Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), akizungumza wakati akifungua Kikao cha Watumishi wa Wizara ya Fedha kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (hayupo pichani), kilichofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP), jijini Dodoma, ambapo amewaagiza watumishi kuimarisha mfumo wa ukusanyaji wa mapato na kuratibu upatikanaji wa fedha ili kutoa fedha kwa wakati kwa miradi yote iliyoidhinishwa na Bunge.
Watumishi wa Wizara ya Fedha, wakifuatilia hotuba ya Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb) (hayupo pichani), wakati akifungua Kikao cha Watumishi wa Wizara ya Fedha kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (hayupo pichani), kilichofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP), jijini Dodoma.
Na. Saidina Msangi na Farida Ramadhani, WF, Dodoma
Watumishi wa Wizara ya Fedha wameagizwa kuimarisha mfumo wa ukusanyaji wa mapato na kuratibu upatikanaji wa fedha ili kutoa fedha kwa wakati kwa ajili ya kutekeleza miradi yote iliyoidhinishwa na Bunge.
Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Fedha kwa niaba ya Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), wakati akifungua kikao cha watumishi na Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya wizara hiyo kilichofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP), jijini Dodoma.
Alisema kuwa ni muhimu watumishi hao kutekeleza majukumu yao na maelekezo yanayotolewa na Serikali kwa wakati ikiwa ni pamoja na kufanyia kazi kwa wakati yatokanayo na mjadala wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2024/25.
‘‘Ni muhimu kuwa mfano katika kuzingatia miongozo ya usimamizi wa mali na fedha za Umma, hususan katika kufungamanisha mahitaji yetu na bajeti iliyoidhinishwa na Bunge pamoja na kuimarisha mfumo wa ushirikishaji, uratibu na kufanya kazi kwa karibu na wadau wetu ili kuongeza ubora wa huduma zetu kwa wateja wa ndani na nje ”, alisisitiza Mhe. Chande.
Aliwaelekeza watumishi hao kutumia taaluma zao katika kushauri na kufanya maamuzi kwa wakati kwa maslahi mapana ya Taifa pamoja na kufanya kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo iliyopo ili kuimarisha mfumo wa utawala bora na utawala wa sheria.
Aidha, aliwaagiza Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya wizara hiyo, kuendelea kusimamia majukumu waliyopewa katika Taasisi wanazoongoza na kuongeza ubunifu na weledi ili kuweza kuchangia fedha katika mfuko Mkuu wa Serikali.
Alisema ni muhimu kusimamia majukumu yao kwa kuzingatia sheria na kanuni, mali na fedha za Serikali ikiwemo kudhibiti matumizi mabaya ya fedha za Umma katika Ununuzi.
‘‘Nendeni mkatekeleze kwa ufanisi Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2023 na Kanuni zake pamoja na kutumia Mfumo wa NeST, tutimize viapo na wajibu wetu katika suala la usimamizi wa mali na fedha za Umma,’’aliagiza Mhe. Chande.
Mhe. Chande alitoa wito kwa watumishi hao kushiriki kikamilifu katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa pamoja na kushiriki katika zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura ili kuweze kutumia haki zao wakati wa uchaguzi mkuu kuchagua viongozi wanaowataka na kuendelea kudumisha amani na utulivu uliopo katika Taifa letu ili shughuli za kiuchumi na kijamii ziendelee kuimarika.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Dkt. Natu El-maamry Mwamba, Naibu Katibu wa wizara hiyo Bi. Jenifa Christian Omolo alisema kuwa lengo la kikao hicho ni kushirikishana masuala mbalimbali ya kiutendaji pamoja masuala mengine yanayogusa maisha ya watumishi nje ya utumishi wa Umma.
‘‘Lengo la kujumuisha masuala ya maisha ya watumishi nje ya utumishi wa Umma ni kukumbushana kuwa sisi watumishi ni sehemu ya Umma, na pia inawezekana leo ni watumishi wa Umma lakini kesho tukawa raia kama raia wengine nje ya utumishi wa Umma’’alieleza Bi Omolo.
Akizungumzia utekelezaji wa majukumu ya wizara Bi. Omolo alisema kuwa Wizara imeendelea kusimamia kwa ufanisi utekelezaji wa mpango na bajeti ya 2023/24, bila kusahau changamoto mbalimbali zilizosababishwa na mabadiliko ya tabianchi.
Alisema wizara imeendelea kutoa huduma kwa wateja kwa mujibu wa muundo na mgawanyo wa majukumu ya Serikali, kubuni na kusimamia utekelezaji wa Sera za Uchumi jumla, Fedha na Ununuzi wa Umma pamoja na kusimamia ukusanyaji wa mapato na utaratibu wa upatikanaji wa fedha kutoka kwa wadau mbalimbali wa maendeleo.
‘‘Tumeendelea kuratibu upatikanaji wa fedha na kuimarisha uhusiano wa masuala ya fedha kwa Taasisi za kikanda na Kimataifa, kutekeleza maelekezo ya viongozi na kushiriki katika shughuli mbalimbali za pamoja za kitaifa ikiwemo michezo ya Mei Mosi, SHIMIWI, maonesho ya SABASABA, Nanenane n.k;’’, alifafanua Bi. Omolo.
Kikao hicho cha wafanyakazi kilijumuisha Wakuu wa Hazina Ndogo, Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara, Wakuu wa Idara na Vitengo pamoja na watumishi wa wizara hiyo kwa ajili ya kushauriana na kubadilishana uzoefu juu ya masuala mbalimbali yanayohusu Wizara, Taasisi na Serikali kwa ujumla.
Naye Mtakwimu Mkuu wa Serikali Bi. Albina Chuwa ameipongeza wizara kwa kufanikisha kikao hicho kikijumuisha viongozi wa Taasisi za wizara na kutoa rai kuwa vikao hivyo vijumuishe watumishi wa Taasisi za wizara ili kuwa na uelewa wa pamoja katika utekelezaji wa majukumu.
No comments:
Post a Comment