Habari za Punde

Kongamano la Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani Mei 3,2017.

HOTUBA YA MGENI RASMI MHE. BALOZI SEIF ALI IDDI, MAKAMU WA PILI WA RAIS WA ZANZIBAR ALIYOITOA KATIKA MAADHIMISHO YA SIKU YA UHURU WA HABARI DUNIANI HAPO UKUMBI WA CHUO CHA UANDISHI WA HABARI TAREHE 3 MEI, 2017 ZANZIBAR

Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Zanzibar,
Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania,
Mkuu wa Chuo cha Uandishi wa Habari Zanzibar,
Mkurugenzi wa TAMWA Zanzibar,
Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Zanzibar,
Jamii ya Wanahabari na wadau wote wa habari,
Mabibi na Mabwana.

Asalam Alaikum,
Awali ya yote, naomba tumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia kukusanyika katika shughuli hii tukiwa wazima kwa lengo la kuadhimisha siku ya uhuru wa habari duniani.
Aidha, napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa waandaaji wa shughuli hii kwa kunitunuku kuwa Mgeni Rasmi.  Kama mjuavyo siku ya habari ni siku muhimu duniani kote ambayo imetangazwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 1993 na kuamuliwa kuadhimishwa kote duniani siku ya leo tarehe 3 Mei.

Ndugu Wananchi, Ndugu Wanahabari,
Kwa mnasaba huo, Wanachama wote wa Umoja wa Mataifa ikiwemo Tanzania tunalo jukumu la kuiadhimisha siku hii pamoja na kuzingatia kwa makini ujumbe unaoambatana na siku hii.  Kwa mwaka huu ujumbe huu unasomeka kwa kiingereza

 “Critical minds for critical times: the media’s role in advancing peaceful, just and inclusive societies”. Kwa tafsiri isiyokuwa rasmi ujumbe huu unasema umakini wa fikra kwa wakati muhimu: “nafasi ya vyombo vya habari katika kuimarisha jamii yenye amani, haki na ujumuishwaji”.

Kwa kifupi Ndugu Wananchi na Wana Habari, ujumbe huu umetoa majukumu mazito kwa kada ya habari ambayo inatakiwa kuimarisha amani, haki na usawa kwa wanajamii wote bila ya kuwabagua ili kila mwanajamii apate haki ya kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.

Ndugu Wananchi,
Vyombo vya habari ni mhimili unaoweza kuwaunganisha wanajamii au kuwatenganisha.  Yote haya yanategemea matumizi ya vyombo hivi. Vikitumiwa vibaya vitatoa matokeo mabaya na vikitumiwa vizuri vitatoa matokeo mazuri ya maendeleo.

Ndugu Wanahabari,
Wakati tunaadhimisha siku hii ya uhuru wa habari kuna mambo manne muhimu kuyakumbuka na kuyazingatia.  Jambo la kwanza, siku ya leo tunasherehekea kuwepo kwa misingi ya uhuru wa vyombo vya habari.  Jambo la pili tunatakiwa kutathmini uhuru huu wa vyombo vya habari duniani kote. 

Jambo la tatu uhuru wa vyombo vya habari unatakiwa kulindwa ili ubakie kuendelea, na Jambo la nne tunatakiwa siku ya leo kuwakumbuka Waandishi wa Habari waliopoteza maisha yao wakati wakitekeleza haki yao ya msingi ya uhuru wa habari.

Ndugu Wanahabari,
Leo ni siku yenu Wanahabari. Naamini mambo haya manne mtayazungumza kwa kirefu. Mimi nikiwa mwanasiasa nitazungumzia mawili au matatu katika hayo.

Napenda kuanza kulizungumzia jambo la tatu la kuulinda uhuru wa vyombo vya habari. Nawatoa wasiwasi Ndugu Wanahabari kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuulinda uhuru wa vyombo vya habari na kama zipo sheria zinazokwamisha uhuru huo Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo itazirekebisha. Lengo letu ni kupanua zaidi uhuru wa vyombo vya habari na sio kuuminya uhuru huo, mradi uhuru huo wa habari hautotumiwa vibaya.

Tunaelewa wazi kuwa uhuru wa vyombo vya habari ndio njia pekee itakayo tuhakikishia kutekelezeka kwa dhana ya utawala bora ambayo miongoni mwa misingi yake ni demokrasia, uwajibikaji, utawala wa sheria, na uwazi.  Uhuru wa vyombo vya habari husaidia kujenga utamaduni wa kuheshimu utawala wa sheria katika nchi na wale watakaokwenda kinyume na kujiweka juu ya sheria (above the law) ikiwa viongozi au wananchi wa kawaida, vyombo vya habari vilivyo huru havitosita kuibua udhaifu huo uliojitokeza.

Bila shaka vyombo vya habari vilivyo huru ndivyo vitakavyoweza kufichua maovu katika jamii kama rushwa, kuwafichuwa wanaojishughulisha na biashara ya madawa ya kulevya, watu wanaoendeleza ukatili dhidi ya wanawake, na viongozi wanaotumia madaraka vibaya Serikalini.  Kwa hivyo Serikali haina sababu kuogopa kuwepo kwa uhuru wa habari nchini kwani uhuru huo ukitumiwa vizuri faida yake ni kubwa mno.

Ndugu Wanahabari,
Siku ya uhuru wa habari inatukumbusha sisi viongozi umuhimu wa kuheshimu uhuru huu kwa faida ya maendeleo ya Taifa letu.  Siku hii pia inawataka nyinyi wanataaluma wa habari na wanahabari kwa jumla kujitathmini kama kweli mnatumia haki yenu hii kwa kufuata maadili ya kazi yenu.

Haja ya vyombo vya habari kujitathmini hivi sasa ni kubwa zaidi pengine kuliko wakati wowote katika historia ya uhuru wa vyombo vya habari. Vyombo vya habari hivi sasa duniani vinapitia katika kipindi kigumu cha kutokuaminiwa na wananchi.  Mifano ifuatayo ya vichwa vya habari vinavyoelezea kutokuaminiwa vyombo vya habari inatisha. 

India media 2nd most untrusted institution (vyombo vya habari ni taasisi ya pili kwa kutokuaminika sana nchini India). Kichwa chengine cha habari kinasema “Americans’ trust in Mass Media sinks  to new low” (kuamini vyombo vya habari kwa Wamarekani kumeshuka kwa kiwango cha chini).

Nyote ni mashahidi ni vyombo vikubwa vya habari duniani vilivyochangia kuupotosha umma duniani kuamini kuwa Iraq ilikuwa na silaha za maangamizi na hatimaye kupelekea kuondolewa kwa nguvu Rais Saddam Hussein na Mataifa makubwa.  Tangu kuondolewa kwa utawala wa Saddam Hussein Iraq bado ipo katika dimbwi la migogoro na machafuko ya kisiasa ambayo tangu kuanza kwake maelfu ya wananchi wameshapoteza maisha. Baya zaidi machafuko hayo hadi leo hayajapatiwa ufumbuzi wa kudumu.

Dhana ya ‘fake news’ yaani ‘habari feki’ aliyokuja nayo Kiongozi mmoja (Rais wa Marekani Donald Trump) hivi karibuni ni dhana inayoitafuna kada ya uandishi wa habari na kupelekea watu kutilia mashaka habari zinazotolewa na vyombo vya habari.  Inawezekana Kiongozi huyo anatumia dhana hii kwa faida zake binafsi za kisiasa. Hata hivyo inaonekana watu wa kawaida wanaanza kuamini vyombo vya habari vingi vinatoa habari feki.

Hivi karibuni chombo chetu cha habari cha Taifa TBC kimeripoti habari feki kwa kutangaza kuwa Rais wa Marekani Donald Trump amempongeza Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli kwa uchapaji wake wa kazi. Habari hii imepelekea uongozi wa TBC kuwasimamisha kazi waandishi wa habari waliohusika kwani habari walizozitowa zilikuwa feki.

Wakati mwengine wafanyabiashara au watu wenye uwezo wa kifedha wanapotaka kujitumbukiza kwenye siasa hununua vyombo vya habari kwa ajili ya kusambaza habari feki ambazo huwajenga au kuwabomoa wapinzani wao.  Nyote ni mashahidi uchaguzi mkuu unapokaribia hujitokeza wanasiasa kuanzisha vyombo vya habari au kuvinunua baadhi ya vyombo vya habari kwa ajili ya kusambaza habari feki.

Ndugu wanahabari,
Kwa mujibu wa taarifa mbali mbali kutokuaminika kwa vyombo vya habari na wananchi kwa mambo yanayoripotiwa kunaongezeka duniani ikiwemo Marekani na nchi za Magharibi zinazojivunia kuwa na vyombo vya habari makini na mahiri.

Kwa hivyo, natoa changamoto kwa waandishi wa habari nchini kulizungumzia kwa kina jambo hili la kuongezeka kwa idadi ya watu  kutokuviamini vyombo vya habari kwa kuamini  vinatoa habari feki.  Lakini kulizungumza tu jambo hili haitoshi, ni vyema  kulitafutia ufumbuzi wake kwani mimi mwenyewe naamini mchango wa vyombo vya habari kwa maendeleo ya nchi hauna mfano wake.

Wakati mtakapokaa chini kutafakari hali hii napenda mzingatie maneno aliyoyanena mwandishi wa habari mkongwe wa gazeti la New York Times la Marekani Bwana Jim Rutenberg pale aliposema:

 “It will be great journalism that saves Journalism”.  Kwa tafsiri isiyo rasmi‘Uandishi wa habari makini ndio unaookoa uandishi wa habari’.

Uandishi wa habari makini ni ule unaofuata maadili, unaotumia utafiti wa kutosha kabla kuchapisha habari na pale makosa yanapotokea kwa bahati mbaya yanarekebishwa mara moja.

Uandishi wa habari makini hujitenga na propaganda, hujitenga na ushabiki wa kisiasa au wa mtu. Uandishi wa habari makini hujitenga na upendeleo na siku zote husimamia ukweli mtupu. Naamini pale mtakaporejea kwenye misingi yenu ya kazi imani ya walimwengu kwa vyombo vya habari itarejea kama zamani.  Maafa ya kuporomoka kwa uandishi wa habari kwa kutokuaminiwa na jamii kubwa ni janga kubwa kwa jamii pengine kuliko maafa yanayoweza kuletwa na mama wa mabomu yote (mother of all bombs).

Ndugu Wanahabari,
Hivi karibuni Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein amewataka Mawaziri na wasaidizi wao kuachana na tabia ya kukwepa waandishi wa habari. Jambo hili nitalisimamia ili kurahisisha utendaji wenu wa kazi.

Naamini wananchi wanayo haki kuelewa Serikali yao inafanya nini na kwa sababu gani.  Kazi hii ya kuwapasha habari wananchi juu ya mambo mbali mbali yanayo endelea Serikalini mwao ni jukumu lenu la msingi.  Wafuateni Mawaziri wakupeni habari hizo, au hata mnifuate mimi wenyewe.  Msiandike mambo bila ya kuwa na uhakika navyo.

Baada ya kusema hayo naomba kuwashukuru tena wale wote waliochangia kwa njia moja au nyengine kufanikisha shughuli hii. Nawatakia kazi njema na mafanikio katika kuadhimisha siku hii.
Ahsanteni kwa kunisikiliza.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.