Habari za Punde

‘Ni aibu wanafunzi wa Zanzibar kufeli Kiswahili’

 MHADHIRI wa Chuo Kikuu Huria Tanzania Profesa Kijiti Shaaban Sengo, akizungumza na washiriki wa uzinduzi wa Chama cha Kiswahili Zanzibar (CHAKIZA) uliofanyika katika Chuo cha Habari Zanzibar leo Machi 11, 2017.
.

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Bi. Khadija Bakari Juma, akiwahutubia washiriki wa hafla ya uzinduzi wa Chama cha Kiswahili Zanzibar (CHAKIZA) uliofanyika leo katika ukumbi wa Chuo cha Habari Zanzibar, ulioko Kilimani mjini Unguja.
PICHA zote na Idara ya Habari Maelezo-ZANZIBAR


Na Salum Vuai, ZANZIBAR

WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Amali imeeleza kusikitishwa kwake na idadi ndogo ya wanafunzi waliofaulu mtihani wa lugha ya Kiswahili, ambao walifanya mtihani wa kidato cha pili mwaka 2016.

Katibu Mkuu wa wizara hiyo Khadija Bakari Juma, akizungumza katika uzinduzi wa Chama cha Kiswahili Zanzibar (CHAKIZA) uliofanyika kwenye ukumbi wa Chuo cha Habari Zanzibar, alisema inasikitisha kuona wanafunzi hao ambao ni Waswahili kwa asili, wanafanya vibaya kwenye mtihani wa somo hilo.

Akiwahutubia washiriki wa hafla hiyo kwa niaba ya Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Katibu Mkuu huyo alisema, matokeo ya mtihani huo yameonesha  wanafunzi wengi walipata chini ya asilimia 50 katika 100.

Alieleza kuwa, matokeo hayo hayastahili kwa wanafunzi waliozaliwa katika mifupa ya Waswahili wa kweli ambao sio wa kujipaka.

Hata hivyo, alisema hali hiyo imesababishwa na watu wengi hapa Zanzibar kuidharau lugha ya Kiswahili na kuzitukuza za kigeni, kwa dhana ya kukubalika kwenye soko la ajira la kimataifa.

Alisema katika ulimwengu wa sasa ambapo hata Kiswahili kinafundishwa hata ngazi ya uzamili na uzamivu, vyuo vingi duniani vinahitaji walimu wa somo hilo hivyo sababu ya kukosa ajira kwa kusoma sana Kiswahili haina mashiko.

Aidha, Khadija alisema misamiati mingi ya lugha ya Kiswahili imekuwa ikipotea kwa kuwa wazazi hawajali kuwaongoza watoto wao pale wanapotamka maneno ya lugha hiyo kimakosa na kuwaacha wakiiharibu lugha hiyo.

“Ni matumaini yangu kwamba kuzinduliwa kwa chama hiki kutaakisi dhamira ya kuundwa kwake ambayo ni kuhakikisha hadhi ya Kiswahili inarudi kama ilivyokuwa awali licha ya kukabiliwa na changamoto za usasa unaotokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia,” alieleza.

Mapema, Mwenyekiti wa CHAKIZA Maalim Hamad Bakari Mshindo, alisema chama hicho hakikuanzishwa kwa ajili ya kushindana na vyama vyengine vilivyotangulia ambavyo lengo lao ni kuiendeleza na kuitetea lugha ya Kiswahili.

Alisema madhumuni ya kuundwa kwa CHAKIZA, ni kushirikiana na vyama hivyo katika kazi ya kuijengea hadhi na kuiimarisha lugha ya Kiswahili ambayo sasa imeanza kuchafuliwa hasa na watu wasioijua.

Mshindo alifahamisha kuwa, CHAKIZA hakitakuwa tu chama cha kuandaa makongamano na semina, bali kitajikita zaidi katika kazi ya kuandika vitabu na machapisho mbalimbali yanayotoa muongozo wa kukiendeleza Kiswahili kikanda na kimataifa.
Naye Katibu Mkuu wa chama hicho Daudi Mohammed Ali, alisema nguvu ya jumuiya yoyote hutokana na wingi wa wanachama wake, hivyo akatoa wito kwa Wazanzibari wote kujiunga na chama hicho bila kujali nafasi au taaluma zao.
“Yumkini watu wengi wanadhani kwamba CHAKIZA ni taasisi ya wasomi wenye viwango vya juu na wataalamu, la hasha! Yeyote anayejitambua kuwa ni Mswahili, na anaumwa na Kiswahili, hiki ni chama  chake, karibuni milango iko wazi,” alifafanua.
Profesa Kijiti Shaaban Sengo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria Tanzania aliyealikwa katika hafla hiyo, alikemea tabia ya baadhi ya watu kudakia maneno yanayotamkwa na watu wanaojiita wataalamu wa Kiswahili bila kujali murua wa maneno hayo mbele ya jamii ya Waswahili wenyewe.
Alisema ni wajibu wa Wswahili wa asili kuwasahihisha na kuwaongoza watu wanaokichafua Kiswahili kwa kudhani kwamba wanavyotamka au kuandika ni sawa.  
Profesa Sengo alisisitiza umuhimu wa kujiendeleza kielimu hata kufikia ngazi ya uzamivu na kuacha kutoa kisingizio cha umri mkubwa na majukumu ya kusomesha watoto.
Chama hicho kilianza harakati za kusajliwa kwake miaka minne iliyopita, na kufanikiwa kupata usajili huo mwishoni wa mwaka 2016.
IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI MAELEZO ZANZIBAR 11 MACHI 2017

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.