Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kulia) akisalimiana na Balozi wa Shirikisho la Urusi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe,Yuri Fedorovich Popov alipofika Ikulu Mjini Zanzibar kwa mazungumzo na Rais leo asubuhi,[Picha na Ikulu.] 23 /02/2017.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kulia) akizungumza na mgeni wake Balozi wa Shirikisho la Urusi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe,Yuri Fedorovich Popov alipofika Ikulu Mjini Zanzibar leo asubuhi,[Picha na Ikulu.] 23 /02/2017.
STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 23.2.2017
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Ali Mohamed Shein ameeleza kuwa
kuimarika zaidi kwa uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo kati ya Urusi
na Zanzibar kutazidisha juhudi za kukuza uchumi hasa katika sekta ya utalii
ambayo Zanzibar imepiga hatua.
Dk. Shein aliyasema
hayo leo Ikulu mjini Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo na Balozi wa Urusi
katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Yuri Fedorovich Popov ambapo katika
mazungumzo hayo balozi huyo alimuahidi Dk. Shein kuwa Urusi itazidisha uhusiano
na ushirikiano kati yake na Zanzibar.
Katika maelezo yake
Dk. Shein alisema kuwa ipo haja ya kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano huo
uliopo kati ya nchi hizo kwa kutambua kuwa thamani yake ni kubwa katika
maendeleo kwa pande zote mbili.
Dk. Shein alisema kuwa
Urusi ni nchi moja wapo inayotoa watalii wengi duniani ambao sio wengi
wanaozitembelea nchi za Bara la Afrika ikiwemo Tanzania, hivyo alisisitiza haja
ya mashirikiano ya pamoja kati ya pande mbili hizo katika kuifanyia kazi sekta
hiyo ambayo nimuhimukatika kukuza uchumi na maendeleo hapa nchini.
Dk. Shein aliongeza
kuwa kurejea huduma za usafiri wa ndege kati ya Tanzania na Urusi kama
ilivyokuwa hapo siku za nyuma kupitia Shirika lake la
ndege la “Aeroflot”, kutasaidia
kwa kiasi kikubwa kuikamarisha sekta ya utalii hapa nchini kwani itasaidia
kuleta watalii kutoka nchi hiyo moja kwa moja.
Sambamba na hayo, Dk.
Shein alimueleza Balozi huyo haja ya kuendeleza na kuongeza nafasi za masomo
kwa vijana wa Zanzibar wanaokwenda nchi hiyo kwa ajili ya kusoma katika kada
mbali mbali za elimu ya juu.
Akizungumzia kuhusu
sekta ya biashara, Dk. Shein alisema kuwa Tanzania ikiwemo Zanzibar ina
historia kubwa katika sekta ya biashara kati yake na Urusi hivyo ipo haja kwa
hatua hiyo kurejeshwa kama ilivyokuwa siku za nyuma.
Aidha, Dk. Shein aliipongeza Serikali
ya Urusi kwa kuendeleza uhusiano na ushirikiano wa karibu kati yake na Zanzibar
na kueleza kuwa nchi hiyo ni miongoni mwa nchi za mwanzo kufungua Ubalozi wake
hapa Zanzibar mara tu baada ya Mapinduzi ya Januari 12, mwaka 1964.
Hivyo, Dk. Shein aliitilia mkazo rai ya Balozi
Yuri Popov ya kuimarisha uhusiano kama ilivyokuwa katika miaka ya 1970 na 1980
ambapo Urusi iliimarisha zaidi uhusiano huo na Tanzania ikiwemo Zanzibar kwani
pia, nchi hiyo ni miongoni mwa nchi za mwanzo kuyatambua Mapinduzi ya Zanzibar
ya Januari 12, 1964.
Nae Balozi wa Urusi katika Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Yuri Fedorovich Popov alimuhakikishia Dk. Shein kuwa Urusi
itaendelea kushirikiana na kuiunga mkono Zanzibar kwa kutambua uhusiano na
ushirikiano mwema wa kihistoria uliopo.
Katika maelezo yake, Balozi Yuri alieleza
kuwa Urusi inatambua umuhimu wa kuimarisha uhusiano na ushirikiano huo ambao
utakuza maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa pande zote mbili.
Kwa upande wa sekta ya utalii, Balozi Popov
alieleza kuwa juhudi za makusudi zitachukuliwa katika kuhakikisha usafiri wa
ndege kati ya Urusi na Tanzania utarejeshwa ili kukuza sekta hiyo ya utalii pamoja
na sekta ya biashara na shughuli za uwekezaji.
Alieleza kuwa kwa upande wa sekta nyengine za
maendeleo nchi yake itaongeza nguvu zaidi katika kuhakikisha mafanikio zaidi
yanapatikana katika sekta hizo ili kuimarisha uchumi na maendeleo kwa nchi
mbili hizo.
Pamoja na hayo, Balozi Popov alitumia fursa
hiyo kumpongeza Rais Dk. Shein kwa kuendelea kuwa Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kipindi cha Pili pamoja na kuwapongeza
wananchi wa Zanzibar huku akiahidi kuwa wananchi wa Urusi wataendeleza
ushirikiano na ndugu zao wa Zanzibar.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address:
2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment