Habari za Punde

Dk Shein Afungua Semina ya Viongozi wa SMZ Zanzibar.

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar                                                                                                                    1.2.2017
RAIS wa  Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa Zanzibar imeweza kupata mafanikio makubwa ya maendeleo lakini yamekuwa yakivizwa kutokana na kutokuwepo kwa takwimu sahihi na zinazokwenda na wakati.

Dk. Shein aliyasema hayo leo huko katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi la zamani, MnaziMmoja Mjini Zanzibar wakati akifungua Semina ya siku moja kwa Viongozi na Watendaji wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuhusu Umuhimu wa Takwimu na Matumizi yake.

Katika maelezo yake, Dk. Shein alisema kuwa hakuna  sababu ya kuyabeza maendeleo makubwa yaliopatikana hapa nchini lakini kuna kila sababu ya kutatua changamoto ya kutokuwepo kwa takwimu sahihi katika taasisi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Dk. Shein ambaye pia, alikuwa Mwenyekitiwa Semina hiyo, alisema kuwa kutokana na hali hiyo ndio maana akaona haja ya kuandaliwa mafunzo hayo ambayo yatasaidia kwa kiasi kikubwa kufikia malengo yaliokusudiwa ambapo mwishoni yatakuja na maazimio ambayo hatimae yatafanyiwa kazi.

Aidha, Dk. Shein alisema kuwa hakuna jambo lolote la maendeleo linaloweza kufanyika na kufanikiwa bila ya kuwepo kwa takwimu sahihi na ufanyaji tafiti huku akisisitiza kuwa upatikanaji wa takwimu sahihi na kwa wakati ni msingi muhimu katika kupanga na kutekeleza mipango yote ya maendeleo.

Kwa maelezo ya Dk. Shein alieleza kuwa juhudi mbali mbali zimechukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kutatua changamoto hiyo ikiwa ni pamoja na kuunda Idara ya Sera na Utafiti, Sheria ya Takwimu lakini bado changamoto hizo zimekuwepo, hivyo aliwataka washiriki wa Semina hiyo kufuatilia kwa makini mafunzo hayo na hatimae kufanyiwa kazi ipasavyo.

Sambamba na hayo, Dk. Shein alisema kuwa kwa upande wa Takwimu Zanzibar imekuwa ikifanya vizuri na kutumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.  

Pia, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee,Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana pamoja katika kuandaa  Semina hiyo.

Dk. Shein pia, alivutia na juhudi za makusudi zilizochukuliwa na uongozi huo  kwa kuanza kutekeleza vizuri maagizo yake tisa aliyoyatoa siku ya tarehe 6 Januari mwaka huu, wakati alipoweka jiwe la msingi kwenye jengo jipya la Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar huko Mazizini Mjini Zanzibar, na kusisitiza kuwa hiyo ndio kasi anayoitaka.

Nae Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Khalid Salum Mohammed alisema kuwa Semina hiyo yametokana na agizo lake alilolitoa siku hiyo katika ufunguzi wa jengo jipya la Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Aidha, Dk. Khalid alisema kuwa mbali ya agizo hilo pia, tayari wameshaanza kuyafanyia kazi maagizo mengine kati ya maagizo tisa aliyoyatoa Rais likiwemo ujenzi wa Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali huko Pemba ambapo tayari mchakato wake unaendelea na jengo hilo linatarajiwa kujengwa huko Gombani katika jengo jipya la ghorofa la Wizara ya Fedha na Mipango.

Pia, Dk. Khalid aliongezea kuwa katika agizo la mafunzo kwa wafanyakazi wa Ofisi hiyo ya Mtakwimu Mkuu, tayari zoezi hilo linaendelea na wafanyakazi wawili wamepatiwa nafasi za masomo maalum juu ya kada hiyo ya takwimu na kwa kila mwaka kwa miaka mitatu ijayo mpango huo utaendelezwa.

Katika mafunzo hayo mada mbali mbali ziliwasilishwa zikiwemo Muhtasari wa Majukumu ya Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali katika upatikanaji wa Takwimu na utekelezaji wake, Umuhimu wa Takwimu, Hatua za uzalishaji na Matumizi yake, Takwimu za Sekta ya Kilimo, Takwimu za Sekta ya Viwanda na Takwimu za sekta za Huduma.

Akitoa mada juu ya Muhtasari wa Majukumu ya Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali katika upatikanaji wa Takwimu na utekelezaji wake Bi Mayasa Mahfoudh Mwinyi alisema kuwa Ofisi hiyo ina jukumu kubwa la kusimamia kikamilifu upatikanaji wa takwimu bora nchini.

Kwa maana kwamba takwimu zinazotolewa zinatakiwa zikidhi vigezo vilivyowekwa vikiwemo usahihi, kukidhi vigezo katika ngazi husika ziwe zinalingana na zinatolewa kwa wakati ili kukidhi haja ya watumiaji wa takwimu hizo yakiwemo maitaji ya Taifa.

Sambamba na hayo, Bi Mayasa alisema kuwa Ofisi hiyo imeweza kuwajengea uwezo kitaalamu wafanyakazi wake ili waweze kutekeleza majuku yao kwa ufanisi zaidi ambapo jumla ya wafanyakazi 30 wamepatiwa mafunzo katika ngazi ya Shahada na Shahada ya Uzamili ndani ya kipindi cha miaka 10 na wafanyakazi 150 wa Ofisi hiyo ambao wamepata mafunzo mafupi mafupi.

Viongozi mbali mbali walihudhuria katika Semina hiyo akiwemo Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi SeifAli Idd pamoja na viongozi wengine na watendaji wa Serikali.
  
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.