STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 29.04.2017
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Ali Mohamed Shein amewataka vijana wa Jimbo la Uzini kuimarisha michezo kwa
lengo la kuwaunganisha na kujenga udugu na umoja miongoni mwao na viongozi wao
wa chama na Serikali wataendelea kuwaunga mkono.
Dk. Shein aliyasema
hayo leo huko katika ukumbi wa Skuli ya Dunga, Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini
Unguja, katika hafla ya kukabidhi vifaa
vya michezo kwa timu 46 za Jimbo la Uzini Mohammed Raza vilivyotolewa na Mwakilishi
wa Jimbo hilo ambayo ilihudhuriwa na viongozi mbali mbali wa chama na Serikali
akiwemo Makamo wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd.
Katika maelezo yake,
Dk. Shein alisema kuwa michezo ndio inayowanganisha vijana na hata wazee na
kuwa kitu kimoja na kuwasisitiza waendelee kucheza michezo mbali mbali hasa
ikizingatiwa kuwa michezo inahistoria kubwa katika kuwanganisha watu kwani ndio
iliyowaunganisha Watanzania kupitia vyama vya siasa kikiwemo ASP, TANU na
hatimae CCM.
Aidha, Dk. Shein alitumia
fursa hiyo kueleza historia ya michezo hapa Zanzibar huku akiwataka vijana kuanza michezo tokea wakiwa skuli kwani michezo ina
nafasi kubwa katika elimu na elimu huenda sambamba na michezo.
Dk. Shein alieleza
kuwa katika maisha ya mwanaadamu yoyote michezo ina umuhimu, mkubwa kwani huleta mshikamano hujenga udugu
na kujuana na pia, husaidia katika kujenga afya ya akili na kiwiliwili kwa
vijana na wazee na watambue kuwa michezo si uhasama.
Sambamba na hayo, Dk.
Shein alisisitiza umuhimu wa michezo kufuata kanuni na taratibu za kucheza na
kuwataka vijana hao kushindana kimichezo na wasijenge uhasama na kupelekea
kupambana kwani hilo sio lengo la michezo.
Pamoja na hayo, Dk.
Shein aliwataka vijana hao wa Jimbo la Uzini kuwa wazalendo wa nchi yao, Jimbo
lao, wazee wao, viongozi wao huku wakitambua kuwa Serikali yao ya Mapinduzi ya
Zanzibar imefanya mambo mengi ya kimaendeleo ambayo wanapaswa kuyaunga mkono.
Akisisitiza haja ya
vijana kuwa wazalendo, Dk. Shein alisema kuwa suala la uzalendo limepungua kwa
kiasi kikubwa hapa nchini hivi sasa na kueleza haja ya kuitumia michezo kwani
michezo ni uzalendo na kuwataka kuwa wazalendo wa timu zao za nyumbani huku
akiwasisitiza kufuata msemo wa Rais wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi Marehemu
Mzee Abeid Amani Karume kuwa “Thamini chako na usahau cha mwenzako’.
Akiwaeleza juu ya ombi
lao la kutengenezewa barabara zao za ndani katika Jimbo hilo, Dk. Shein alisema
kuwa azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuzitengeneza barabara hizo
iko pale pale na kuwaeleza jambo linalochelewesha azma hiyo ni uhaba wa vifaa
ambapo tayari serikali ina mpango wa kununua vifaa zaidi vya kutengenezea
barabara ukiwemo mtambo mpya wa kupikia lami.
Nae Mwakilishi wa Jimbo
la Uzini Mohammed Raza alieleza kuwa mashirikiano ya pamoja kati yake na
viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na viongozi wa Serikali wa Wilaya na Mkoa
ndio yaliopelekea kupata mafanikio hayo.
Aliongeza kuwa yote
anayoyafanya kwa Jimbo hilo akiwa ni Mwakilishi wa wananchi wa Jimbo hilo la
Uzini ni utekelezaji wa Ilani ya
Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010-2020 ambayo inasisitiza uimarishaji wa sekta ya
michezo.
Alieleza kuwa kufanya
hivyo ni njia moja wapo ya kuwapa wananchi haki yao ya kuwachagua viongozi
ambao huwatumikia katika vyombo vya kutunga sheria sambamba na kuwa na majibu
rahisi mbele ya wananchi wakati ukifika wa kuwaomba ridhaa yao ili wakuchague.
Pamoja na hayo, Raza
aliwaahidi wanachi wa Jimbo la Uzini wakiwemo vijana kuwa ataendelea
kuwatumikia na kusisitiza mashirikiano ya pamoja ambayo ndio ngao kubwa ya maendeleo
Jimboni humo huku akiwataka kuendeleza michezo kwa amani na ushirikiano.
Mbali ya mafanikio
makubwa yaliopatikana katika Jimbo hilo la Uzini Mwakilishi huyo alieleza
changamoto ya miundombinu ya barabara za ndani zilizomo katika Jimbo hilo
zikiwemo zile zenye kiwango cha kifusi
Nao wananchi wa Jimbo
la Uzini katika risala yao iliyosomwa na Hamad Ali Haji, walimpongeza Dk. Shein
kwa kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa vitendo na kuahidi kuendelea
kumuunga mkono.
Walimuhakikishia kuwa
wataendelea kudumisha amani na utulivu na kuuunga mkono uongozi wake pamoja na
chama chao cha CCM ambapo pia walitumia fursa hiyo kuyaeleza mambo mbali mbali
ya maendeleo waliyofanyiwa na Mwakilishi wao huyo tokea walipompa ridhaa ya
kuwaongoza katika jimbo lao hilo la
Uzini.
Miongoni mwa vifaa
vilivyotolewa katika hafla hiyo ni pamoja jezi, mipira, viatu, soksi na
shinguard ambavyo vyote vina thamani ya Tsh. Milioni 25.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment