Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Azungumza na Mkuu wa Majeshi Tanzania Ofisini Kwake Vuga.

Mkuu Mpya wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Tanzania Generali Venance Mabeyo kushoto  akisalimiana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipofika Ofisini kwakeVuga Mjini Zanzibar  kujitambulisha  rasmi baada ya kuteuliwa hivi karibuni na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli  kushika wadhifa huo. 
Generali Venance Mabeyo kushoto akimuhakikishia Balozi Seif  jukumu la Majeshi ya Ulinzi na Usalama Tanzania kuendelea kusimamia amani kwa nguvu zake zote.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kati kati akiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Tanzania Generali Venance Mabeyo kulia yake.Kushoto ya Balozi Seif ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohamed Aboud Mohamed.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohamed Aboud Mohamed  Kulia akiagana na Mkuu wa  Majeshi ya Ulinzi na Usalama Tanzania Generali Venance Mabeyo  mara baada ya mazungumzo yao.
Aliyepo kati kati yao akiwashuhudia ni Makamau wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.

Picha na – OMPR – ZNZ.

Na Othman Khamis OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema nguvu na sifa za kiulinzi zilizojengeka ndani ya Majeshi ya Ulinzi na Usalama ya Tanzania katika nyanja za Kimataifa itabaki kuwa Historia endapo nidhamu ndani ya Majeshi hayo itaendelea kuwa ya kudumu.

Alisema suala la nidhamu ambalo ndilo kigezo pekee kilichopelekea Umoja wa Mataifa kuyaamini Majeshi ya Tanzania katika ulinzi wa amani katika Nchi zenye migogoro ya vita vya wenyewe kwa wenyewe  hasa Barani Afrika linapaswa kusimamiwa kwa nguvu zote.

Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati akizungumza na Mkuu Mpya wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Tanzania Generali Venance Mabeyo aliyeteuliwa hivi karibuni na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli ambae alifika kujitambulisha rasmi Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Alisema umahiri wa Majeshi hayo katika ulinzi wa Kimataifa,Kitaifa, Raia, pamoja na Mali zao umepelekea kuaminika vyema kitendo ambacho kimewapa faraja Wananchi walio wengi hapa Nchini pamoja na Mataifa wanayopangiwa kusimamia Ulinzi wa Amani.

Hata hivyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema zipo baadhi ya changamoto zinazoyakabili Majeshi hayo ya Ulinzi na Usalama Nchini, lakini umahiri uliopo wa Viongozi na Maafisa wa Vikosi hivyo changamoto hizo zitapungua au kuondoka kabisa.

Akigusia migogoro iliyowahi kijichomoza kati ya Kambi za Vikosi vya Ulinzi na Baadhi ya Wananchi wanaoishi pembezoni mwa Kambi hizo Balozi Seif alisema Vikao vya pamoja kati ya Viongozi wa Serikali kwa kushirikiana na Maafisa wa Vikosi husika na Wananchi hao vimesaidia kuondosha migogoro hiyo.

Balozi Seif aliwashauri Wananchi kujiepusha na tabia ya kuyatumia maeneo yaliyo karibu na Kambi za ulinzi kwa kujenga nyumba za makaazi ya kudumu au kulima ili kujikinga na hitilafu zinazoweza kutokea za miripuko ya silaha nzito ambazo baadae huleta athari za kiafya au wakati mwengine vifo.

Mapema Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Tanzania Generali Venance Mabeyo alimuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba majeshi ya Ulinzi na Usalama ya Tanzania  yataendelea kuwajali na kuwaheshimu Wananchi kwani wao ni sehemu ya Majeshi hayo.

General Mabeyo alisema vijana wanaounda Majeshi hayo  ya Ulinzi ni miongoni mwa Watoto, ndugu na Jamaa wa damu wa Wananchi wa Taifa hili wanaohitaji kuendelea kupewa ushirikiano utakaodumisha upendo na mshikamano wa pande mbili husika.

Mkuu huyo wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Tanzania amezishukuru Serikali zote mbili za Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuyawezesha Majeshi hayo kutekeleza vyema majukumu yao ya ulinzi ya kila siku.

Alieleza kwamba Majeshi hayo yako tayari kuendelea kupokea maagizo, ushauri na hata msaada kutoka kwa Viongozi wa Kitaifa  na Wananchi na Raia wema katika kuona usalama na amani wa Taifa la Tanzania unaendelea kushamiri wakati wote.

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Tanzania Generali Venance Mabeyo ameanza kushika wadhifa huo katika miezi ya hivi karibuni baada ya aliyekuwa akishikilia nafasi hiyo Genarali Davis Mwamunyage kumaliza muda wake wa utumishi kwa mujibu wa Sheria.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.