Habari za Punde

Kima Punju hupatikana Zanzibar tu duniani kote

Na Ali M. Khamis


Watu wengi hawafahamu vivutio vilivyopo visiwa vya Zanzibar ambapo wanafikiria kuwa Zanzibar ina uzuri wa fukwe za bahari tu.

Kumbe si fukwe tu bali kuna vivutio vingi vya asili ambavyo vinapatikana kama vile msitu wa jozani ambao umekuwa kivutio kikubwa kwa watu wengi na wataliii kupendelea kwenda kuutembelea.

Ni   umbali  wa  kilomita  35 kutoka kusini  mashariki  mwa  Unguja  ambapo  utakuta  msitu wa hifadhi wenye kupakana na ghuba ya Chwaka. Hifadhi  hiyo  imejumuisha vijiji tisa  vikiwemo Pete, Kitogani ,Ukongoroni  chwaka ,Charawe ,Unguja ukuu,  Michamvi na Cheju.
     
Hifadhi  ya  msitu  huo kuna wanyama adimu ambao hawapatikani katika hifadhi nyingine yoyote njee ya visiwa vya Zanzibar. Wanyama hao ni kama vile  chura wa Jozani, Chuwi wa Zanzibar, Jongoo wa Jozani, Paa Nungwa na Kima punju (Red Colobus Monkey) ambao wamekuwa vivutio  vikubwa   vya  utali  na kuwafanya  watu kila kona ya Dunia kufunga safari na kwenda kuvingalia vivutio hivyo.

Katika Wanyama wote hao Kimapunju ndio kivutio kikuu cha watalii kutokana na rangi yake, umbile na tabia yao ya kuishi ujamaa kama Binadamu.

Uso wa Kima punju ni mweusi una taji la manyoya meupe, rangi ya pinki kwenye midomo na pua, pia ana mkia mrefu wenye rangi nyeusi kwa juu na nyeupe kwa chini na wanyama hao hupatikana kwenye hifadhi za misitu ya Jozani (Unguja) na Ngezi (Pemba).

Kima punju huishi kwa kufuatana kwa makundi na kila kundi huwa kuna dume mmoja ambapo dume huyo kamwe hakubali kuliacha kundi hilo kuingiliwa na dume mwengine hadi kufa kwake.

Pia Kima punju hupendelea sana kula majani  machanga ya miti kama vilele vya mipera na majani ya mikungu ambayo ndio hupendelea kula zaidi jambo ambalo husababisha mikungu yote ya Jozani kutokuwa na majani kabisa kwani  yakichipua tu huliwa na wanyama hao.

Wanyama hao hula maganda ya matunda  kama vile Embe, Mapera na makoroma ya nazi na hawali kabisa matunda yenye sukari  kama vile Embe mbivu ,Ndizi mbivu  kutokana na matumbo yao kushindwa kusaga vitu vya sukari (insuline  hormone). 

Vile vile  Kima punju hupendelea kula makaa  meusi kama tiba ya maradhi mbali mbali yanayowasumbua na ni kinga  ya maradhi yao.

Kima punju hukaa  zaidi ya miezi mitano bila kunywa maji kutokana na vyakula wanavyokula si kumtaka kunywa maji, kwani mara nyingi hula vyakula vyenye ukakasi vikiwemo vya  majani machanga.

Mradi wa kuhifadhi msitu wa Jozani wa Jozani-Chwaka Bay Conservation Project uliokuwepo kati ya mwaka 1995 mpaka mwaka 2003 ulimchagua mnyama huyu kuwa kwenye nembo ya utunzaji mazingira Zanzibar.

Kima punju wako kwenye hatari kubwa ya kupotea na tayari Shirika la Kuhufadhi Wanyamapori Duniani (IUCN) limewaweka kwenye mstari mwekundu. Hali hii imetokana na makazi hao kuharibiwa na binadamu kwa uvunaji wa miti kwa ajili ya mbao, uchomaji wa misitu na usafishaji wa misitu kwa ajili ya mashamba.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.