KAMISHNA wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) ofisi ya Zanzibar, Mhe. Khatibu Mwinyichande amewataka watumishi wa tume hiyo kufanya kazi kwa weledi na kuzingatia maadili ya kazi zao kwa mujibu wa taratibu, kanuni na Sheria za Utumishi wa Umma.
Kamishna Mwinyichande ametoa rai hiyo wakati alipozungumza na watumishi 10 waliohamia ofisini hapo kutoka taasisi mbalimbali za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) katika ofisi za THBUB Zanzibar leo Julai 11, 2025 ikiwa ni hatua za kuwakaribisha rasmi kwenye tume hiyo.
Akizungumza kuhusu kufanya kazi na THBUB Mhe. Mwinyichande amewataka watumishi hao kufanya kazi kwa kuzingatia misingi mikuu inayoiongoza tume hiyo ambayo ni kuheshimu haki za binadamu na misingi ya utawala bora.
“Kila mmoja ajue anafanya kazi kwa mujibu wa miongozo na maadili ya Tume, kazi za tume ni za kushirikiana ukiachia za kila mtu na kada ya utaalamu wake, ni vyema nyote mkaijua tume kwa undani wake ili iwe wepesi kwenu kuijua na kuinakili misingi ya kazi za tume muelewe haki inaanzia wapi na muweze kuifanyia kazi kwa kufuata misingi ya utawala bora.” alilisitiza Mhe. MwinyiChande.
Katika hatua nyingine, Mhe. Mwinyichande amewasisitiza watumishi hao kufanya kazi kwa timu ya kushirikiana ili kujijengea ufanisi na weledi wa kazi za tume sambamba na kuwanasisihi kuachana na mazoea waliyotoka nayo sehemu walizowahi kufanyia kazi hasa mazoea yenye kupotosha bali waboreshe na kujenga ustawi wa jamii iliyo bora kwenye maeneo yao ya kazi.
Akizungumzia eneo la utawala bora, Kamishna Mwinyichande pia amewasisitiza watumishi hao kulifanyia kazi kwa uweledi na ufanisi wa hali ya juu ili kuhakikisha haki inatekelezwa kwa kila aliyevunjiwa.
Naye, Katibu Msaidizi wa THBUB, Juma Msafiri Karibona amewataka watumishi hao kufanya kazi kwa kuzingatia maadili a sheria ya Tume na kuwa na ushirikiano baina ya wafanyakazi wapya, waliohamia na wa zamani ili kujenga jamii iliyokusudiwa.
Nao watumishi hao waliohamia kutoka kwenye taasisi za SMZ, wameahidi kufanya kazi kwa weledi, ufanisi na ushirikiano ili kufanikisha malengo ya Tume.
No comments:
Post a Comment