Habari za Punde

Rasimu ya Katiba ZFA yahojiwa kwanini iandikwe kwa kiingereza?



Na: Abubakar Khatib “Kisandu”, Zanzibar.

Baadhi ya wadau wa Soka Visiwani Zanzibar wameijia juu Rasimu ya awali ya katiba ya ZFA iliyowasilishwa hivi karibuni kwa kusema kuna vipengele havifai kabisa kuwemo na kwanini katibu na Mwenyekiti wa ZFA Wilaya awe na elimu kuanzia kidato cha nne wakati huo huo wakihoji kwanini iandikwe kwa lugha ya Kiengereza wakati wao ni Waswahili na wanatumia lugha yao ya Kiswahili.

Wakizungumza wakati tofauti na Mtandao huu baadhi ya Viongozi wa ZFA Wilaya ambao hawakupenda majina yao kutajwa wamesema ni vigumu sana kupita rasimu hiyo kwani ina mapungufu mengi sana.

“Hii Rasimu ina vichekesho sana tulipoiona tulishtuka, sisi viongozi ati tuwe na elimu kuanzia Form IV, kisha imeandikwa kwa Kiengereza wakati sisi ni Waswahili!, si rahisi kupita mazali na sisi ni miongoni mwa wapitishaji, kwasababu uongozi si kusoma bali uongozi ni kipaji na mapenzi ya kitu”.

Juzi Jumatatu ya Mei 29, 2017 Kamati ya kuandika upya katiba ya ZFA chini ya katibu wao Saleh Ali Said iliwasilisha rasimu ya awali kwa katibu mkuu wa Chama hicho kwenye Afisi ya ZFA iliyopo Aman Mjini Unguja na sasa inasubiriwa kusambazwa kwa wadau wao kwa ajili ya kupitiwa.

Kwa mujibu wa katiba ya ZFA wadau wao ni Viongozi wa Zfa wilaya, Vilabu, kamati ya ufundi, kamati ya soka la vijana, kamati ya soka LA ufukweni, kamati ya watu wenye ulemavu, kamati ya waamuzi na kamati ya soka la Wanawake ambao wote tayari wameshapatiwa rasimu hiyo.

Lakini bado baadhi ya Wadau hao wana hofu kubwa baada ya kuona sifa nyingi zimebdilika zikiwemo ya kuwa na Elimu ya Kidato cha nne kwa Katibu na Mwenyekiti wa ZFA Wilaya ambapo baadhi yao viongozi hao hawana sifa hiyo.

Mtandao huu ukamtafuta Katibu wa Kamati hiyo ya kuandika upya katiba ya ZFA Saleh Ali Said ambae pia ni Mwanasheria wa Chama hicho ambapo amewatoa wasi wasi wadau waliyopata mshtuko mkubwa baada ya kuiona Rasimu hiyo huku akiwaambia kuwa hiyo ni Rasimu tu na wapitishaji ni wao na ZFA ambapo wao wamepewa kuiangalia kisha kama ina kasoro watatoa michango yao wapi na wapi parekebishwe ili ipatikane katiba iliyobora zaidi ambayo inaendana na CAF.

“Mimi nawaambia wasishtuke hiyo ni Rasimu tu, na wao waipitie na waifahamu vizuri kisha watatoa michango yao, lakini yote ya yote wenye maamuzi ya mwisho ya kuipitisha hiyo ni ZFA, sisi kamati kazi yetu ndio hiyo tunasubiri jukumu jengine, na hicho Kiengereza kama hawafahamu tutawasaidia mana mimi ukiachia kuwa katibu wa kamati hii pia ni Mwanasheria wa ZFA, sasa tutawatafsiria na pia huko CAF huipeleki katiba kwa Kiswahili, unapeleka Katiba kwa Kiengereza ukisikia Uganda, Kenya, Msubiji na hata wenzetu Tanzania wote katiba zao kwa Kiengereza wala si Kiswahili, muhimu palipokuwa hapajafahamika tutawatfsiria”. Alisema Saleh.

Kamati ya kuandika upya katiba ya ZFA ina wajumbe sita (6) ambao ni Afan Othman Juma (Mwenyekiti), Saleh Ali Said (Katibu), Othman Ali Hamad (Msaidizi Katibu), pia yumo Kocha mkuu wa timu ya Taifa ya Zanzibar ya soka la Wanawake (Zanzibar Queens) Nassra Juma na wengine ni Eliud Peter Mvella na Ame Abdallah  Dunia.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.