Habari za Punde

Rais Dk Shein afanya uteuzi wa viongozi


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, leo amefanya uteuzi wa viongozi katika taasisi mbalimbali za serikali.

Katika uteuzi huo, dk. shein amemteua SACP Haji Hamdun Omar kuwa Naibu Kamishna wa Chuo cha Mafunzo, na Luteni Kanali Mussa Mohammed Shaame kuwa Mkuu wa Utawala katika Jeshi la Kujenga Uchumi, JKU.

Rais Dk. Shein pia amemteua Abdi Omar Maalim kuwa Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi ya shirika la meli na uwakala, huku Hassan Abdalla Rashid akiteuliwa kuwa Katibu Tawala wa wilaya ya Micheweni.

Katika Idara ya Habari Maelezo, iliyo chini ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, Dk. Juma Mohammed Salum ameteuliwa kuwa Naibu Mkurugenzi.

Taarifa ya ofisi ya rais iliyosainiwa na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee, imesema pia Miza Hassan Faki ameteuliwa kuwa Katibu Tawala wilaya ya Mkoani.

Aidha Kanali Ali Hassan Hamad, anakuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa taasisi ya utafiti wa mifugo katika Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi.

Uteuzi wote huo umeanza leo tarehe 19 Juni, 2017.
       
IMETOLEWA NA OFISI YA RAIS IKULU KUPITIA IDARA YA HABARI MAELEZO ZANZIBAR
19 JUNI 2017.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.