STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Pemba 23.08.2017
RAIS wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, amesema kuwa lengo la Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar la kuliimarisha zao la karafuu ni kuwaneemesha wakulima wa zao hilo na
kuwafanya wawe na maisha bora zaidi kuliko ilivyo sasa.
Amesema mipango ya kuliongezea
thamani zao hilo pamoja na kuyatambua mashamba ya Serikali inalenga kuwaongezea
kipato wananchi pamoja na kuwaweka utaratibu mzuri ambao baadae utawafanya
wanaoyatumia vyema na kwa uadilifu mashamba hayo kuweza kumilikishwa.
Dk. Shein aliyasema hayo leo
mara baada ya kushiriki kikamilifu katika shughuli za uchumaji na uchambuaji wa
karafuu huko katika kambi ya Karafuu ya Mshashani ya mkulima Mohammed Kai
Bakari iliyopo Kifundi,Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Amesema utaratibu wa sasa
ambapo wakulima wa karafuu wanauza karafuu zao Shirika la Taifa la Biashara (ZSTC)
kama zilivyo baada ya kukaushwa na ZSTC kuuza kwenye soko la dunia, haziipi
faida kubwa serikali wala mkulima kuliko ambavyo zao hilo lingeongezwa thamani.
Kutokana na hali hiyo, Dk.
Shein amesisitiza kuwa tafiti zitaendelea kufanywa kwa lengo la kuliongezea
thamani zao hilo la karafuu na kuna haja ya wanasayansi waongeze kasi katika
kuliongezeza thamani zao hilo.
Aidha, amesema mchakato wa
sasa ambao serikali unaendelea nao wa kuyatambua mashamba yake hatimaye utaweka
utaratibu mzuri wa kuwamilikisha wakulima wanaoyatumia vizuri.
Dk. Shein alisema kuwa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imefanya uwamuzi wa makusudi wa kuliongezea
bei zao hilo kwa lengo la kulipa heshima zao la karafuu.
Aliongeza kuwa Serikali
haina nia wala lengo la kuwanyanganya wakulima mashamba ya karafuu kama
inavyoelezwa na baadhi ya watu wachache bali ina mpaongo wa kuyatambua mashamba
yake yote ya karafuu pamoja na eka za serikali.
Dk. Shein alieleza kuwa
kila mwenye haki ya kupewa shamba ama heka atapewa kwa taratibu zitakazopewa na
wale wenye kuyashughulikia mashamba hayo hivi sasa watapewa kipaumbele.
Nae Waziri wa Kilimo,
Maliasili, Mifugo na Uvuvi Hamad Rashid Mohamed alitoa shukurani kwa Rais Dk.
Shein kwa kushiriki vyema katika shughuli ya uchumaji na uchambuzi wa karafuu.
Aliongeza kuwa ukulima wa
zao la karafuu ni mgumu hivyo hatua za serikali za kuwaongezea wakulima beo za
zao hilo na kutoa agizo kuwa asilimia 80 ya bei ya dunia walipwe wakulima ni
mfano mzuri wa kuonesha kuwa Rais Dk. Shein na Serikali anayoiongoza inawajali
wakulima.
Mapema Dk. Shein alipata
maelezo juu ya ukodishwaji wa zao hilo la karafuu ulioanza tarehe 5 mwezi huu
na tayari mashamba 100 yameshakodishwa yenye thamani ya TZS 158.9.
Shamba la mzee Mohammed
Bakari Kai lima mikarafuu 125 bado halijakodoshwa lakini wakati ukifika wa
ukodishwaji kipaumbele kitawekwa kwa msimamizi wa shamba hilo ambaye ni mkulima
maarufu na mwenye sifa za kilimo ambaye aliwahi kupewa zawadi ya mkulima bora
hapo mwaka juzi.
Balozi Ali Karume ambaye
ni Kaimu Waziri wa Bishara, Viwanda na Masoko alieleza haja ya kulithamini zao
hilo kwani ni zao la uchumi hapa nchini.
Nae mkulima huyo Mohammed
Kai alitoa pongezi kwa Rais Dk. Shein kwa hatua yake ya kufika katika shamba na
hatimae katika kambi yake na kujionea shughuli za kambini hapo na kuungana na
wakulima kwa kuchambua karafuu.
Mkulima huyo alieleza
anavyofarajika na juhudi za Dk. Shein chini ya Serikali anayoiongoza katika
kuliimarisha zao hilo la karafuu huku akieleza uzoefu wake katika kilimo cha
karafuu pamoja na zawadi alizowahi kupewa kutokana na ukulima wake.
Mapema Dk. Shein aliweka
jiwe la Msingi katika Skuli ya Chiba na kueleza azma ya Serikali ya kuiendeleza
skuli hiyo ili watoto wapate fursa ya kusoma na kuondoa tatizo la kwenda skuli
za mbali na makaazi yao.
Dk. Shein aliwapongeza
wazee pamoja na Mfuko wa Halmashauri kwa juhudi kubwa walizozichukua katika
ujenzi wa madarasa manne ya skuli hiyo pamoja na ofisi za mwalimu mkuu
ambapohadi kufikia hatua hiyo ujenzi umegharimu TZS milioni 37.3.
Aidha, aliwataka watoto wa
Chimba wasome kwa juhudi kubwa na kuwasisitiza kuwa Chimba itajengwa na
wanachimba wenyewe.
Aidha, aliwata walimu
kuwasomesha watoto vyema na wasichanganye elimu na siasa wala wasisomeshe kwa
kuwababaisha kwani lengo ni kuwapa elimu bora watoto wote.
Pamona ja hayo, Dk. Shein
aliwahakikishia wananchi wa Chimba kuwa barabara yao yenye urefu wa kilomita
8.9 itajengwa kwa kiwango cha lami.
Akiwa katika ziara hiyo
Dk. Shein aliweka jiwe la msingi katika Tawi la CCM Njuguni na baadae kupigisha
harambee kwa lengo la kumaliza ujenzi wa Tawi hilo ambapo zilipatikana fedha
zote milioni saba ambapo yeye alichangia milioni mbili.
Katika maelezo yake, Dk.
Shein alisema kuwa ujenzi wa matawi ya chama ni njia moja wapo ya kukiimarisha
chama hicho na hatimae kuweza kuongeza wanachama na kuweza kufanya vyema
shughuli za chama kwa ufanisi zaidi.
Kabla ya hapo Dk. Shein
alipokea taarifa ya Mkoa wa Kaskazini Pemba hapo katika ukumbi wa Chuo Kikuu
cha Taifa SUZA, Mchangamdogo.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment