Habari za Punde

Chuo cha Diplomasia chapokea ufadhili wa Kompyuta 150 kutoka kwa Serikali ya Jamhuri ya Korea.


Na.Rose Mbilinyi. 
Chuo cha Diplomasia ambacho kilianzishwa kwa ushirikiano wa Serikali ya Tanzania na Msumbiji, kimepokea ufadhili wa kompyuta za mezani 150 ambazo zilikabidhiwa na Serikali ya Jamhuri ya Korea kupitia ofisi zake za Ubalozi zilizopo hapa nchini. Hafla hiyo  ya makabidhiano ilifanyika jana Kurasini - Jijini Dar es Salaam

Katika makabidhiano hayo Balozi wa Korea nchini Mhe. Song Geum Young alieleza kuwa Serikali ya Jamhuri ya Korea inatambua mchango mkubwa wa sekta ya elimu katika maendeleo ya Taifa lolote hususan Kiuchumi, kijamii na hata kisiasa. Hivyo kufuatia umuhimu huo Serikali ya Korea pamoja na kufadhili miradi mingine katika sekta ya afya na ujenzi wa miundombinu pia imeahidi kuanzisha  ushirikiano baina ya Chuo cha Diplomasia cha Tanzania na Chuo cha Taifa cha Diplomasia cha nchini Korea.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ramadhan Muombwa Mwinyi ambaye aliiwakilisha Wizara katika hafla ya makabidhidhiano ya kampyuta hizo, aliishukuru Serikali ya Jamhuri ya Korea pamoja na kutambua mchango wake katika ufadhili wa kozi za muda mfupi na muda mrefu kwa watanzania na kwamba Tanzania itaendelea kuzitumia nafasi hizo kwa tija ya Taifa.

Pia Mwenyekiti wa Chuo cha Diplomasia kwa niaba ya Bodi na uongozi wa chuo hicho kwa ujumla ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Korea kwa kutambua umuhimu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika taaluma ya Uhusiano wa Kimataaifa. “Serikali yetu itahakikisha inazalisha wanadiplomasia wenye uwezo mkubwa katika TEHAMA ili kuweza kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia ulimwenguni” alisema Balozi Sefue

Korea ni nchi ya uchumi wa kati hata hivyo ni miongoni mwa mataifa ya Bara la Asia ambayo uchumi wake umekua kwa kasi  kutokana na msisitizo mkubwa uliowekwa na taifa hilo katika kusimamia sekta ya Elimu ili iweze kuchangia maendeleo katika sekta nyingine. Hivyo ni wakati sasa watanzania wakaiga mfano huu kwa kutekeleza sera ya Serikali ya awamu ya tano ya Tanzania ya Viwanda kupitia elimu.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.