Habari za Punde

Waziri Hamad Rashid Awataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya Kudhibiti Uchimbaji wa Mchanga Kuepeka Athari za Kimazingira.


















WAZIRI wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Mhe. Hamad Rashid Mohammed (Wa tatu kutoka kushoto), akizungumza na wakuu wa mikoa, wilaya, wawakilishi wa vyombo vya ulinzi na watendaji wa wizara yake juu ya hatua za serikali kupunguza kasi ya uchimbaji na utumiaji mchanga. Wengine kutoka kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Kusini Dk. Idrissa Muslim Hijja, Katibu Mkuu WKMMU Juma Ali Juma na Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Vuai Mwinyi Mohammed. (Picha na Salum Vuai-MAELEZO).


Na Salum Vuai, Maelezo Zanzibar.

WAZIRI wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Hamad Rashid Mohammed, amesema iwapo uchimbaji wa mchanga hautadhibitiwa, kuna hatari ya kuisababishiaZanzibar janga la kimazingira na balaa la njaa.

Akizungumza na Wakuu wa Mikoa na Wilaya za Unguja katika ukumbi wa Kilimo-ASSP Maruhubi mjini Unguja, Hamad amesema licha ya serikali kutoa tamko la kumalizika kwa mchanga bado kuna watu wasitaka kufuata maelekezo wanayopewa.

Alisema baada ya wizara kutangaza mkakati wa serikali na kuwataka wananchi wakubali kubadilika na kuhama kwenye matumizi ya mchanga, kumejitokeza watu wanaokaidi agizo hilo na kujaribu kuipima ubavu serikali kwa kubuni njia za panya za kuchimba na kutorosha rasilimali hiyo.

Aidha, alisema wajanja hao wanaokwenda mashimoni nyakati za usiku kwa kuvizia, wanatumia mwanya wa tahadhari iliyotolewa, kuuza mchanga kwa bei kubwa huku wakikwepa kulipa kodi serikalini.

Akitoa mfano wa hivi karibuni, alisema katika doria iliyofanywa usiku wa kuamkia jana Wilaya ya Kaskazini ‘B’ baada ya kupata taarifa za kuwepo watu wanaochimba mchanga kuanzia saa tano usiku, gari kadhaa zilikamatwa zikiwa zimesheheni mchanga bila ya kuwa na kibali.

“Tumezipeleka kituo cha polisi Mahonda ili wahusika wachukuliwe hatua kwa kuchimba mchanga bila kibali tena kwa wakati wa usiku ambao hauruhusiwi,” alieleza Waziri huyo.
Aidha, alisema amemuagiza mkuu wa kituo hicho kuandika ripoti juu ya kadhia hiyo na kuiwasilisha katika idara husika ili kujiridhisha baada ya ripoti ya awali kutofautiana na ile ya kikosi cha doria.    

Kutokana na hali hiyo, Waziri Hamad amewataka wakuu wa mikoa na wilaya kushirikiana na Wizara yake katika kusimamia mpango wa kudhibiti uchimbaji na biashara ya mchanga nchini.

Aidha, jeshi la polisi, vikosi vyengine na kamati za ulinzi na usalama pia vimekumbushwa wajibu wao katika kuhakikisha vinafuatilia na kuchukua hatua kwa wote watakaopatikana wakikiuka utaratibu wa uchimbaji wa rasilimali hiyo uliowekwa na serikali.     

Akifafanua zaidi alisema, kukaidi maelekezo ya serikali kuna athari kubwa kwa kuwa watu wanaotaka mchanga hulazimika kukata miti ikiwemo minazi na miembe, na kwa bahati mbaya ardhi hiyo ni yenye rutuba na inategemewa kwa kilimo.

Katika hali kama hiyo, alionesha wasiwasi wake kuwa, iwapo watu wataachiwa waendelee kuvuna rasilimali ya mchanga kiholela, vizazi vijavyo  havitakuta urithi wa ardhi inayofaa kwa shughuli za uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara.

“Kama tunataka kukaribisha ardhi kame na njaa, basi tuwaachie watu wafanye watakavyo. Vita hivi ni vigumu na ni vya kila mmoja wetu. Lazima tubadilike kwani kuna malighafi nyingi na rahisi zinazoweza kutumiwa kwa shughuli za ujenzi, tusing’ang’anie mchanga ambao kwa kweli umekwisha,” alisisitiza. 

Kwa hivyo aliwaomba  wakuu hao wa mikoa, wilaya, masheha na madiwani washirikiane na vyombo vya ulinzi pamoja na kutoa elimu kwa wanachi ili malengo ya serikali yaweze kufikiwa ikizingatiwa hayalengi kumkomoa mtu bali yanaangalia mustakbali mwema wa nchi na watu wake.

Wakizungumza kwenye kikao hicho, wakuu hao wa mikoa na wilaya, walisema wako tayari kubeba dhamana hiyo wakitambua athari iliyopo mbele ambayo walikiri imeanza kujionesha kwenye maeneo yao.

Akielezea uzoefu wa mkoa wa Mjini Magharibi katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zikiwemo za kiuhalifu, Mkuu wa mkoa huo Ayoub Mohammed Mahmoud, alisema iwapo wizara imekusudia kwa dhati kupambana na uharibifu wa rasilimali zilizopo, ni lazima ijipige kifua na kuvumilia vikwazo vitakavyoingia katikati ya safari hiyo.

Aidha, alisema tayari ofisi yake imeshaunda kikosi kazi ambacho pamoja na majukumu mengine, pia kitapewa kazi ya kufanya doria na kuwashughulikia watakaokiuka utaratibu wa kuchimba mchanga.

Alisema kikosi hicho kitatangazwa na kuanza kazi rasmi baada ya wiki moja.

Mapema, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Juma Ali Juma, alisema ni juu ya serikali za mikoa na wilaya, kukaa na wananchi wa maeneo yao na kuwaelimisha juu ya janga linaloinyemelea nchi iwapo wataendelea na misimamo hasi wakikataa kufuata maagizo ya serikali.
CAPS:

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.