STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 26.2.2017
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Ali Mohamed Shein amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imedhamiria
kuzipandisha hadhi Hospitali ya Kivunge na Makunduchi kuwa za Mkoa katika
kipindi kifupi kijacho.
Dk. Shein aliyasema
hayo katika chakula cha usiku kilichoandaliwa na Wizara ya Afya kwa ajili ya
kuchangia fedha za kusaidia Hospitali ya Makunduchi na Hospitali ya Kivunge
ikiwa ni pamoja na maadhimisho ya miaka kumi ya Mradi wa kuendeleza huduma za
afya Zanzibar (HIPZ), huko katika ukumbi wa Hoteli ya Park Hyatt mjini
Zanzibar.
Katika hotuba yake, Dk.
Shein alisema kuwa juhudi za Mradi wa kuendeleza huduma za afya Zanzibar
(HIPZ), sio tu umeweza kusaidia kuziweka hospitali za Makunduchi na Kivunge
katika hali nzuri na bora katika utoaji wa huduma lakini amesema mradi huo
umesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza msongamano wa wagonjwa katika hospitali
kuu ya Mnazi Mmoja.
Dk. Shein alitumia
fursa hiyo kutoa shukurani kwa uongozi wa Mradi huo wa HIPZ kwa kuweza kuimarisha
huduma za afya, miundombinu, usimamizi na uwajibikaji katika Hospitali hizo.
Aliongeza kuwa Mradi
wa HIPZ umesaidia sana kutekeleza azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuzifanya
Hospitali hizo kuwa na hadhi ya Hospitali ya Wilaya hali ambayo imeonesha njia
ya kutekeleza lengo la kuzifanya Hospitali hizo kuwa za Mkoa.
Aidha, Dk. Shein
alitoa wito kwa Wizara ya Afya kuimarisha utoaji mafunzo kupitia Maradi huo kwa
madaktari wazalendo kupitia madaktari wageni wanaokuja kufanya kazi Zanzibar
kupitia katika Mradi huo wa HIPZ.
Pamoja na hayo, Dk.
Shein alitoa wito kwa wananchi kuendelea kuzitumia huduma zinazotolewa na
wataalamu wa HIPZ kupitia Hospitali ya
Kivunge na Makunduchi badala ya
kukimbilia Hospitali Kuu ya MnaziMmoja.
Dk. Shein katika alieleza
juhudi za Serikali katika kuimarisha sekta ya afya nchini ikiwa ni pamoja na
kuimarisha huduma za afya, ujenzi wa Hospitali ya Abdalla Mzee, Hospitali ya
Mnazi Mmoja, kuimarisha miundombinu ya hospitali, vifaa na mafunzo huku
akieleza kuwa Serikali imeongeza Bajeti ya Wizara ya Afya kutoka Tsh. Bilioni 4.3
mwaka 2015/2016 hadi kufikia Bilioni 4.9 katika mwaka wa fedha wa 2016/2017.
Katika maelezo yake
kwenye hotuba hiyo Dk. Shein alisema kuwa Mradi huo wa HIPZ umeimarishwa kwa mashirikiana
kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzbar pamoja na madaktari kutoka nchini
Uingereza, Canada na sehemu nyengine duniani.
Pamoja na hayo, Dk.
Shein aliwaahidi viongozi wa Mradi huo kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Znzibar
itaendea kuwaunga mkono ili Mradi huo uwe endelevu na uweze kufanya kazi
vizuri.
Alitumia fursa hiyo
pia, kuwashukuru Washirika wa maendeleo kwa kuendeleza aushirikiano na Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha huduma za afya.
Katika hafla hiyo jumla
ya Tsh. Milioni 67 zilichangwa katika harambee ilioendeshwa ukumbini hapo
ambapo Dk. Shein alichangia milioni kumi pamoja na Mama Mwanamwema Shein nae alichangia
milioni tano.
Nae Waziri wa Afya,
Mahamoud Thabit Kombo kwa upande wake alieleza mashirikiano mazuri yaliopo kati
ya HIPZ na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara yake ya Afya na
kumpongeza Rais Dk. Shein kwa kuwa kiungo kati Wizara hiyo na Mradi huo
wa HIPZ.
Nao viongozi wa HIPZ
kwa nyakati tofauti walieleza mafanikio na changamoto walizokabiliana nazo
ndani ya miaka kumi ya Mradi huo na kuahidi kuendelea kuiunga mkono Serikali
katika kuimaruisha sekta ya afya hapa nchini.
Sambamba na hayo
walieleza mashirikiano mazuri waliyoyapata kutoka Serikalini pamoja na kutoka
kwa washirika mbali mbali wa maendeleo.
Mradi wa HIPZ ulianzishwa
mwaka 2006 ambao unafanyakazi chini ya Wizara ya Afya ili kuimarisha huduma
zote za afya za Hospitali ya Makunduchi na Kivunge.
Viongozi mbali mbali
walihudhuria katika hafla hiyo akiwemo Makamo wa Pili wa Rais Balozi Seif Idd,
Mama Asha Balozi, Mawaziri, viongozi Serikali na viongozi wa HIPZ wakiongozwa na Dk. Ruaraidh Mac Donagh pamoja na wageni
wengine.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address:
2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment