinda mtumiaji na kuongeza mapato.  

Ndugu Wananchi,
Serikali imeendelea kusimamia biashara ya karafuu kupitia Shirika la ZSTC.  Wakulima wa karafuu wameendelea kulipwa TZS 14,000 kwa kilo moja, ikiwa ni sawa na asilimia 80 ya bei ya soko  ya kuuzia nje. Katika mwaka 2015/16, ZSTC ilinunua tani 5,764.8 za karafuu, kwa TZS bilioni 80.9  Katika mwaka 2015/16, ZSTC iliuza nje ya nchi, jumla ya tani 5667 za karafuu, zenye thamani ya USD milioni 45.63, sawa na TZS bilioni 98.2.  Kadhalika, Shirika limeuza nje ya nchi mafuta ya viungo yenye thamani ya TZS milioni 872.37 katika mwaka 2016.

Katika kipindi hiki, Serikali imeendelea na utaratibu wake wa kuwapa wakulima wa karafuu miche ya mikarafuu bure, kwa lengo la kuliendeleza zao hilo.  Jumla ya miche 450,540 ya mikarafuu ilitolewa Unguja na Pemba.  Kadhalika, maandalizi ya Mkakati wa Tasnia Malibunifu (Branding),  kwa karafuu za Zanzibar na viungo vyengine yalikamilishwa na majaribio yake yamezinduliwa tarehe 6 Januari, 2017. 

Ndugu Wananchi,
Miongoni mwa  malengo ya Serikali, katika kipindi hiki cha pili cha Awamu ya Saba, ni kuimarisha viwanda, ili kupunguza uagiziaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi, kuongeza usafirishaji wa bidhaa hizo kwenda nje,  kuimarisha utumiaji wa malighafi zinazopatikana nchini na kuongeza ajira kwa wananchi.

Sekta ya Viwanda ilichangia asilimia 19.8 ya Pato la Taifa katika mwaka 2015 ikilinganishwa na asilimia 16.8 mwaka 2014.  Hii ni sawa na ongezeko la asilimia 3.0.  Katika mwaka 2016, viwanda vitatu vikubwa vya watu binafsi, kiwanda cha maziwa cha Azam, kiwanda cha “Zanzibar Milling Corporation”, kilichopo Mtoni na kiwanda cha Sukari kilichopo Mahonda vimeendelea kufanya kazi ya uzalishaji.  Aidha, Kiwanda cha Serikali cha Makonyo ya Karafuu na Viungo vyengine  kimeendelea na uzalishaji.   Vile vile, Kiwanda cha Matrekta, Mbweni kimefanya kazi ya kuyatengeneza matrekta yote ya Serikali, kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi katika kilimo cha mpunga. 

Ndugu Wananchi,
Katika kipindi hiki, Serikali kwa kushirikiana na wawekezaji na wafanyabiashara, imeanza kuchukua hatua ya ujenzi wa Ukanda wa Darajani na Michenzani,  “Mapinduzi Square”, ambapo yatajengwa maduka ya biashara, maeneo ya kuegesha  gari, kumbi za mikutano, ofisi na kadhalika.  Michoro kwa upande wa Darajani imetayarishwa na Serikali inawasiliana na UNESCO kwa ajili ya kuzingatia utaratibu wa uhifadhi wa Mji Mkongwe.  Ujenzi wa Darajani na Michenzani wote utasimamiwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii ya “ZSSF”.

Ndugu Wananchi,
Katika kipindi hiki cha 2015/16, Serikali kwa kushirikiana na Kampuni ya SS Bakhresa imeanza ujenzi wa miundombinu ya mji mpya  wa kisasa (Fumba Bay Satelite City), uliopo Fumba katika eneo la EPZ.  Kadhalika, nyumba za kisasa 150 kati ya 500, zimejengwa kwenye Mradi wa “Uptown living” unaoendeshwa na Kampuni ya “Union Property Developers”.  Mji mpya wa kisasa wa  (Fumba Bay Satelite City) na  mradi wa nyumba mpya 150 “Uptown Living” zikiwa kwenye hatua mbali mbali za ujenzi zimewekewa mawe ya msingi tarehe 9 Januari, 2017.

Vile vile, mradi wa ujenzi wa nyumba za kisasa katika eneo la Nyamanzi  umeanza kutekelezwa katika kipindi hiki.  Hadi hivi, sasa nyumba 20 kati ya nyumba 1300 zimeanzwa kujengwa na zimefikia katika hatua mbali mbali.

Ndugu Wananchi,
Kupitia Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF), Serikali ilianza kutekeleza mradi wa ujenzi wa  nyumba katika eneo la Mbweni. Mradi huo ni  wa ujenzi wa majengo 18 yenye urefu wa ghorofa 7, yatakuwa na nyumba 252 (Flats). Hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Novemba 2016, tayari majengo matano yamejengwa yenye jumla ya nyumba 70  za kuishi. Majengo haya yanatarajiwa kumalizika mwezi wa Aprili, 2016.

Ndugu Wananchi,
Kadhalika, ujenzi wa hoteli kubwa ya kisasa ya “Verde” (Mtoni Marine) ya nyota tano na vyumba 106, umeanza katika kipindi hiki na umefanyika kwa kasi sana.  Hoteli hii inajengwa na Kampuni ya SS Bakhressa iliwekewa jiwe la msingi tarehe 3 Januari, 2017,  na ujenzi unatarajiwa kukamilika hivi karibuni. 

Ndugu Wananchi,
Kuhusu utalii, katika mwaka 2016, jumla ya watalii 332,379 waliitembelea Zanzibar katika kipindi cha Januari hadi Novemba, 2016.  Idadi hii ni ongezeko la asilimia 13 ikilinganishwa na watalii 294,243 waliofika nchini mwaka 2015.    Utalii ulichangia Pato la Taifa kwa asilimia 27.

Katika kipindi hiki, Serikali ilitekeleza uamuzi wake wa kukiunganisha Chuo cha Utalii cha  Maruhubi na Chuo Kikuu cha Taifa (SUZA).  Madhumuni ya uamuzi huu ulikuwa ni kukiandaa Chuo hicho ili kutoa elimu ya juu kwa madhumuni ya kuimarisha taaluma ya utalii na huduma zake kwa jumla.

Katika kipindi hiki,  Serikali imeendelea kutoa ruzuku ya asilimia 75 ya gharama za  pembejeo za kilimo  zikiwemo mbegu, mbolea, dawa za magugu na huduma za matrekta kwa wakulima wa Unguja na Pemba.  Kuhusu kilimo cha mpunga wa umwagiliaji maji, katika kipindi hiki, Serikali imeendelea na ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji maji kutoka hekta 800 za sasa hadi kufikia hekta 1,560,  Pamoja na hatua hizo, Serikali ilianza ukarabati wa ghala mbili za kuhifadhia chakula  ambapo jumla ya TZS milioni 200 zimeanza kutumika kwa ajili ya kukamilisha matengezo makubwa ya ghala hizo ziliopo Malindi.   Pamoja na matengenezo hayo ya ghala, vitendea kazi vya ghalani vitanunuliwa ili lengo la kuhifadhia chakula liweze kufikiwa.

Kadhalika, Serikali imeziimarisha shughuli za utafiti wa kilimo katika Taasisi ya Utafiti wa Kilimo ya Kizimbani. Katika kipindi hiki, Taasisi hii iligundua mbegu mpya mbili za muhogo zenye uzazi mkubwa na zenye kustahamili maradhi pamoja na kuendeleza utafiti kwenye mbegu tatu za mpunga mpya.

Kuhusu Chuo cha Kilimo Kizimbani,  wahitimu 130 walimaliza masomo ya Cheti cha Kilimo na wahitimu 100 katika Stashahada ya kilimo, katika mwaka 2016.   Wahitimu hawa, watapoajiriwa  wataongeza nguvu katika kazi za ugani wa kilimo na ufugaji. 

Ndugu Wananchi,
Ufugaji bora na wa kisasa ni miongoni mwa malengo ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba. Katika kipindi hiki cha 2016, Serikali iliongeza jitihada katika kuongeza kipato cha wafugaji. Mradi mkubwa wa mifugo ulizinduliwa kwa ufadhili wa IFAD na “HEIFER International”. Mradi huu unatarajiwa kuongeza idadi ya ng’ombe wa kisasa na uzalishaji wa maziwa.

Jumla ya wafugaji mbali mbali walitembelewa na kupatiwa mafunzo ya kitaalamu na ufugaji bora wa ng’ombe, mbuzi na kuku.  Serikali inaendelea kuziimarisha huduma za uchunguzi wa maradhi ya mifugo na utibabu kwa kuongeza wataalamu, vifaa na kuimarisha maabara ya Maruhubi.  Vile vile iliendeleza ujenzi wa vituo vya karantini na vituo vya uzalishaji na  ilianza kuandaa utaratibu wa kuanzisha Taasisi ya Utafiti wa Mifugo.

Ndugu Wananchi,
Serikali imefanya jitihada kubwa katika kuendeleza sekta ya uvuvi.  Maandalizi ya kuanzisha mradi wa kituo cha kuzalisha vifaranga vya samaki huko Beit el Ras, yamekamilika.  Mradi huo utasaidia kuongeza uzalishaji wa vifaranga vya samaki kwa lengo la kuongeza idadi ya wafugaji na kurahisisha upatikanaji wa samaki nchini.

Katika kipindi hiki, kiwango cha samaki waliovuliwa mwaka 2016,  kilifikia tani 33,000, wenye thamani ya TZS bilioni 136.2 ikilinganishwa na tani 31,435 wenye thamani ya TZS bilioni 123.8  mwaka 2015, ikiwa ni ongezeko la asimilia 5.26. 

Matayarisho ya ujenzi wa soko jipya la kisasa la samaki katika eneo la Malindi,  yamekamilika katika kipindi hiki.  Miundombinu ya maji, umeme na huduma nyengine kutoka Serikalini  zimeshafikishwa katika eneo la ujenzi  na wakati wote wote ujenzi huo utaanza kwa ufadhili wa Serikali ya Japan.  Ujenzi wa soko la Malindi unakwenda sambamba na uamuzi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wa kuanzisha kampuni yake wenyewe ya uvuvi.  Kampuni hiyo, inatarajiwa kuanza baadae mwaka huu. 

Kwa mwaka 2016, uzalishaji wa mwani ulifikia tani 11,210  zenye thamani ya TZS bilioni 4.7.   Kwa upande wa mwani, Zanzibar ni nchi ya tatu ya uzalishaji wa zao hilo duniani. Serikali itaendeleza juhudi za kuwatafutia wananchi soko la uhakika la mwani na kuwahamasisha kuongeza uzalishaji wa zao hilo.

Ndugu Wananchi,
Serikali inachukua jitihada mbali mbali katika kuimarisha matumizi bora ya ardhi ndogo tuliyo nayo,  kukabiliana na athari za mazingira na kuongeza kasi ya kutatua migogoro ya ardhi.  Kuhusu migogoro ya ardhi, jumla ya migogoro 215 imetatuliwa kati ya mwezi wa Januari hadi Oktoba 2016 kwenye Mahkama ya Ardhi ikilinganishwa na migogoro 178 iliyotatuliwa katika kipindi kama hicho katika mwaka 2015. Natoa wito kwa wananchi wazingatie Sheria ya Ardhi na Mipango Miji na Vijiji ili kuepuka kuanzisha migogoro mengine maana hiyo iliyopita inatosha.

Ndugu Wananchi,
Kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita, Serikali imefanya ufuatiliaji wa maeneo 35 yaliyoharibiwa kutokana na uharibifu wa mazingira, 23 Unguja,  na 12 Pemba.  Katika kutekeleza Sheria Namba 3 ya Usimamizi wa Mazingira ya Zanzibar ya mwaka 2015, jumla ya miradi 33 imefanyiwa tathmini za kimazingira na kupewa vyeti baina ya mwezi wa Januari hadi Oktoba, 2016. 

Serikali itaendelea  kuelimisha  wananchi kuhusu athari za uharibifu wa mazingira na suala la mabadiliko ya tabianchi na itaendelea kushirikiana na Washirika wa Maendeleo katika kukabiliana na  athari za mazingira pamoja na mabadiliko ya tabianchi.
 
Ndugu Wananchi,
Uimarishaji wa miundombinu ya barabara ni muhimu katika kuchochea kasi ya maendeleo ya kiuchumi na kuimarisha huduma za jamii.  Katika kuimarisha ujenzi wa barabara, kwa upande wa Unguja, kazi ya ujenzi wa barabara ya Mwanakwerekwe  hadi  Fuoni Polisi (km 4) imekamilika. Barabara kutoka Maktaba Kuu hadi Gofu,  Kwarara hadi Fuoni pamoja na barabara ya Kinazini  hadi Kariakoo  zimefanyiwa matengenezo ya dharura kwa kiwango cha lami. Aidha, ujenzi wa barabara ya Jendele kupitia Cheju hadi  Unguja Ukuu Kaebona, (km 11.7), matengenezo yake yanaendelea vizuri  ambapo   km 3, kati ya hizo zimeshakamilika kwa kiwango cha lami.

Kwa upande wa Pemba, Serikali inaendelea na ujenzi wa barabara ya Ole hadi Kengeja (km 35) katika hatua ya kuweka kifusi, na km 11, kati ya hizo zimekamilika.  Ujenzi huo bado unaendelea. Aidha, kazi ya ujenzi wa barabara kutoka Mgagadu hadi Kiwani (km 7) kwa kiwango cha lami utakamilika mwezi huu wa Januari.


Ndugu Wananchi,
Katika mwaka 2016, idadi ya abiria waliotumia bandari zetu za Unguja na Pemba walifikia 2,412,657 kutoka abiria 1,938,857 mwaka 2015, sawa na ongezeko la abiria 473,800, ikiwa ni sawa na asilimia 19.6.  Katika kuimarisha huduma za bandari za kupakia na kuteremsha makontena na mizigo mengine, Serikali imenunua vifaa vipya vya kutekeleza kazi hiyo.  Jumla ya TZS bilioni 11.00 zimetumika katika kununua vifaa na zana mbali mbali,  katika mwaka 2016.  Vifaa hivyo vimezinduliwa rasmi, katika shamra shamra za sherehe za Mapinduzi hapo tarehe 4 Januari, 2016.

Aidha, huduma za usafiri wa meli za Serikali baina ya visiwa vya Unguja na Pemba zimekuwa za uhakika zaidi,  baada ya Serikali kununua meli mpya ya MV Mapinduzi II, ambayo tayari imeshaanza kufanya kazi baina ya Unguja, Pemba na Dar es Salaam katika kipindi cha mwaka mmoja. Matayarisho ya ununuzi wa meli nyengine ndogo ya mizigo na abiria inayolingana na MV Maendeleo pamoja na meli ya mafuta inayolingana na meli ya MT Ukombozi yamekamilika.  Meli hizi mbili zinatarajiwa kununuliwa katika mwaka huu wa fedha.

Ndugu Wananchi,
Kadhalika, katika kuimarisha huduma za uwanja wa ndege, Serikali imenunua gari mpya nne za kisasa za zimamoto.  Kituo kipya cha zimamoto kimejengwa, kitakachoweza kuzihifadhi gari zote nne kwa wakati mmoja, pamoja na ofisi za maofisa wa zimamoto, ghala,  na  kadhalika. 

Katika mwaka 2016, Serikali iliendelea na mpango wake wa kuimarisha kiwanja cha ndege cha kimataifa cha Abeid Amani Karume.  Ujenzi wa jengo  la abiria jipya ulisita kutokana  na changamoto  zilizojitokeza.   Hata hivyo, changamoto hizo zitapatiwa ufumbuzi hivi karibuni na ujenzi utaendelea.  Kuhusu uwanja wa ndege wa Pemba, mipango ilitayarishwa ya kufanya upembuzi yakinifu kwa kukipanua kiwanja hicho, ili ndege kubwa za aina ya Boeing 737 - 800 ziweze kutua pamoja na ujenzi wa jengo la abiria jengine.  Fedha kwa ajili ya kazi hio tayari zimepatikana kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika. 

Ndugu Wananchi,
Kuanzia mwezi Februari hadi Oktoba 2016, jumla ya vijiji 34 vimepatiwa umeme, Unguja na Pemba, ambapo vijiji 17 kati ya hivyo ni vya Unguja na 17 vya Pemba. Matayarisho ya kupeleka umeme katika Kisiwa cha Fundo, Pemba, yameanza ambapo kazi hiyo inatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Juni, 2017. Aidha, Serikali imepanga kuufikisha umeme katika Kisiwa cha Kokota na Uvinje huko Pemba.

Katika kuhakikisha wananchi wenye kipato cha chini wanafaidika na huduma za umeme, katika mwaka wa fedha 2014/2015 na mwaka 2015/2016, wananchi wapatao 4,487 wameungiwa umeme kwa njia ya mkopo. Mikopo iliyotolewa ina  thamani ya  TZS bilioni 1.35. Kati ya wananchi walionufaika na mikopo hiyo,  1,290 ni wa Unguja na 3,197 ni kutoka Pemba.

Ndugu Wananchi,
Tarehe 15 Novemba, 2016 Zanzibar, ilifungua ukurasa mpya wa historia kufuatia kutiwa saini  kwa Sheria Namba 6 ya Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia ya mwaka 2016, inayoipa uwezo Zanzibar kushughulikia utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia. Kwa mara nyengine tena, natoa shukurani zangu za dhati kwa Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Awamu ya Nne, Mhe. Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, kwa jinsi tulivyoshirikiana, ili kuhakikisha kwamba kabla hajaondoka madarakani,  suala la Zanzibar kusimamia utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia, linapatiwa ufumbuzi.

Hivi sasa, Serikali inaendelea na mazungumzo na wawakilishi wa kampuni za mafuta zilizojitokeza ili hatua za utafutaji na baadae uchimbaji wa mafuta na gesi asilia uweze kuanza.

Ndugu Wananchi,
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, imeendelea kutoa elimu bila ya malipo wala ubaguzi.  Katika mwaka 2016, idadi ya skuli imeongezeka kutoka 792 mwaka 2015 hadi 843, sawa na ongezeko la asilimia 7.  Idadi ya wanafunzi walioandikishwa, nayo imeongezeka kutoka wanafunzi 388,616 mwaka 2015 hadi kufikia 424,074 mwaka 2016, sawa na ongezeko la asilimia 8.36.  Kwa lengo la kuondoa msongamano wa wanafunzi katika skuli za sekondari, Serikali imeshakamilisha michoro ya ujenzi wa skuli 9 za ghorofa zitakazojengwa katika Wilaya ya Mjini, Magharibi A na B kwa Unguja na Wilaya zote nne za Pemba.  Fedha za ujenzi huo tayari zimepatikana kutoka Benki ya Dunia.

Aidha, vituo viwili vipya vya mafunzo ya amali vimeanza kujengwa huko Makunduchi, Unguja na Daya Mtambwe, Pemba kwa mkopo wa Benki ya Maendeleo ya Afrika.  Vile vile,  jengo jipya la Taasisi ya Karume ya Sayansi na Teknolojia litakalokuwa na madarasa, maabara na karakana limeanza kujengwa na jiwe la msingi liliwekwa rasmi tarehe 8 Januari, 2017 na linatarajiwa kukamilika, mwezi wa Mei, 2017. 

Ndugu Wananchi,
Mafanikio yamepatikana katika kuimarisha elimu ya juu. Idadi ya wanafunzi wanaosoma elimu ya juu katika vyuo vikuu vya Zanzibar imeongezeka, kutoka wanafunzi 6,370 mwaka 2015 hadi kufikia 7,383 mwaka 2016, ongezeko hili ni sawa na asilimia 5.9.  Katika kupanua fursa za elimu ya juu, Serikali imekiunganisha Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) na Chuo cha Utalii Maruhubi,  Chuo cha Ukaguzi wa Fedha Chwaka pamoja na Chuo cha Sayansi za Afya Mbweni, ili vyuo hivyo vilivyounganishwa viweze fursa ya kutoa elimu ya juu na kuongeza idadi ya wanafunzi wa elimu ya juu.

Kuhusu mikopo ya elimu ya juu, Serikali imetoa mikopo  kwa  wanafunzi 2,655 na   jumla ya TZS bilioni 3.7 zimetolewa kwa ajili ya wanafunzi hao.  Kadhalika, Serikali imekusanya jumla ya TZS milioni  480 kutoka kwa wahitimu waliorudisha mikopo, kwenye Bodi ya mikopo ya Elimu ya Juu. Nawahimiza wahitimu wanaodaiwa, wayalipe madeni yao hayo, ili wanafunzi wengine nao waweze kufaidika.

Ndugu Wananchi,
Kwa kutambua umuhimu wa afya kwa wananchi, katika mwaka 2016 Serikali imeendelea kuchukua hatua madhubuti ili kuhakikisha huduma za afya zinawafikia wananchi wote mijini na vijijini bila ya ubaguzi.

Katika mwaka 2016, vituo vinne vipya  vya afya vimejengwa na  kuifanya Zanzibar kuwa na  jumla ya vituo vya afya 152 ikiwa ni ongezeko la asilimia 13.4 ikilinganishwa na vituo 134 katika mwaka 2014/2015. Matengenezo makubwa yamefanywa katika kuimarisha miundombinu ya hospitali za Koteji na kuzipatia vifaa vya kisasa vya kutolea huduma na vitafikia hadhi ya hospital za Wilaya hivi karibuni.

Ndugu Wananchi,
Katika kuimarisha huduma za rufaa kwenye Hospitali ya Mnazi Mmoja, ujenzi wa wodi ya wazazi ya vitanda 100 na wodi ya watoto yenye vitanda 100, pamoja na vyumba maalum vya kutolea huduma za maradhi ya figo, zilizinduliwa rasmi tarehe 21 Novemba, 2016.  Vifaa vipya vya kisasa vimewekwa katika wodi zote mbili.   Sheria ya kuiongoza Hospitali ya Mnazi Mmoja imetungwa na tayari inafanya kazi na Bodi ya Ushauri, nayo tayari imeteuliwa na imeanza kazi zake.

Baada ya kujengwa upya, Hospitali ya Abdalla Mzee, iliopo Mkoani Pemba na kutiwa vifaa vya kisasa vya matibabu na uchunguzi wa maradhi kwa ajili ya kutolea huduma, hospital hii iliyopandishwa daraja kuwa ya Mkoa, ilizinduliwa rasmi tarehe 26 Novemba, 2016.  Hospitali hii itakuwa na uwezo wa kulaza wagonjwa 160 kwa wakati mmoja, wenye matatizo mbali mbali. Hospitali ya Wete na Chake Chake nazo zimeimarishwa katika kipindi hiki, kwa kupatiwa vifaa na nyenzo mbali mbali za kutolea huduma. 

Ndugu Wananchi,
Jitihada zetu zimefanikiwa sana katika kupambana na maradhi kwa kushirikiana na taasisi mbali mbali duniani.  Mafanikio yaliyopatikana yanatia moyo dhidi ya mapambano ya UKIMWI, Malaria, Kipindupindu, Kifua Kikuu, na maradhi mengine ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza.  Kiwango cha malaria na kasi ya kuenea kwake, kimezidi kushuka na kufikia asilimia  0.4, mwaka 2015-2016, kutoka asilimia 0.6, mwaka 2013-2014.

Upatikanaji wa dawa katika hospitali zote na katika vituo vya afya vyote vya Serikali umeimarika sana baada ya kuongeza bajeti ya Serikali, kutoka TZS bilioni 4.3, mwaka 2015/2016 hadi kufikia TZS bilioni 4.9 mwaka 2016/2017 pamoja na TZS bilioni 1.5 kutoka kwa Washirika wa Maendeleo.  Fedha za kununulia dawa zilifikia TZS bilioni 6.4 sawa na ongezeko la asilimia 48.8.

Maradhi ya kipindupindu yaliikumba nchi yetu kuanzia Septemba, 2015 hadi Julai, 2016.  Jumla ya wagonjwa 4,330 waliambukizwa na kutibiwa maradhi hayo katika vituo 21, vilivyofunguliwa Unguja na Pemba.  Kati ya wagonjwa hao, wagonjwa 48 sawa na asilimia 1.5 walifariki dunia na maradhi hayo hivi sasa yamemalizika.  Serikali inawapa pole, wafiwa, ndugu na jamaa wa ndugu zetu hawa waliofariki. 
Ndugu Wananchi,
Hadi sasa, mahitaji ya jumla ya maji safi na salama kwa Mikoa yote ya Zanzibar kwa siku ni lita  milioni 177.4  na maji yanayopatikana ni lita  milioni 140.7, sawa na asilimia 79.3 ya mahitaji. Kwa kiwango hiki, upungufu uliopo kwa siku ni lita milioni 36.7 sawa na asilimia 20.7.  Hata hivyo, Serikali ilifanya jitihada katika kukabiliana na hali hiyo ya upungufu wa maji katika maeneo mbali mbali.

Katika Mkoa wa Mjini Magharibi, Serikali kupitia Mamlaka ya Maji ya Zanzibar (ZAWA), imeanza kutekeleza Mradi wa Kuimarisha Miundombinu ya Maji (ZUWSP) katika  shehia 27 za Mji Mkongwe na Ng’ambo ya zamani.  Kupitia mradi huu, visima vipya 9 vitachimbwa, visima 23 vya zamani  vitatengenezwa na mabomba yenye urefu wa kilomita 68 yatalazwa. Kadhalika, matangi makubwa matatu; yatajengwa Saateni na Mnara wa Mbao.  Mradi huu utatekelezwa kwa fedha za mkopo wa  USD milioni 21.25 kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika na mchango wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wa  USD milioni 2.428.


Vile vile, visima 150 vilivyochimbwa kwa msaada wa  Serikali ya Ras-Al-Khaimah vinaendelezwa ili viweze kutumika.  Hadi mwisho wa mwezi Disemba, 2016 visima 17 kati ya vilivyochimbwa,  maji yalianza kupatikana.

Ndugu Wananchi,
Kwa upande wa miradi itakayotekelezwa hapo baadae kwa ajili ya kuimarisha huduma za maji, jumla ya USD milioni 92, ikiwa ni mkopo kutoka Serikali ya India zimepatikana kwa ajili ya kuimarisha huduma za maji katika Wilaya ya Magharibi B na baadhi ya maeneo katika Mkoa wa Mjini Magharibi.  Vile vile, jumla ya USD milioni 100 zitatolewa na Serikali ya Japan, ikiwa ni msaada kwa ajili ya kuimarisha huduma za maji katika eneo la Migombani, Dole na Fumba.  Kadhalika, Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China, itasaidia uchimbaji wa visima na usambazaji maji huko Chaani, Donge, Kisongoni na Miwani.

Ndugu Wananchi,
Katika kuliimarisha Shirika la Utangazaji la Zanzibar (ZBC), Serikali, mnamo mwezi wa Novemba, 2016,  imenunua vifaa vipya vya kisasa na mitambo kwa ajili ya ZBC TV na Radio.  Vifaa hivyo vinatarajiwa kufika nchini hivi karibuni.  Vile vile, vifaa mbali mbali vimeagizwa pamoja na ving’amuzi vipya na vya kisasa kwa ajili ya mitambo ya digitali ya ZBC TV.  Kwa kupatikana vifaa hivyo, ZBC wataweza kuzima, mitambo ya “Analog” kuanzia Aprili mwaka huu.  Aidha, jengo la “Karume House” na jengo la ZBC Radio yameanza kufanyiwa matengenezo makubwa ili yalingane na vifaa vitakavyowekwa.

Kwa upande wa Shirika la Magazeti la Zanzibar,  Serikali imeanza kununua vifaa vipya na nyenzo mbali mbali na kulikarabati jengo litakalotumiwa na wafanyakazi wa Zanzibar Leo liliopo Kikwajuni.  Katika kipindi hiki, uongozi  wa gazeti wa Zanzibar Leo utaongeza usambazaji wa gazeti hilo kutoka nakala 692 hadi 3,000.


Ndugu Wananchi,
Hivi karibuni Serikali imetoa tamko la  Kisheria Nambari 54 la  mwaka 2016 kwa lengo la  kuimarisha  utendaji wa  iliyokuwa  Idara ya Upigaji Chapa  na Mpiga Chapa  Mkuu wa Serikali  na kuanzisha Wakala wa Serikali wa  Uchapaji Zanzibar.  Aidha, mitambo mipya ya kisasa  ya upigaji chapa ilinunuliwa na ilifungwa kwenye jengo jipya hapo Maruhubi.  Baada ya jitihada hizi, hivi sasa kazi zote za Wizara zote za Serikali  za upigaji chapa zinatekelezwa katika Wakala wa Serikali wa Upigaji Chapa Zanzibar na pia, utatengeneza gazeti la Zanzibar Leo ambalo litachapishwa hapo.

Ndugu Wananchi,
Shughuli za utamaduni na michezo zimeendelezwa vyema katika mwaka 2016.  Tamasha la Filamu la Kimataifa la Zanzibar (ZIFF), Sauti za Busara na Tamasha la Utamaduni wa Mzanzibari, yamefanyika.  Wasanii wa fani mbali mbali, wameendelea kuitumia studio mpya ya Rahaleo kwa ajili ya kurekodia kazi zao.  Kuhusu sekta ya michezo, maadhimisho ya siku ya mazoezi yanayofanyika kila mwaka tarehe 1 Januari yameendelezwa.  Vile vile, Serikali imeendelea kutoa vifaa vya michezo kwa timu mbali mbali na  imeanza kutekeleza Agizo la Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu ya mwaka 2015-2020, ambapo kiwanja cha michezo kwa Wilaya ya Kusini Unguja, kimeanza kujengwa Kitogani, kati ya viwanja vitano vilivyoagizwa kwenye Ilani.

Kwa lengo la kukabiliana na tatizo la ajira kwa vijana, Serikali imechukua hatua ya kuimarisha Mfuko wa Vijana unaoratibiwa na Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, ili kuwawezesha vijana wajiajiri wenyewe.  Hadi kufikia Novemba, 2016, mikopo ya TZS bilioni 1.075 imetolewa kwa vijana 2,326, Unguja na Pemba.  Vile vile, vijana 1,824 waliajiriwa kwenye sekta binafsi katika mwaka 2016 na ajira kutoka Serikalini zilikuwa 711.

Ndugu Wananchi,
Mafanikio yamepatikana katika kuuendeleza Mfuko wa Kuwawezesha Wananchi Kiuchumi, ambapo hadi kufikia Disemba, 2016 jumla ya TZS bilioni 1.76 wamekopeshwa wananchi wanaofanya shughuli mbali mbali Unguja na Pemba.  Kati ya fedha hizo zilizokopeshwa, TZS bilioni 1.06 tayari zimelipwa.  Katika jitihada za kuandaa ajira, Serikali imeanzisha kituo cha kulelea wajasiriamali Mbweni ambapo wajasiriamali 819 wamepatiwa mafunzo.  Kituo hicho kimepanuliwa ili kutoa fursa zaidi kwa wajasiriamali. Aidha, Serikali ina mpango wa kujenga kituo kama hicho katika eneo la Tibirinzi Chake Chake Pemba, ili wajasiriamali wa Pemba nao waweze kufaidika na huduma za mafunzo ya ujasiriamali.

Aidha, katika kukabiliana na vitendo vya udhalilishaji wa wanawake na watoto, Serikali imeendeleza kampeni kwa kupiga vita vitendo hivyo, ambapo vituo vya mkono kwa mkono vimesaidia sana.  Wananchi wengi wameunga mkono mapambano haya.  Hata hivyo, tatizo la udhalilishaji bado lipo.  Katika mwaka huu, Serikali itaandaa mikakati maalum katika kupambana na vitendo vya udhalilishaji wa wanawake na watoto.  Natoa wito kwamba sote tushirikiane katika kuvikomesha vitendo hivi viovu.


Ndugu Wananchi,
Serikali imeanza kuwalipa wazee TZS 20,000 ikiwa ni pencheni ya jamii kwa mwezi kwa wazee waliofikia umri wa miaka 70, kwa Unguja na Pemba kwa lengo la kuwatunza.  Hadi Disemba 2016, jumla ya wazee 25,259 waliosajiliwa wamelipwa ambapo TZS bilioni 4.3 zimetumika. 

Katika mwaka 2016, Serikali imeendelea kuwatunza wazee wanaoishi katika nyumba za wazee Sebuleni, Welezo na Limbani kwa kuwapatia malazi, matibabu na fedha za matumizi ya kila mwezi. 

Kadhalika, jitihada za kuwahudumia watu wenye ulemavu zimefanywa ambapo jumla ya watu 125 walipewa vifaa vikiwemo magongo ya kutembelea, viti vya magurudumu na fimbo nyeupe.  Vile vile, jumla watu wenye ulemavu 16,611 wamesajiliwa ili kurahisisha namna ya kuwahudumia.  Aidha, hadi sasa jumla ya TZS milioni 167.4 zimekusanywa kwa ajili ya kuendeleza Mfuko wa watu wenye ulemavu ambazo zitatumika kwa ajili ya kuwaendeleza.


Ndugu Wananchi,
Serikali, katika mwaka 2016, imeshughulikia nidhamu za wafanyakazi kwa mujibu wa Sheria Nam. 2 ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2011 na Kanuni za Kazi.  Wapo watumishi walioondoshwa kwenye dhamana za uteuzi kwa kukiuka maadili ya kazi, vile vile, wapo waliosimamishwa kazi kutokana na ubadhirifu wa mali za umma na wanaendelea kuchunguzwa na kushughulikiwa na taasisi zinazohusika.  Katika kipindi hiki, Serikali imesimamia udhibiti wa matumizi ya fedha za umma kwa kupunguza safari za nchi za nje na za ndani ya nchi kwa watumishi wa umma.  Mikutano, semina na kongamano imefanyika bila ya wahusika kulipwa posho katika wakati wa saa za kazi. 

Kwa jumla, uwajibikaji wa wafanyakazi kazini umeongezeka ingawa bado wapo wafanyakazi wanaoendelea kufanya kazi kwa mazowea.  Serikali, itaendelea kuchukua hatua za ziada ya kusimamia nidhamu kazini. Zaidi ya hayo katika kipindi hichi mipango yote inakamilika ya kuwalipa wafanykaazi wa Serikali kima cha chini cha mshahara kutoka TZS 150,000 kwa sasa hadi TZS 300,000, kiwango hichi kimeongezeka sasa kwa asilimia mia moja, mshahara huu mpya utaanza kulipwa kuanzia mwezi April hivi karibuni.

Katika mwaka 2016, Serikali imeimarisha mfumo wa sheria, kupitia mradi wa mageuzi ya sekta ya sheria, kwa kufanya mabadiliko katika utendaji kazi wa Mahkama, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu na Vyuo vya Mafunzo.  Taasisi hizo zimejengewa uwezo zaidi.  Mahkama ya Chake Chake imezinduliwa rasmi, baada ya ukarabati mkubwa, ujenzi wa Mahkama ya watoto ya Mahonda umekamilika na matayarisho ya ujenzi wa Mahkama Kuu mpya huko Tunguu umeanza.

Katika mwaka 2016, Baraza la Wawakilishi limetekeleza majukumu yake kwa kufanya mikutano minne ya kawaida, ukiwemo mkutano mmoja wa kupitia bajeti ya Serikali ya mwaka 2016/2017.  Jumla ya maswali 910 yaliulizwa na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, kati ya hayo maswali 254 yalikuwa ni ya msingi na 656 ya nyongeza.  Maswali yote hayo yalijibiwa  na mawaziri wa Wizara mbali mbali.

Kadhalika, jumla ya miswada 12 ya sheria imejadiliwa na kutungiwa sheria.  Miongoni mwa hiyo ni, ule unaohusiana na Sheria Namba 6 ya mwaka 2016 ya Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia na marekebisho madogo ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, kuhusu uteuzi wa Rais wa nafasi 10 za wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.

Ndugu Wananchi,
Kwa lengo la kukabiliana na vitendo vya rushwa na uhujumu wa uchumi, katika kipindi cha mwaka 2016, Mamlaka ya Rushwa na Uhujumu wa Uchumi imeshughulikia tuhuma 46 ambazo zipo katika hatua nzuri za uchunguzi na 6 zipo Mahkamani.  Kadhalika, Mamlaka imeendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya madhara ya vitendo vya rushwa na uhujumu wa uchumi kwenye shehia 123 Unguja na Pemba.

Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma iliyoanzishwa kwa mujibu wa Sheria Nam. 4 ya mwaka 2015, ilianza kazi zake mwezi wa Aprili, 2016.  Viongozi wa Umma, walipewa fomu za Tamko la Mali na Madeni na kutakiwa wazijaze na wazirudishe fomu hizo kwenye Tume si zaidi ya tarehe 31 Disemba, 2016. Wale viongozi ambao walishindwa kuziwasilisha fomu zao, baada ya tarehe 31 Disemba, 2016; watakuwa wamevunja sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.  Tume ya Maadili ya Umma itawachukulia hatua. Kadhalika, Tume itazihakiki taarifa zote zilizowasilishwa na viongozi wa umma.

Katika mwaka 2016, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ziliandaa Kongamano la Tatu la Watanzania wanaoishi nchi za nje ambalo lilifanyika Zanzibar kwa mafanikio.  Kadhalika, Wazanzibari wanaoishi nje ya nchi  walichangia kujenga madarasa ya skuli, kutoa vitabu vya masomo mbali mbali pamoja na samani katika skuli na vyuo vyetu nchini.

Ndugu Wananchi,
Kudumishwa kwa Mapinduzi ya Zanzibar ambayo leo yametimiza miaka 53, lazima twende sambamba na kudumishwa na kuendelezwa kwa Muungano wa Tanzania ambao ifikapo tarehe 26 Aprili mwaka huu wa 2017 utatimiza miaka 53 tangu kuasisiwa kwake.

Kadhalika, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuyaendeleza masuala ya Muungano.  Vile vile, tutahakikisha kuwa tunashirikiana  katika mambo yasiyo ya Muungano kwa faida ya pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.   Mimi na  Mheshimiwa Dk. John Pombe Joseph Magufuli tunatambua uzito wa dhamana mliyotupa Watanzania katika kuhakikisha kwamba Muungano wa Tanzania unadumu na unaimarika kwa dhamira ile ile ya viongozi wetu wa Awamu zilizotangulia.
Ndugu Wananchi,
Siri kubwa ya mafanikio tunayoendelea kuyapata nchini ni kuendelea kuwepo kwa amani na utulivu.  Kwa hivyo, kuhimiza amani na kuiendeleza ni wajibu kwa viongozi wote pamoja na wananchi.  Tusichoke kuhimizana  juu ya umuhimu wa amani, ili tuweze kupiga hatua zaidi katika kukuza uchumi na ustawi wa wananchi.  Nakuhakikishieni wananchi nyote, kwamba Serikali zetu zote mbili; zitachukua  hatua ili nchi yetu inabaki kuwa nchi ya amani na utulivu. 

Ndugu  Wananchi,
Nakamilisha hotuba yangu kwa kutoa shukurani zangu za dhati kwa mara nyengine tena kwa viongozi na wageni wetu wote mliokuja kutuunga mkono katika maadhimisho ya Miaka 53 ya Mapinduzi.  Vile vile, natoa shukurani zangu kwa Kamati ya Halmashauri ya Sherehe na Maadhimisho inayoongozwa na Mheshimiwa Makamo wa Pili wa  Rais;  Balozi Seif Ali Iddi kwa uongozi wake mahiri ambao umezifanikisha sherehe zetu hizi.

Vile vile, natoa shukurani kwa nchi zote marafiki, washirika wetu wa maendeleo, taasisi na mashirika ya kimataifa wanaoshirikiana nasi katika kuifanikisha mipango yetu ya maendeleo.  Kadhalika, natoa shukurani kwa viongozi na wafanyakazi wote wa Serikali kwa jitihada zenu za kuwatumikia wananchi wote kwa misingi ya haki, uadilifu na utumishi bora.  Matumaini yangu ni kuwa tutaendelea kushirikiana na kuongeza kasi katika kuyatekeleza majukumu yetu, ili nchi yetu izidi kupiga hatua za maendeleo.

Kadhalika, shukurani zangu,  zende kwa makamanda na wapiganaji wa   vikosi vyetu vya ulinzi na usalama kwa kuendelea kudumisha ulinzi wa nchi yetu na mipaka yake.  Vile vile, nawapongeza kwa gwaride la ukakamavu lililozipamba sherehe zetu za leo.  Aidha, natoa shukurani kwa wasanii waliotuburudisha, vijana wetu, pamoja na wafanyakazi wa vyombo vya habari pamoja kwa kuzitangaza sherehe zetu kwa wananchi ambao kwa sababu mbali mbali hawakuweza kuhudhuria. Nakutakieni nyote safari njema ya kurudi nyumbani.

MAPINDUZI DAIMA

MUNGU IBARIKI ZANZIBAR

MUNGU IBARIKI TANZANIA

MUNGU IBARIKI AFRIKA

Ahsanteni kwa kunisikiliza.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.