Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na wananchi wa Kisiwa cha Tumbatu wakati alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Skuli ya Sekondari Tumbatu ikiwa muendelezo wa ziara yake ya kukagua miradi mbali mbali ya maendeleo.
Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema amefurahishwa na ushirikiano unaotolewa na wananchi wa Kisiwa cha Tumbatu kwa wakandarasi wanaojenga miradi mbali mbali ya maendeleo kisiwani humo.
Ameyasema hayo katika ziara yake ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa skuli ya Sekondari ya ghorofa ( G+3 ) inayojengwa katika kijiji cha Tumbatu Gomani Mhe. Hemed amesema dhamira ya Serikali ya Awamu ya Nane ( 8) inayoongozwa Rais Dkt. Mwinyi ni kuona wananchi wa Tumbatu wanapata huduma zote za stahiki za kimaendeleo kwa kiwango kinachokubalika sawa na sehemu nyengine.
Makamu wa Pili wa Rais amesema wananchi wa Tumbatu wana kila sababu ya kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Dkt Mwinyi ikiwemo za kuwaletea maendeleo endelevu katika nyanja mbali mbali ikiwemo Elimu, Afya, Barabara, umeme na maji safi na salama ili ustawi wa wananchi wa Tumbatu uweze kuimarika zaidi.
Mhe. Hemed amewaahidi wananchi wa Kisiwa cha Tumbatu kuwa Serikali itahakikisha inazipatia ufumbuzi changamoto zilizomo kisiwani humo ikiwa ni pamoja na kuajiri madaktari wazawa na watumishi wa kada nyengine wanaotoka maeneo hayo ili kuepusha usumbufu wa kutokupatikana huduma kwa wakati.
Sambamba na hayo Mhe.Hemed amewataka wananchi wa Tumbatu na wazanzibar kwa ujumla kuendelea kudumisha Amani na ushirikiano uliopo nchini ili kuweza kupata maendeleo endelevu yatakayokuwa na faida kwa vizazi vya sasa na baadae.
Nae Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe.Lela Mohamed Mussa amesema dhamira ya Rais Dkt Mwinyi ya kuleta mageuzi katika sekta ya elimu mijini na vijijini inaonekana wazi wazi kwa kujengwa skuli za kisasa zenye kukidhi mahitaji yote ya kufundishia na kujisomea.
Mhe. Lela amewashukuru wananchi wa Tumbatu kwa ushirikiano wao mkubwa na wakupigiwa mfano wanaowapatia Wizara ya elimu na wakandarasi wanaojenga miradi mbali mbali kisiwani hapo jambo linalowapa nguvu wakandarasi ya kumaliza ujenzi huo kwa wakati na kwa kiwango kilichokusudiwa.
Kwa upande wake Mkandarasi kutoka kampuni ya Simba Developers Ltd Lukas S amesema licha ya kukabiliwa na changamoto ya usafirishaji wa material kwa ajili ya ujenzi kampuni itahakikisha inakabidhi jengo hilo mwishoni wa mwezi wa nane ili kuwawezesha wanafunzi kuendelea na masomo yao katika mazingira bora.
Lukas amesema kampuni ya Simba Developers inaahidi kulijenga jengo hilo kwa viwango na ubora wa hali ya juu ambalo litawahudumia zaidi ya wanafunzi 1890 kwa mkondo mmoja wa masomo.
Imetolewa na kitengo cha Habari (OMPR)
Leo Tarehe…20 . 07. 2024
No comments:
Post a Comment