Na.Haji Nassor - Pemba.
WALISHASEMA
waliotutangulia kuwa, nguo ya kuazimwa haiendewi ngomani.
Walijenga hofu kuwa, maana mwenyewe anaweza kukuadhiri, au hata
kukuvua na pengine ngoma ndo kwanza ‘inogele’.
Hawa, hawakuwa tofauti na wale waliotuambia kuwa, mtegemea cha
ndugu hufa masikini.Yote kwa yote, kumbe kumiliki chako ni jambo la faraja, maana
unaweza kukitumia, kukipunzisha wakati wowote uupendao.
Na ndio maana kauli hizo na nyengine, zimekuwa zikirejewa mara
kwa mara na wanaharakati wanaopambaana na magwiji wanaowapa watoto mimba za
umri mdogo.hapa Zanzibar.
Wanaharakati hawa wamekuwa wakisaka mwarubaini na tatizo hilo
kwa mtoto wa kike, miaka nenda miaka rudi, ingawa kikwazo wanachokumbana nacho
ni ukosefu wa mashine ya vina saba ‘DNA’ Zazibar.
Changamoto ya mashine hiyo, imeshabisha hodi serikali kuu, baada
ya wanaharakati hao na waathirika wa mimba za mapema kuwa na sauti moja kwa
muda mrefu sasa.
Mdau mkuu wa kadhia hizi Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake
Tanzania ‘TAMWA’ kimekua kikihaha kila kona ya dunia, kuona kundi hili la
watoto wa kike linakuwa huru kama yalivyo makundi mengine.
Afisa Miradi wa TAMWA ofisi ya Zanzibar, Asha Abdi Makame,
anaesema wamekuwa wakisaka, kwanza uwezo wa kuwafikia walengwa, ili kuwapa
taaluma ya kujikinga na kadhia hiyo.
“Sisi kama TAMWA kwanza tuntoa elimu ya athari za ndoa za mapema
na mimba za umri mdogo, lakini hata waandishi wa habari huwa tunawapa elimu ili
kuvitumia vyombo vyao kuelimisha hili’’,alisema.
Yeye anasema, TAMWA pamoja na shughuli zake nyengine, lakini
suala la kupiga vita mimba na ndoa za mapema, wamelipa kipaumbele cha pekee,
maana hata hivi karibuni baada ya kuhangaika wamepata mradi.
“Mfano wenzetu wa EU, wametufadhili ingawa tumeshirikiana na Shiriaka
la Kimatafa la Idadi ya Watu ‘UNFPA’ kuwa mradi wa kupiga vita mimba na ndoa za
mapema kwa watoto wa wasichana, sasa tunatarajia mafanikio’’,alifafanua.
TAMWA inakiri kuwa ukosefu wa mashine ya DNA, ni moja ya ukuta
mkubwa wa kumaliza kesi za mimba za umri mdogo wa watoto wa kike, kutokana na
Zanzibar kutokuwa na mashine yake yenyewe.
Analalamika kuwa kuwepo kwa mashine hiyo hospitali ya Muhimbili
pekee, ni udhaifu mkubwa, kwa wale watoto wa kike waliopewa ujauzito na kisha
kesi zao zikahitaji ‘DNA mahakamani.
‘’Unajua nguo ya kuazimwa haiendewi ngomani, sasa lazima
serikali inunue yake yenyewe, inaweza kuwa mwarubaini wa kuzipunguza ama
kuzimaliza kesi za mimba za mapema kwa watoto wetu’’,alisema.
Aliekuwa Mdhamini Afisi ya Mkurugenzi wa Mahitaka Pemba wakati
huo Al-baghiri Yakout Juma, anasema wanazo kezi zaidi ya 12 ambazo zinaendelea
kusota kwenye mahakama za Mkoa, zikisubiri kipimo cha ‘DNA’ kilichopo hospitali
ya Muhimbili.
“Unajua zinapopelekwa ‘sampuli’ kwa ajili ya kipimo cha ‘DNA’
Hospitali ya Muhimbili, ni sawa na kusema ndio mtoto wa kike ameshakoseshwa
haki yake, maana matokea hadi kurudi ni zaidi ya mwaka mmoja’’,anasema.
Mtoto wa kike (19) ambae anakesi katika mahakama ya Mkoa Chake
chake, tokea mwaka 2013, kwa sasa ameshajifungua na mwanawe anasoma skuli ya
maandalizi, ambapo kesi yake inasubiri matokeo ya ‘DNA’.
“Sina hakika kwamba kesi itatolewa hukumu, maana hata alienipa
ujauzito ameshamaliza kusoma chuo, na sasa yuko Unguja, anakuja kila baada ya
miezi miwili kughairishiwa kesi yake’’,anasema.
Nae muathirika wa mimba ambae amejifungua mwaka 2014 na tayari
sampuli ya damu imeshachukuliwa na kupelekwa Muhimbili, anasema hana hakika
sana kwamba kesi yake itamalizwa.
“Nasikia wapo wenzangu wana miaka zaidi ya minne bila ya matokeo
kurudi, sasa lazima Zanzibar iwe na ya kwake ili kupunguza foleni mahakamani,
na sisi tupate haki zetu mapema’’,alifafanua.
Yeye anasema kama serikali ya Zanzibar haina uwezo wa kununua
mashine ya ‘DNA’ ni vyema iwaombe wafadhili kama EU, UNESCO, DANIDA, WHO ili
wanunue, maana vyenginevyo wengine watakosa haki.
Fatma Marouz Kombo ambae ni Makamu Mwenyekiti wa Jumuia
Kuelimisha Athari za Madawa wa Kulevya, Ukimwi na Mimba za Utotoni ‘JUKAMKUM’
Pemba, anasema mwarubaini pekee wa kuzimaliza kesi za mimba ni kuwepo kwa
mashine ya ‘DNA’ Zanzibar, ambayo ndio chaka la vyombo vya sheria kwa sasa.
“Wakati umefika kwa serikali kununua mashine ya ‘DNA’ ili hawa
wanaowapa mimba watoto wetu, wasiwe na pakukimbilia, maana sasa wamekuwa
wakidunda mitaani, kwa vile hichi kipimo hakipo kwetu’’,aliweka wazi.
“Inaweza kuwa juhudi zetu za kutomeza hilo zikawa butu, iwapo
serikali yetu haitoharakisha kumiliki mashine yake ya ‘DNA’ badala ya kutegemea
ilioko Muhimbili’’,alifafanua.
Ali Mbarouk Omar ambae ni Afisa Mawasiliano wa Klabu ya watoto
Pemba ‘PCC’ anasema uwepo wa mwashine ya ‘DNA’ wahalifu wa kuwapa mimba watoto
watafikia mwisho.
“Lakini hata ukienda Dawati la jinsia la wanawake na watoto na
mahakamani, kesi nyingi zimelala sababu ikiwa ni kukosekana kwa kipimo cha DNA,
sasa ni kazi kwa serikali, kuinunua na kuondoa adha hiyo’’,alifafanua.
Katibu wa Jumuia ya Kupunguza Umaskini na Kuboresha Hali za
Wananchi Pemba (KUKHAWA) Hafidh Abdi Said, anasema pamoja na ushahidi
kukamilika, bado tatizo la kukosekana kwa mshine ‘DNA’ ni changamoto nyengine
katika vyombo vya kisheria.
Hivyo vyombo vya sheria nchini, wametakiwa kuacha kisingizio cha
ukosefu wa kipimo cha vina saba ‘DNA’ na kuwaachia huru wanaowadhalilisha
wanawake na watoto, ikiwa ni pamoja na wanaowapa mimba.
Afisa Mipango wilaya ya Chakechake Pemba, Kassim Ali Omar nae
akifungua kongamano la siku moja, la kupinga ukatili wa kijinsia,
lililoandaliwa na jumuia ya kimataifa ya ‘YUNA’ alipigia chapuo kuweko kwa
mashine hiyo hapa Zanzibar.
“Sio busara kwa vyombo hivyo, kupata kichaka cha ukosefu wa
kipimo hicho, na hatimae kuwaacha watoto wa wanawake, wakiwa wamedhalilika na
wakosaji, kudunga mitaani’’,anafafanua.
Akizungumza kwenye mdahalo huo, Mkuu wa Idara ya wanawake na
watoto wa Wizara ya uwezeshaji, ustawi wa Jamii maendeleo ya wanawake na watoto
Pemba wakati huo, Sara Khamis Salim, anasema wazazi wamekuwa wakijitahidi
katika malezi, ingawa watoto hubuni njia ya kuwatoroka.
Afisa mkuu wa dawati la jinsia na watoto la Polisi mkoa wa
kusini Pemba, Asha Talib, anasema wamekuwa wakikabiliwa na changamoto kadhaa,
katika kutomeza kesi za udhalilishaji wa kijinsia.
Polisi kwa makusudi limeanzisha madawati zaidi ya 417 Tanzania,
ili kuhakikisha wanawake na watoto wanaishi bila ya ukatili, ingawa jamii
imekuwa ikiviza nguvu hizo kwa kutokuwa tayari kutoa ushirikiano.
Hivi
karibuni Mkuu wa upelelezi na makosa ya jinai Jeshi la Polisi wilaya ya
Micheweni Pemba, Suleiman Khamis Juma, wakati akitoa mada juu ya majukumu ya
jeshi la Polisi, ukumbi wa Benjamin Mkapa Pemba, anasema kuwa kushughulikia
makosa ya udhalilishaji na ulawiti ni moja ya jukumu la jeshi la polisi.
Chakufurahisa
afisa huyo anaeleza kwenye kongamano hilo kuwa, jeshi la polisi kwa sasa
linamchakato wa kujenga maabara kubwa na ya kisasa katika maeneo ya wilaya ya
Kibaha mkoani Pwani, kwa lengo la kupunguza usumbufu na msongamano wa vipimo
vya vinasaba DNA.
Mwanasheria
wa serikali kutoka ofisi ya DPP Zanzibar ofisi ya Pemba, Ali Haidari Mohamed,
yeye anasema vitendo vya ubakaji na udhalilishaji, vimekuwa vikishika kasi
kubwa na kuwaathiri watoto kisaikolojia.
Lakini
Mratibu wa shirika Action Aid Pemba, Omar Ali Salum, aliitaka jamii kuacha
tabia ya kusuluhishana wenyewe kwa wenyewe, pale zinapotokea kesi hizo na
badala yake kuzifikisha kwenye vyombo vya sheria.
Naibu
Katibu Mkuu wziara inayoshughulikia wanawake na watoto Zanzibar Mauwa Makame
Rajab, ansema wazo la wanaharakati la kutiaka serikali inunue mashine hiyo ni
jambo jema, na sasa hilo linatarajiwa kufanyika.
‘’Unajua
kuwa zipo kesi nyingi mapaka waathirika wanakata tamaa za watoto wetu kupewa
ujauzito, sasa ni kweli Serikali ifanya hima kuwepo kwa mashine
hiyo’’,alifafanua.
Tokea
mwaka 2011 hadi mwezi mwaka 2017 Dawati la Polisi mkoa wa Kusini Pemba
lilipokea kesi 10 za mimba, kwa ajili ya kupatiwa kipimo vya ‘DNA’ na hadi
mwaka 2014 ni mbili zilizorudi na nyengine zikiwa foleni kusubiria kipimo
hicho.
Mambo hayo ni tofauti kwa jamii ya leo, na ndio maana wapo
watoto wa kike 196, kati yao 122 wameripotiwa kupewa ujauzito na 74 kuolewa
wakiwa chini ya umri wa miaka 18.
Idadi hiyo ni ile kuanzia mwezi Januari mwaka 2012 hadi mwezi Disemba
mwaka 2016, tena hali hiyo ni kwa wilaya
za Chakechake na Mkoni pekee.
Uchunguzi ukabaini kuwa, kwa mwaka 2012 pekee, kesi za mimba za
utotoni zilikuwa 73, wakati kipindi cha mwezi Januari hadi disemba 2014,
ziliripotiwa kesi 49 za mimba kwa wanafunzi.
Kesi za ndoa kwa wanafunzi, kulikuwa na idadi ya 54, kwa mwaka
2012 na mwaka 2016 kuliripotiwa kesi 20 katika taasisi mbali mbali.
Wizara ya elimu pekee ilikusanya jumla ya kesi 67 za mimba na
ndoa, ambapo kati ya hizo, mwaka 2012 kesi za ndoa zilikuwa 38, wakati kesi za
mimba kwa wanafunzi zilikuwa 14, wakati mwaka huu kumesharipotiwa kesi 9 za
ndoa na 6 za mimba.
Vyanzo mbali mbali vya habari, vilisema chanzo cha kujitokeza
kwa matendo hayo husababishwa na mambo kadhaa, ikiwa ni pamoja na ukosefu wa
mashine ya DNA Zanzibar.
Sheha wa shehia ya Madungu wilaya ya Chakechake, Mafunda Hamad
Rubea, aliweka wazi kuwa, kwa kama Serikali ikinunua mashine yake, sasa watoto
wa kike watapata haki zao kwenye kesi za mimba na ubakaji.
Mrajisi wa Elimu Zanzibar Siajabu Suleiman Pandu, anasema
ukosefu wa mashine ya ‘DNA’ kwa Zanzibar ndio kikwazo pekee, maana mtoto wa
kike huathirika mara mbili na wa kiume mara moja.
“Mtoto wa kike kwanza kesi yake huchelewa maana hata samapuli ya
vina saba ikija, mwenzake ameshasahu machungu yeye bado, sasa lazima tuwe na
yetu Zanzibar’’,alisema.
Shirika la Kimataifala Kuchangia Maendeleo ya Mtoto, limeeleza kuwa,
wasichana zaidi ya milioni 14 huolewa wakiwa na umri chini ya miaka 18, katika
nchi za kusini mwa jangwa la sahara, nchi za Chad, Niger na Mali zinaongoza.
Azimio la Umoja wa Mataifa la kupunguza aina zote za
udhalilishaji kwa wanawake (CEDAW) haliruhusu watoto wenye umri wa chini ya
miaka 18 kuolewa.
Azimio la Haki za Binaadamu (the 1948 UDHR) linasema kwamba ndoa
yoyote nilazima iwe ni ya maridhiano na kwamba mtoto mwenye umri chini ya miaka
18 huwa hana maamuzi huru.
Kila mwaka, watoto milioni 7.3 wa kike chini ya umri wa
miaka 18 hushika na kujifungua mimba, imesema ripoti mpya kuhusu hali ya idadi
ya watu mwaka 2013, ambayo imetolewa na Shirika la Mfuko wa Idadi ya Watu
katika Umoja wa Mataifa, UNFPA.
Ripoti hiyo imesema, milioni 2 kati ya watoto hao wana umri usozidi miaka 14, na kwamba watoto
hao hukumbana na matatizo ya muda mrefu ya kiafya na kijamii kutokana na mimba
hizo, yakiwemo vifo vinavyohusiana na uzazi.
Katika kukuza kampeni
dhidi ya mimba za utotoni, na unyanyasaji kwa watoto, UNFPA nchini Tanzania, limeshiriki katika
mashindano ya riadha ya Kilimanjaro Marathon nchini humo.
Hata hivyo aliekuwahi
kuwa Naibu Waziri wa Afya, Dk. Sira Ubwa Mamboya mwezi Julai mwaka 2011,
alisema Serikali ina mpango wa kununua mashine ya ‘DNA’ kutokana na umuhimu
wake.
Alibainisha kuwa Serikali imeshafanya upembuzi yakinifu kwa kushirikiana
na ofisi ya maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano Tanzania,
pamoja na kutayarisha jengo la Mkemia Mkuu kwa ajili ya kuweka mashine hiyo.
Aidha alisema DNA ni mashine ya kupima uasilia pale panapotokezea utata wa
mtoto, kipimo hicho hufanyika baada ya kuzaliwa mtoto na kuthibitisha nani baba
halisi.
Sasa serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar hivi karibuni kupitia waziri wake katika afisi ya Makamu
wa pili wa rais Zanzibar Mohamed Aboud Mohamed, amesema tayari serikali
imeshatenga shilingi bilioni 1 kwa ajili ya ununuzi wa mashine hiyo.
“Sasa serikali
imeshatenga bilioni 1 kutoka kwenye fungu la Mkemia mkuu wa serikali kwenye
mwaka huu wa fedha wa 2017/2018 kwa ajili ua kununua mashine ya
DNA”,anabainisha.
Jengine linalotarajiwa
kufanywa sambamba ni serikali imeshatenga shilingi milioni 175 kwa ajili ya
matumizi ya shughuli mbali mbali za mapambano ikiwemo kuwaelimisha wananchi.
No comments:
Post a Comment