Habari za Punde

Waziri Kombo akutana na Mkuu wa Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya Umoja wa Afrika

 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo 

amekutana na Mkuu wa Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya Umoja wa Afrika (AU), na Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Botswana, Mhe. Mokqweets Masisi katika Ofisi ndogo za Wizara, jijini Dar es Salaam.

Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya AU iko nchini  kuangalia zoezi la Uchaguzi Mkuu wa Tanzania unaotarajiwa kufanyika tarehe 29 Octoba, 2025, ili kuhakiki Utekelezaji wa Demokrasia ya kweli kupitia Uchaguzi huo, kwa kuzingatia misingi ya haki, uwazi na uhuru. 

Akizungumza katika katika Mkutano huo, Mhe. Kombo amesema Serikali ya Tanzania imefanya jitihada mbalimbali ili  kuhakikisha uchaguzi mkuu unafanyika kwa amani na uwazi na unakuwa huru na wa haki.

Mhe. Kombo aliikaribisha kwa dhati Misheni hiyo ya AU nchini na kuipongeza kwa utekelezaji na kufuatilia  zoezi la Uchaguzi Mkuu nchini.

"Utekelezaji wa misheni kama hii ni changamoto kubwa inayohitaji rasilimali nyingi na jitihada za dhati, na uwepo wa Mheshimiwa Masisi ni ishara ya mshikamano wa kikanda na kujitolea katika demokrasia" Alifafanua Mhe. Balozi Kombo.

Waziri Kombo alielezea mafanikio ya awamu ya kwanza ya tathmini ya awali ya uchaguzi, iliyofanyika Juni 2025, iliyoongozwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Afrika Kusini Dkt. Pumzille Mlambo–Ngcuka ambapo maoni yaliyotolewa katika tathmini hiyo, yaliimarisha jitihada za Tanzania katika maandalizi ya Uchaguzi Mkuu.

Aidha, Waziri Kombo alieleza azma ya Serikali ya kuimarisha demokrasia katika Uchaguzi Mkuu ujao na kuahidi ushirikiano kamili wa Serikali na wadau wote wa uchaguzi katika mipango yote ya uchaguzi.

Waziri Kombo pia alisema  takwimu zinaonyesha ongezeko la asilimia 26.5 katika idadi ya wapiga kura, na kuelezea mipango ya kampeni za uchaguzi, elimu kwa wapiga kura, na jitihada za kuelimisha wananchi kupitia mashirika ya kiraia.

" jitihada hizi zote zinalenga kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa usahihi, haki, na kuakisi mapenzi ya wananchi wote wa Tanzania" Alibainisha Mhe. Kombo.

Waziri Kombo pia aliishukuru Misheni hiyo ya AU kwa juhudi zake za kukuza demokrasia na utawala bora, na kuwatakia mafanikio katika utekelezaji wa majukumu yake wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.

Naye Mkuu wa Misheni hiyo ya AU Mhe. Masisi aliishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuiamini Misheni hiyo na aliweka bayana kuwa timu yake itazingatia maadili ya Uchaguzi Mkuu pamoja na Sheria na miongozi ya nchi na ya AU katika kutekeleza majukumu yao.





No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.