Habari za Punde

Rais wa Zanzibar Dk Shein Atembelea Majengo ya Tume Maisara.


STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
 Zanzibar                                                                                                           13.2.2017
---
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa Tume zote duniani zina majengo na ofisi zinazofanana na hadhi na kazi zinazofanywa na ofisi hizo hivyo, Serikali anayoiongoza itahakikisha Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) inapata ofisi zinazokwenda na wakati kabla ya uchaguzi ujao wa mwaka 2020. 

Dk. Shein aliyasema hayo leo mara baada ya kufanya ziara fupi ya kulitembelea jengo la Ofisi za Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar huko Maisara mjini Zanzibar, ikiwa ni ahadi yake aliyoitoa hivi karibuni wakati alipokabidhiwa ripoti ya uchaguzi wa tarehe 25 Oktoba pamoja na uchaguzi wa Marudio wa tarehe 20 Machi 2016 na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar Jecha Salim Jecha kuwa leo atazitembelea Ofisi hizo.

Katika maelezo yake Dk. Shein alisema kuwa Tume zote za uchaguzi  duniani  zipo katika mazingira na sehemu nzuri kwa kutambua kuwa chombo kinachosimamia uchaguzi ni lazima kiwe katika mazingira mazuri yanayoendana na hadhi yake hivyo, lazima Serikali ifanye juhudi za kuhakikisha Ofisi za Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar inakuwa katika mazingira mazuri.

Dk. Shein alisema kuwa ni vyema wakati uchaguzi wa mwaka 2020 ukiandaliwa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) iwe na Ofisi nzuri na zenye nafasi kwa ajili ya kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi pamoja na vifaaa na vitendea kazi imara yakiwemo magari na kuahidi kuwa Serikali anayoiongoza itafanya juhudi katika kuhakikisha changamoto hiyo inapata ufumbuzi.

Alisema kuwa kwa upande wa Tume ya Uchaguzi ya Taifa (NEC) tayari inampango wa kujenga jengo lake huko Dodoma ambalo litakuwa na mazingiza mazuri hivyo, kwa upande wa Zanzibar Ofisi hizo za Tume nazo ni vyema zikawa zinaenda na wakati uliopo kwa kuwa na majengo yanayoendana na hadhi ya Tume.


Kutokana na hilo, Dk. Shein aliahidi suala hilo kupatiwa ufumbuzi na jawabu muwafaka litapatikana haraka iwezekanavyo na kusema kuwa wakati wowote jibu muwafaka litapatikana kama Serikali itajenga jengo jipya ama kufanyiwa ukarabati au upanuzi kwa majengo yaliopo sehemu hiyo likiwemo jengo jengine pembezoni mwa Ofisi za Tume hizo ambalo halitumiki kwa sasa.

“Nitafanya maamuzi leo na mchana huu tutakuwa na kikao na tutaamua na kukuarifuni maamuazi tuliyoamua juu ya ujezi wa Ofisi ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar”,alisisistiza Dk. Shein.

Aidha, Dk. Shein alielendelea kuwasisitiza viongozi na wafanyakazi wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar waendelee kufanya kazi zao na kujituma huku akiwaahidi kuwa Serikali yao ya Mapinduzi ya Zanzibar ipo na itaendelea kuwaunga mkono na wala wasiwe na wasi wasi.

Mapema Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Jecha Salim Jecha  alitoa pongezi zake kwa niaba ya Tume hiyo kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein kwa kufanya ziara yake hiyo ya kuzitembelea Ofisi za Tume hiyo kutokana na ombi lake alilolitoa kwa Rais hivi karibuni.

Mwenyekiti huyo wa Tume ya Uchaguzi alitumia fursa hiyo kueleza changamoto wanazozipata kutokana na ufinyu wa nafasi katika ofisi zao sambamba na mahitaji yao ya vifaa na vitendea kazi vyengine yakiwemo magari.

Katika ziara hiyo Dk. Shein alitembelea sehemu mbali mbali za ofisi hiyo na kupata maelezo kutokana na changamoto ya ufinyu wa nafasi za ofisi za Tume hiyo, pia, alioneshwa kiwanja kiliopo pembeni ya jengo la Tume hiyo pamoja na kukagua, jengo ambalo halitumiki kwa hivi sasa ambalo liko pembezoni mwa ofisi za Tume hiyo.

Viongozi mbali mbali wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, waliungana na Rais Dk. Shein katika ziara hiyo fupi ambayo pia, ni muhimu akiwemo Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd, Mawaziri, Makamishna na viongozi wengine wa Serikali.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.