Habari za Punde

Chumvi ya Madini Joto Haitumiki Ipasavyo

Na Salmin Juma Pemba. 
WAKAAZI wa Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba wako hatarini kupata ugonjwa wa goita  pamoja na matatizo ya  kuzaa watoto wenye udumavu wa akili  na kuharibu mimba  kwa akinamama baada ya  kubainika  kuwa chumvi yenye madini joto haitumiki ipasavyo  katika Wilaya ahiyo.

Mkuu wa kitengo cha Lishe cha Wizara ya Afya Pemba Raya Mkoko amesema kuwa utafiti uliofanywa katika familia 2,685 ni  familia 345 sawa na asilimia kumi na tatu (13%)  ambazo zimebainika kuwa zinatumia chumvi zenye madini joto.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Ofisini kwake Wete , Raya amesema utafiti huo umefanywa na maafisa Lishe ambao walipita katika Skuli na kuwataka wanafunzi kila mmoja kuchukua chumvi wanayotumia nyumbani na kubainika familia 2,340 zinatumia chumvi isiyo na madini joto.

Raya Mkoko ameitaka jamii hususani ya Wilaya ya Micheweni  kuifanyia uchunguzi wa chumvi ambazo wananunua kwa kutumia njia asili kuiangalia ili kujiridhisha kama kuna madini joto kabla ya kuinunua na kutumia .

Afisa Mkaguzi wa bodi ya Chakula , Dawa na Vipodozi Pemba Juma Seif Khamis amesema bodi imejipanga kutumia sheria kwa mkulima  na  muuzaji ambaye atabainika kusambaza na kuuza chumvi isiyokuwa na madini joto .

Amesema awali bodi , kitengo cha Lishe pamoja na wazalishaji wa chumvi Pemba walikubaliana kuwa , kila upande uchukuwe hatua za utoaji wa elimu  kwa wananchi  huku  akisema hatua za kihseria zitachukuliwa kwa atakaye kaidi .

Hivyo amewataka wananchi kutoa taarifa kwa taasisi husika baada ya kubaini kwamba kuna chumvi inauzwa na ambayo haina madini joto ili muhusika aweze kuchukuliwa hatua kisheria ikiwa ni pamoja na kuiangamiza chumvi hiyo .

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.