Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Azungumza na Bolozi wa Korea ya Kusini Ofisini Kwake Vuga Zanzibar.

 Balozi wa Korea Nchini Tanzania Bwana Song Geum Yong akisalimiana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Vuga Mjini Zanzibar  walipokutana kwa kubadilishana mawazo.
Balozi Song Kati kati akielezea faraja yake kwa Balozi Seif kutokana na Makampuni na Taasisi za nchi yake kuonyesha azma ya kutaka kusadia maendeleo ya Wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
Balozi Seif Kushoto akisisitiza malengo ya SMZ katika kuimarisha miundombinu ya sekta mbali mbali nchini ili kuwajengea maisha bora wananchi wake.
Balozi Seif  Kushoto akimpatia zawadi ya vyakula vya viungo Balozi wa Korea Kusini Bwana Song mara baada ya kumaliza mazungumzo yao Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.(Picha na – OPMR – ZNZ.)

Na Othman Khamis OMPR.
Balozi wa Korea Kusini Nchini Tanzania Bwana Song Geum Yong  amesema Zanzibar inazidi kubadilika Kimaendeleo kutokana na kasi kubwa ya  miundombinu inayoendelea kuwekwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikiungwa mkono na  Mataifa na Taasisi washirika wa Maendeleo.

Amesema Taasisi na Makampuni ya Korea  yanafurahia mabadiliko hayo  na kuamua kusaidia ujenzi wa Miradi ya Kielimu akiutolea mfano ule wa Skuli ya Sekondari ya Kwarara  uliomalizika hivi karibuni  ili kuipa nguvu zaidi Sekta ya Elimu Zanzibar  ambayo  ndio kichwa cha maendeleo hayo.

Balozi Song Geum Yong  alieleza hayo wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Vuga Mjini Zanzibar  aliyekuwepo Visiwani Zanzibar katika uzinduzi wa Skuli hiyo pamoja na kuhudhuria maadhimisho ya sherehe za kutimia miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Alisema anapata  faraja kuona kuwa ujenzi wa Skuli hiyo uliopata msaada kutoka Shirika la Maendeleo ya Korea { KOICA }, Good Neighbors, Shirika la Utangazaji la Korea { SBS } na Taasisi ya Wasanifu Majengo ya Korea umekwenda sambamba na ujenzi wa Kituo cha Habari cha Kimataifa cha Tumaini.

Balozi Song alieleza kwamba Kituo hicho  cha kurekodia Matangazo ya Redio na Televisheni cha Tumaini kilichoanzishwa kwenye Skuli hiyo ya Sekondari Kwarara kwa kiasi kikubwa  kitasaidia kutoa Taaluma kwa Wanafunzi pamoja na Wananchi wa sehemu mbali mbali hapa Zanzibar.

Akitoa shukrani zake kwa misaada mbali mbali inayotolewa na  Korea kwa Tanzania na Zanzibar kwa jumla Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  alisema Serikali inakusudia kujenga Bara bara ya lami inayoingia kutoka bara bara Kuu hadi kwenye Skuli hiyo ili kuwaondoshea usumbufu wa Mawasiliano Wananchi na Wanafunzi wa eneo hilo.

Balozi Seif alisema Korea ya Kusini inastahiki kupongezwa  kwa jitihada zake za kuunga mkono maendeleo ya Zanzibar, lakini  hata hivyo alimshauri Balozi Song  kutumia maarifa yake katika kuzishawishi Taasisi na Makampuni ya nchi yake kuendelea kuelekeza nguvu zao katika uwekezaji  wa sekta tofauti ikiwemo ile ya usafiri wa Baharini.

Alisema  sekta ya Kilimo Zanzibar hasa katika upande wa umwagiliaji  pia inastahiki kuungwa mkono zaidi  ili kuwaongezea nguvu za uzalishaji Wakulima kwa vile zaidi ya asilima 80 ya Wananchi wa Visiwa vya Zanzibar wanaendesha maisha yao kwa kutegemea sekta hiyo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.