Na Salmin Juma, Pemba
Mwakilishi wa Jimbo la Ziwani Suleiman Makame Ali ameitaka jamii na wafadhili kutoa ushirikiano katika miradi ilioanzishwa na wajasiriamali wadogo wadogo ambao wameonesha muelekeo wa kutaka kujiajiri wenyewe ili kujikwamua kimaisha.
Amesema hayo wakati alipokuwa akitembelea mradi wa mabwawa ya ufugaji wa samaki katika kikundi cha "Tujipange sote" huko Ndagoni, wilaya ya Chake Chake Pemba.
Amesema kuwa nivyema kwa vijana kutumia fursa zitolewazo Serikalini pamoja na kutumia ufugaji wa kisasa ili kuendana na wakati uliopo .
Aidha ameisa jamii kuacha tabia ya wizi na uharibifu wa mazao na mifugo na yeyote atakaefanya uharibifu hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
Nae Katibu wa kikundi hicho Hamad Mwahenzi Mdachi, amesema katika mradi wao bado hawana elimu ya kutosha na kuiomba Serikali iwasaidie kupata wafadhili na elimu ya ufugaji wa samaki iweze kuwasaidia katika harakati zao.
Mshika fedha wa kikundi hicho Halima Ali Sefu ametoa wito kwa jamii kuacha tabia ya kukaa barazani nabadala yake waunde Vikundi vya ushirika na kubuni miradi mbali mbali ili kujikwamua na hali ya utegemezi katika jamii zao.
Amesema mradi wao kwa sasa una wanachama 20 wanawake 13 na wanaume 7 ambapo wanajishughulisha na ufugaji wa Samaki ,Nyuki na upandaji wa Mikoko ambapo zaidi ya mikoko elfu 21 tayari imeshapandwa.
No comments:
Post a Comment