STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 2.06.2017
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameeleza azma ya Zanzibar kukuza na kuimarisha
uhusiano kati yake na Morocco hasa katika masuala ya kiuchumi, kijamii na
kiutamaduni kwa faida ya nchi mbili hizo pamoja na watu wake.
Dk. Shein aliyasema hayo
leo katika mazungumzo kati yake na Balozi wa Ufalme wa Morocco katika Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Abdelilah Benryane, mazungumzo yaliofanyika Ikulu
mjini Zanzibar.
Katika mazungumzo hayo, Dk.
Shein alimuhakikishia Balozi Benryane kuwa Zanzibar itaimarisha zaidi uhusiano
na ushirikiano kati yake na Morocco huku akieleza kuwa Zanzibar ina mambo mengi
ya kujifunza kutoka nchini humo.
Dk. Shein alisema kuwa ziara
ya kiongozi wa nchi hiyo Mfalme Mohammed VI aliyoifanya hapa nchini mnamo mwezi
Oktoba mwaka jana imeonesha dalili za uhusiano na ushirikiano mwema kati ya
Tanzania na Morocco.
Aliongeza kuwa katika
ziara hiyo muhimu ambapo Tanzania ilisaini makubaliano takriban 24 ya
ushirikiano kati yake na Morocco katika sekta mbali mbali za maendeleo ikiwemo
kilimo, gesi, mafuta, utalii na nyenginezo.
Dk. Shein alimueleza
Balozi huyo kuwa kutokana na Zanzibar kuwa ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, makubaliano hayo pia, yataifaidisha Zanzibar kwa upande wake na
kusisitiza kuwa kutokana na hatua hiyo kuna umuhimu mkubwa wa kuzidisha
mashirikiano ili makubaliano hayo yaweze kwenda vizuri zaidi.
Aidha, Dk. Shein
alimueleza kiongozi huyo juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
katika kuimarisha sekta ya utalii na kusisitiza haja ya kuwepo kwa mashirikiano
hasa ikizingatiwa Morocco ni miongoni mwa nchi za Bara la Afrika iliyopiga
hatua kubwa katika sekta ya utalii.
Pamoja na hayo, Dk.
Shein alimueleza Balozi huyo umhimu wa kushirikiana katika sekta nyenginezo
ambazo nchi hiyo imepiga hatua ikiwa ni pamoja na sekta ya afya, elimu na
utamaduni huku akimueleza haja kwa pande mbili hizo kuanzisha proramu za
wanafunzi kutembeleana kimasomo kwa ajili ya kujenga utaalamu na uzoefu.
Sambamba na hayo, Dk.
Shein alitumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji wa Morocco kuja kuekeza
Zanzibar katika sekta mbali mbali ikiwemo sekta ya uvuvi hasa wa bahari kuu na
kumueleza balozi huyo wa Morocco haja ya kuitangaza Zanzibar nchini mwake
kiutalii.
Aliongeza kuwa Zanzibar
ina sifa zote za uwekezaji hasa katika sekta hiyo ya uvuvi hasa ikizingatiwa
kuwa ni nchi ya visiwa vilivyozungukwa na bahari ambayo ina samaki wengi ambao
ni maarufu na wanaopendwa duniani wakiwemo samaki aina ya jodari.
Nae Balozi wa Ufalme wa Morocco
katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Abdelilah Benryane alimueleza Dk. Shein
kuwa Morocco inajivunia uhusiano na ushirikiano mwema uliopo kati yake na
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo Zanzibar.
Balozi Benryane alisema
kuwa Morocco iko tayari kushirikiana na Zanzibar katika kuendeleza miradi mbali
mbali ya maendeleo na kumuhakikishia Rais Dk. Shein kuwa nchi yake itatoa
nafasi za masomo katika kada mbali mbali kwa wanafunzi wa elimu ya juu wa
Zanzibar ikiwa ni pamoja na nafasi za masomo ya elimu ya dini.
Aidha, alieleza haja ya
kuwepo mashirikiano ya kubadilishana uzoefu na utaalamu kwa wanafunzi wa
Zanzibar na wale wa nchi yake kutokana na nchi hiyo kuwa na vyuo vingi
vinavyotoa mafunzo kadhaa.
Pamoja na hayo, Balozi
huyo alimuhakikishia Dk. Shein kuwa juhudi za makusudi atazichukua katika
kuhakikisha anajenga mashirikiano mazuri nchini mwake kwa kuendeleza uhusiano
na ushirikiano na Zanzibar katika sekta muhimu za maendeleo zikiwemo elimu,
afya, kilimo, uvuvi, utalii na nyenginezo
Akizungumzia juu ya
sekta ya utalii, Balozi huyo alisema kuwa nchi yake imepiga hatua kubwa katika
sekta hiyo ambapo hivi sasa inapokea watalii milioni 16 kwa mwaka kufuatia
program ijulikanayo ‘Azur Blue’ iliyoanzishwa na kiongozi wa nchi hiyo Mfalme
Momamed VI ambapo pia, katika programu ya pili wamejiwekea hadi kufikia mwaka
2020 watapokea watalii wapatao milioni 20.
Hivyo, alieleza kuwa
nchi yake itakuza uhusiano na Zanzibar katika kuimarisha sekta hiyo hasa
ikizingatiwa kuwa nchini mwake kuna miundombinu mingi ya kuimarisha sekta hiyo
vikiwemo vyuo vya mafunzo ya kitalii.
Wakati huo huo, Dk. Shein alikutana
na Brigedia Jenerali Fadhil Omar Nondo aliyefika Ikulu mjini Zanzibar kwa ajili
ya kujitambulisha baada ya kuteuliwa kuwa Mkuu mpya wa Brigedi ya Nyuki Zanzibar.
Dk. Shein alitumia fursa
hiyo kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli
ambaye pia, ni Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi kwa kumteua Brigedia
Jenerali Fadhil Omar Nondo kushika wadhifa na kumpongeza Brigedia huyo huku
akimuhakikishi kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wake itampa
mashirikiano makubwa kama ilivyofanya kwa viongozi waliokuwepo kabla yake.
Nae, Brigedia Jenerali Nondo
alimuahidi Dk. Shein kuwa ataendeleza uhusiano na ushirikiano mwema ulipo kati
ya Majeshi ya Ulinzi Tanznia pamoja na
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar huku akisifu mashirikiano mazuri anayoyapata
kutoka kwa viongozi wa Serikali na viongozi wa vikosi vya ulinzi vya SMZ na
kuahidi kutoa ushirikiano kwao pamoja na kwa wananchi wote wa Zanzibar.
Brigedia Jenerali Fadhil
Omar Nondo anashika nafasi ya Marehemu Bregedia Jenerali
Cyril Ivor Mhaiki, aliyekuwa Kamanda wa Brigedia ya Nyuki Zanzibar, ambaye
alifariki dunia tarehe 13, Disemba mwaka 2016 huko katika Hospitali ya Jeshi la
Wananchi wa Tanzania, Lugalo jijini Dar-es-Salaam na kuzikwa Mkoani kwao Ruvuma.
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment