Habari za Punde

Msiwatumie ‘makaka poa’ kwenye harusi: Dc Chakechake

Na. Haji Nassor. Pemba.
Jamii nchini, imeshauriwa isiwatumie wanaume wanaofanyiwa au wanafanya matendo ya udhalilishaji ‘makaka poa’ katika kupamba au kusherehesha harusi ndani ya familia.

Kauli hiyo imetolea na Mkuu wa wilaya ya Chakechake Salama Mbaruok Khatib, alipokuwa akifungua mkutano wa wadau, kuhusu hifadhi na ushirikishwaji wa mtoto ulioandaliwa na shirika la SOS na kufanyika Chakechake Pemba.

Alisema, familia zinazopendelea kuwapa kipaumbele vijana hao na kuwakabidhi kupamba au kusherehesha kwenye shughuli za harusi, ni kuchochea na kuyapalilia matendo hayo ndani jamii.

Mkuu huyo wa wilaya alieleza kuwa, udhalilishaji wanaofanyiwa wanaume na watoto wengine wa kike sio jambo jema, hivyo kuendelea kuwatumia ni kuonyesha tendo hilo linakubalika ndani ya jamii.

“Jamani, sisi jamii wapo wenzetu ambao wamekuwa wakifanyiwa udhalilishaij “makaka poa” tuacheni kuwatumia kwenye harusi, maana itatafsiriwa kuwa hilo wanalofanyiwa, kama vile linakubalika ndani jamii, jambo ambalo sio sahihi”,alisema.

Hata hivyo Mkuu huyo wa wilaya, ameisisitiza jamii kuendelea kuwalea watoto na kuwapatia haki zao kadhaa za msingi ikiwemo elimu, ili kuwajengea mazingira madhubuti hapo baadae.

Mapema Mratibu wa shirika la SOS Pemba, Husna Juma alisema, kila mmoja anawajibu na jukumu la kumlinda mtoto ndani ya jamii, badala ya kugawana majukumu.

Alieleza kuwa, suala la kumlinda, kuimarisha na kuzienzi haki za mtoto, haliko kwa wazazi na walezi pekee, bali hata ndugu, jamaa na marafiki wanalojukumu hilo.

Katika hatua nyengine, alifafanua kuwa mpango wa kuwaweka pamoja na kuwapa malezi yanayokidhi haja, yalianza tokea baada ya vita vya pili vya dunia, na hadi leo matunda yameshapatikana.

“Mpango wa kuanzisha kijiji cha SOS kwa Tanzania kimeanza Zanzibar na sasa pia mwaka 2007 kumeshaanzishwa mpango wa kuwafuata watoto ili kuwapatia huduma husika’’,alifafanua.

Baadhi ya washiriki wa mkutano huo, wamesema kazi kubwa ipo kwa jamii, kuendelea kushirikiana ili kuwadhibiti watoto wasikose malezi na matunzo.

Siti Habib kutoka Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar ZLSC tawi la Pemba, alisema wenyewe wamekuwa na mpango wa mkakati wa kutoa mafunzo ili watoto wazielewe haki zao.

Nae Seif Mohamed Seif kutoka wizara ya elimu, alisema wamekuwa wakijitahidi kuhakikisha hakuna mtoto anaefikia umri wa kusoma, kukosa haki hiyo.

Mkutano huo wa siku mbili wa wadau wa hifadhi na ushirikishwaji wa mtoto, umeandaliwa na SOS ikiwa ni miongoni mwa mikutano yao na wadau katika kulinda mtoto.

Shirika la watoto la SOS ambayo kisiwani Pemba haina kijiji kama kilichoko kisiwani Unguja, ingawa ina watoto zaidi ya 800, ambao huwafikia kwa kuwapa huudma moja kwa moja na kuziwezesha familia zao, kujengewa uwezo ili waweze kujitegemea. 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.