Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kulia) alipokuwa akisalimiana na mgeni wake Mwenyekiti wa Kampuni ya "Engineering Consultants Groups"-ECG Bw.Amr Hassan Allouba alipofika Ikulu Mjini Zanzibar leo na ujumbe wake.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kulia) alipokuwa akizungumza na mgeni wake Mwenyekiti wa Kampuni ya "Engineering Consultants Groups"-ECG Bw.Amr Hassan Allouba yaliyofanyika Ikulu Mjini Zanzibar leo
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kulia) alipokuwa akifuatana na Mwenyekiti wa Kampuni ya "Engineering Consultants Groups"-ECG Bw.Amr Hassan Allouba (katikati) baada ya mazungumzo yao yaliyofanyika Ikulu Mjini Zanzibar leo,(kushoto) Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Nchini Misri Balozi Mohamed Haji Hamza.
[Picha na Ikulu.]24/04/2017.
STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 24.04.2017

AZMA ya
Kampuni ya ‘Engineering Consultants Group’ kutoka Misri ya kushirikiana na
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika sekta ya ujenzi wa miji mipya ya
kisasa inayotumia teknolojia mpya katika kurahisisha maisha ya wakaazi wake ‘Smart
City’ itasaidia kufikia lengo la ujenzi wa miji hiyo inayokusudiwa kujengwa hapa
Zanzibar sambamba na kuimarisha sekta ya uwekezaji.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein Aliyasema hayo leo wakati alipokuwa na
mazungumzo na Mwenyekiti wa Kampuni ya ‘Engineering Consultants Group’ Mhandisi
Amr Hassan Allouba, Ikulu mjini Zanzibar.
Katika maelezo yake, Dk. Shein aliyasema kuwa katika kuimarisha utekelezaji wa Mipango
miji, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
imo katika jitihada za makusudi za kuhakikisha inashirikiana na Kampuni mbali
mbali za ndani na nje ya nchi katika ujenzi wa miji ya kisasa hapa Zanzibar.
Aidha, Dk. Shein alisema kuwa azma ya Serikali ni
kuufanya Mji wa Zanzibar kupiga hatua kubwa zaidi za kimaendeleo katika maamuzi ya ziada ya kufanya kitovu cha
Mji (Ngambo) kuwa ni ‘Smart City’ ambayo ni nadharia mpya yenye lengo la
kufanya miji iwe sio tu mizuri ya kileo na endelevu bali hutumia utaalamu na
teknolojia mpya.
Dk. Shein alisema kuwa kujitokeza kwa Kampuni hiyo
na kuonesha azma ya kutaka kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
katika sekta hiyo ni jambo la faraja hali ambayo inatoa nafasi kwa Zanzibar
kuzidi kujiwekea mazingira mazuri katika utekelezaji wa azma hiyo sambamba na
kujipanga vyema kiuwekezaji.
Rais Dk. Shein alimueleza Mwenyekiti huyo wa
Kampuni ya ECG yenye Makao Makuu yake mjini Cairo, Misri kuwa tayari Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar imeshatenga maeneo huru ya uwekezaji Fumba kwa upande
wa Unguja na Micheweni kwa upande wa Pemba na katika maeneo yote hayo Serikali
inaendelea kutoa fursa kwa wawekezaji kuekeza katika sekta mbali mbali za
maendeleo.
Aliongeza kuwa Zanzibar iko tayari kushirikiana na
Kampuni hiyo kwani itapata mengi ya kujifunza kutokana na uzoefu mkubwa ulionao
na kusisitiza kuwa ujenzi wa miji mipya
ya kisasa inahitajika hasa ikizingatiwa kuwa maendeleo na teknolojia yamezidi
kuimarika duniani kote ambapo kampuni hiyo nayo iko katika hatua hiyo.
Aidha, Dk. Shein alimueleza Mwenyekiti huyo alieongozana
na kiongozi wa Kampuni hiyo kwa upande wa
nchi za Bara la Afrika Sherif Mourad wakiwa na Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania nchini Misri, Balozi Mohammed Hamza kuwa Zanzibar ina uhusiano na
ushirikiano mwema na wakihistoria kati yake na Misri.
Aliongeza kuwa Misri ni miongoni mwa nchi za
mwanzo zilizoanzisha uhusiano wa kidiplomasia kati yake na Zanzibar mara tu
baada ya Mapinduzi Matkukufu ya Januari 12, 1964 hatua ambayo ilipelekea
mashirikiano mazuri yaliopelekea kukuza uhusiano na ushirikiana katika sekta ya
elimu, afya na nyenginezo.
Sambamba na hayo, Dk. Shein alieleza kuwa wanafunzi
walio wengi wa Zanzibar walipata fursa ya kusoma nchini Misri hasa katika Chuo
Kikuu cha Al-Azhar na vyuo vyenginevyo na wengine kupata fursa ya kusomea
udaktari na fani nyengine zikiwemo za elimu ya dini ya Kiislamu, habari na
nyenginezo.
Nae Mwenyekiti wa Kampuni ya ‘Engineering
Consultants Group’ Mhandisi Amr Hassan Allouba alimueleza Dk. Shein azma ya
Kampuni hiyo kushirikiana na Zanzibar katika kuimarisha miji mipya ya kisasa
ambayo inaendana na teknolojia ya kisasa ambayo itaiwezesha Zanzibar kuimarika
kiuchumi, kibiashara na utoaji huduma
kwa jamii.
Mhandisi Allouba alimuelezea Dk. Shein uzoefu wa
kazi za Kampuni hiyo ndani na nje ya Misri pamoja na mafanikio iliyoyapata na
kueleza kuwa Kamupuni yake iko tayari kuleta neema hiyo kwa Zanzibar ili
kuwasaidia wananchi pamoja na Serikali yao katika kukuza uchumi wake na
kuimarisha maendeleo.
Alieleza kuwa miradi hiyo kwa uzoefu wake imekuwa
ni kichocheo kikubwa cha ajira hali ambayo imepelekea kuimarika kwa soko la
ajira katika maeneo yote ambayo tayari wameshaitekeleza.
Alisema kuwa mbali ya kuimarika kwa ajira pia,
hatua hiyo itasaidia katika kuifanya Zanzibar iimarike na iwe mbele katika
sekta ya teknolojia ya kisasa kutokana na uzoefu walionao katika miradi hiyo.
Hivyo, Mwenyekiti huyo amemuhakikishia Dk. Shein
kuwa Kampuni yake iko tayari kuimarisha uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya
Misri na Zanzibar kwa kuja kuekeza Zanzibar kwani ni pande mbili zenye uhusiano
na udugu wa kihistoria, hivyo hatua hiyo itapanua wigo wa maendeleo kwa
Zanzibar.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address:
2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment