STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 16.05.2017
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amewafariji na kuwapa pole wananchi waliopata
athari baada ya nyumba zao kuezuka mapaa kufuatia upepo mkali uliotokea hapo jana
mnamo majira ya saa tatu asubuhi na kuathiri nyumba zipatazo 123.
Upepo huo, ulitokea
katika maeneo ya Nyarugusu, Pangawe, Kinuni, Makondeko na Shehia ya Mwanakwerekwe na kupelekea nyumba kadhaa
kuezeka mapaa.
Akiwa katika eneo hilo
mara baada ya kukagua baadhi ya nyumba zilizopata athari, Rais Dk. Shein
aliwaeleza wananchi hao kuwa Serikali yao ipo na itachukua kila jitihada katika
kuhakikisha inawapa msaada unaostahiki haraka iwezekanavyo.
Dk. Shein aliwapa pole
wananchi hao na kuwapongeza kwa ushirikiano wao mkubwa waliouonesha katika
kipindi hichi na kueleza kuvutiwa kwake na juhudi zao hizo.
Alisema kuwa yeye
mwenyewe binafsi baada ya kupata taarifa hiyo akiwa huko kisiwani Pemba hapo
jana ambako alikwenda kuwafariji wananchi waliopata athari za mvua za masika
zinazoendelea kunyesha ambazo zimeharibu makaazi ya watu, miundombinu ya
barabara, madaraja na mazao kiswani humo, alipatwa na simanzi na majonzi
makubwa sana.
Alisisitiza kuwa hiyo yote
ni shani yake Mwenyezi Mungu, na mtukuio kama hayo si mara ya kwanza kutokea na
yanapotokea huwa hayana taarifa ambapo aliwahimiza wananchi kusaidiana, kustiriana
na wale wote wenye uwezo wawasaidia wasio na uwezo huku akieleza kuwa Serikali
kwa upande wake ina jukumu la msingi la kuwatendelea mema wananchi wake.
Dk. Shein aliwataka
wananchi kutolaumiana kwani hakuna mtu aliyoyatenda na kuwataka wananchi
kutowabeza waliopatwa na athari hiyo kwani janga hilo linaweza kumpata mtu
yeyote na wakati wowote.
Aidha, Alieleza kuwa
mipango ya Serikali ni mizuri lakini inazidiwa kimo na mipango ya Mwenyezi
Mungu, hivyo aliwasisitiza wananchi kusaidiana na kuahudi kuwa Serikali kwa
upande wake itaongeza nguvu kwani ipo na iko imara na haitochelea kutoa misaada
na itawasaidia wale wote waliokuwa hawana uwezo.
Mapema wananchi
walioathirika na upepo huo katika maeneo ya Pangawe na Makondeko walimueleza Dk.
Shein jinsi upepo huo mkali ulivyoanza na hatimae kuleta athari kubwa katika
eneo hilo na namna walivyokabiliana nao huku wakitoa pongeza kwa Dk. Shein kwa
kuwajali na kuwathamini kutokana na kitendo chake hicho cha kwenda kuwafariji
na kuwapa pole.
Dk. Shein alitumia fursa
hiyo kuwapongeza viongozi wa Mkoa, Wilaya, Jimbo, Manispaa na wengineo kwa
hatua madhubuti walizozichukua katika kukabiliana na tukio hilo ambalo
limeathiri nyumba za wananchi.
Akizungumza na waandishi
wa habari Dk. Shein alisisitiza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaandaa
utaratibu maalum wa kuhakikisha kila mwenye uwezo akiwa ndani ama nje ya nchi
anaweza kuchangia katika maafa yaliyosababishwa na mvua hizi za masika
zinazoendelea kwani Serikali haiwezi kufanya mambo yote peke yake.
Alieleza haja ya kuwepo
maandalizi katika kukabiliana na matukio kama hayo na kuahidi kwa upande wa
Serikali itajiandaa lakini pia aliwataka wananchi nao wajiande kwa kuepuka
kufanya vitendo ambavyo vitapelekea kuzidisha athari za mvua zikiwemo ujenzi
usio salama.
Mkuu wa Mkoa wa Mjini
Magharibi Ayoub Mohammed pamoja na Uongozi wa Manispaa Wilaya ya Magharibi B, walimueleza Dk. Shein
hatua za awali zilizochukuliwa ikiwa ni pamoja na kuwapatia chakula wananchi
hao walioathirika kwa kila nyumba kupewa kipolo cha mchele wa kilo 25 huku
juhudi zikifanywa kufuatia Kamati maalum kuundwa ambayo inafanya kazi na
kuahidi kutoa taarifa ndani ya masaa 24.
Mkuu wa Mkoa huyo
alieleza kuwa nyumba zilizoathirika idadi yake ni 123 ambapo 96 ni za Shehia ya
Kinuni, 26 Shehia ya Mwanakwerekwe na nyumba moja ni ya Shehia ya Pangawe.
Nae Mbunge wa Jimbo la
Pangawe Shamsi Vuai Nahodha kwa niaba ya wananchi wa Jimbo hilo na Majimbo ya
jirani yaliyoathirika walieleza kufarajika kwao kwa ziara hiyo ya Dk. Shein ya
kwenda kuwaona na kuwapa pole.
Alieleza kuwa kutokana
na wananchi hao kupita katika kipindi kigumu sana katika msimu huu wa mvua za
masika, Mbunge huyo alisema kuwa
Serikali imeonesha juhudi kubwa katika kuwasaidia wananchi ambapo viongozi wa
siasa nao kwa upande wao wamekuwa wakiwaunga mkono na kuwafariji pamoja na
kuwasaidia huku akisifu moyo waliouonesha wananchi hao katika kipindi hichi na
kuwataka waendelee nao.
Akitoa neno la shukurani
kwa Rais, Mwakilishi wa Jimbo la Pangawe ambaye pia, ni Naibu Waziri, Wizara ya
Nchi Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Khamis
Juma Maalim alisema kuwa ujio wa viongozi wa Serikali akiwemo Rais wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein umewapa faraja kubwa
wananchi wa maeneo hayo ambao wameathirika na upepo huo.
Rajab Mkasaba,
Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment