STATE HOUSE
ZANZIBAR
OFFICE OF THE
PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 11.4.2017
UMOJA wa Mataifa (UN), umeahidi kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika
kuimarisha miradi yake ya maendeleo ikiwemo ile inayosimamiwa na Mashirika ya
Umoja huo.
Hayo yalielezwa na Mratibu Mkaazi wa
Umoja wa Mataifa nchini Tanzania ambaye pia, ni Mwakilishi Mkaazi wa Shrika la
Maendeleo la Umoja wa Mataifa UNDP Alvero Rodriguez akiwa amefuatana na viongozi
wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa wanaofanya kazi zao hapa Zanzibar ambao wapo
hapa nchini kwa mkutano maalum wa kila mwaka unaofanywa na Umoja huo.
Mapema akitoa maelezo yake Mratibu huyo
Mkaazi wa UN nchini Tanzania ambaye alifuatana na Wawakilishi Wakaazi wa
Mashirika ya UN wanaofanya kazi zao hapa Tanzania alitoa pongezi kwa Dk. Shein
kwa Serikali anayoiongoza kwa kusimamia vyema miradi ya maendeleo na kuahidi
kuendelea kuunga mkono juhudi hizo.
Rodriguez alisema kuwa UN inathamini sana
uhusiano na ushirikiano uliopo kati yake na Tanzania ikiwemo Zanzibar, hivyo
basi ni vyema hatua hizo zikaendelezwa kwa manufaa ya nchi na wananchi wake
wote.
Katika maelezo yake Rodriguez alieleza
kuwa UN imeamua kwa makusudi kuendelea kuunga mkono sekta za maendeleo zikiwemo
elimu, afya, kilimo, mazingira, athari za tabia nchi, kupambana na umasikini
pampja na unyanyasaji wa kijinsia kwa akina mama na watoto, changamoto ya ajira,
na nyenginezo.
Aidha, alisema kuwa UN iko tayari
kuendelea kuunga mkono seta hizo hasa ikizingatiwa kuwepo kwa madaliko makubwa
ya kiuchumi duniani hatua ambayo inatoa nafasi kwa Umoja huo kuongeza nguvu kwa
Mashirika yake kuendelea kusaidia nchi kama Tanzania ikiwemo Zanzibar.
Sambamba na hayo, kiongozi huyo wa UN
nchini Tanzania alieleza hatua zinazoendelea katika kuiunga mkono Zanzibar
katika hatua zake za Kukuza Uchumi na Kupambana na Umasikini na kutekeleza Dira
2020.
Nao ujumbe huo wa UN nchini Tanzania,
kupitia Mashirika yake yalitoa pongezi kwa Dk. Shein kutokana na uongozi wake
katika kuendeleza miradi ya maendeleo inayosimamiwa na mashirika hayo huku
wakiahidi kuendelea kumuunga mkono.
Nae Rais Dk. Ali Mohamed Shein kwa upande
wake alitoa pongezi kwa Umoja wa Mataifa kupitia mashirika yake kwa
mashirikiano makubwa inayoyatoa kwa Zanzibar na Tanzania kwa jumla.
Dk. Shein alitumia fursa hiyo kueleza
changamoto mbali mbali zilizopo katika sekta za maendeleo ikiwemo elimu, afya,
ajira, unyanyasaji wa wanawake na watoto, athari za tabia na mambo mengineyo.
Hata hivyo, Dk. Shein alitumia fursa hiyo
kuueleza ujumbe huo wa UN kuwa mbali ya changamoto hizo Zanzibar haikufunga
mikono na imekuwa ikichukua juhudi za makususdi katika kuhakikisha changamoto
hizo zinapatiwa ufumbuzi kwa mashirikiano ya Mashirika hayo ya Umoja wa
Mataifa.
Dk. Shein alisema kuwa hatua mbali mbali
zimekuwa zikichukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuhakikisha
sekta ya elimu kwa kuendelea na ujenzi wa skuli mpya za Msingi na Sekondari,
Vyuo Vikuu. Aidha, alieleza namna Serikali ilivyoelekeza nguvu katika kilimo
cha umwagiliaji maji.
Pia, alieleza juhudi zinazochukuliwa
katika kuimarisha sekta ya afya,mafanikio yaliopatikana katika kupambana na
Malaria, kupambana na unyanyasaji wa akina mama na watoto na kueleza mikakati
mipya iliyowekwa na Serikali katika kupambana na kadhia hiyo hivi sasa.
Aidha, Dk. Shein alieleza kuwa kuwepo kwa
Ofisi za pamoja za Umoja wa Mataifa hapa Zanzibar ‘One UN’ kumeweza kurahisisha
kwa kiasi kkkubwa ufanyaji kazi wa Mashirika hayo na kupelekea kufanya kazi kwa
ufanisi mkubwa zaidi.
Wakati huo huo, Dk. Shein alikutana na Mabalozi wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania waliokuja kumuaga Rais, ambapo akitoa nasaha na maelekezo kwa
Mabalozi hao, Dk. Shein alisema kuwa nchi zote wanazokwenda kufanya kazi
Mabalozi hao ni muhimu na kuwataka kutambua kuwa katika ufanyaji kazi wao wajue
kuwa Jamhuri ya Muungani wa Tanzania ina pande mbili.
Alieleza haja ya kuimarisha uchumi wa
kidiplomasia katika uwakilishi wao katika nchi watakazozifanyia kazi na
kusisitiza kuwa katika suala zima la uchumi hivi sasa Tanzania imeweka
kipaumbele sekta ya viwanda hivyo, ni vyema wakaitangaza ikiwa ni pamoja na
kuwashajiisha wawekezaji kuja kuekeza hasa katika sekta ya viwanda.
Pamoja na hayo, alieleza haja kwa
viongozi hao kuutangaza utalii wa Tanzania ambapo kwa upande wa Zanzibar na
Tanzania Bara sekta hiyo imeendelea kupewa kipaumbele kutokana na mchango wake
mkubwa wa uchumi na pato la Taifa kwa ujumla.
Aidha, alisisitiza haja ya kuyashajiisha
mashirika ya ndege kufanya safari zao hapa Tanzania yakiwemo mashirika ya ndege
ya India, Ujerumani, Algeria na nchi nyenginezo huku akitilia mkazo umuhimu wa kuwasaisia
wanafunzi ambao wanasoma katika nchi wanazoenda kuzifanyia kazi pale wanapokuwa
na matatizo yao.
Nao Mabalozi hao walimshukuru Dk. Shein
kwa nasaha na maelekezo yake na kuahidi kuyazingatia na kufanya kazi hasa suala
zima la uzalendo katika Muungano.
Miongoni mwa Mabalozi hao ni Balozi Omar
Yussuf Mzee anekwenda nchini Algeria, Balozi Abdalla Saleh Posi anenkwenda nchini
Ujerumani, Balozi Baraka Luvanda anaekwenda India, Balozi Sylivester Ambukile anaekwenda
nchini Afrika Kusini, Balozi Daudi Massima anekwenda nchini Israil na Balaozi
Sylivester Massele Mabumba anaekwenda Umoja wa Visiwa vya Comoro.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024
2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment