Habari za Punde

Jamii Imetakiwa Kuona Aibu Kutumia Fedha za Suluhu za Kesi za Ubakaji na Ulawiti - ZLSC

Na.Haji Nassor - Pemba.

JAMII kisiwani Pemba, imetakiwa kuona vibaya na aibu kutumia fedha zinazotokana na sulhu za kesi za watoto wao waliobakwa au kulwitiwa, kwani kufanya hivyo hakusaidii kupunguza matendo hayo.

Akizungumza na wananchi wa shehia za Ukutini Jimbo la Chambani wilaya ya Mkoani na shehia ya  Wingwi mapofu wilaya ya Micheweni Pemba, Afisa Mipango wa Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar ZLSC tawi la Pemba, Khalfan Amour Mohamed, alipokuwa akizungumza na wananchi hao kwenye mikutano ya kutoa msaada wa kisheria kwa wananchi.

Alisema wapo baadhi ya wazazi na walezi wamekuwa na mtindo wa kuzimaliza kienyeji kesi hizo kwa kuchukua fedha ambazo kisha huzitumia kwa mahitaji ya kila siku.
Afisa Mipango huyo alisema lazima jami ifike pahala ione aibu na fedheha kwa kukubali kesi za watoto wao waliobakw au kulawitiwa kuchukua fedha ili zimalizike kienyeji wakidhani kufanya hivyo ndio suluhu.

Alieleza kuwa, wazazi hao wamekuwa wakifanya hivyo ikiwa ni aina moja ya rushwa ya muhali, huku watoto wao wakikosa haki zao, na wafanyaji wa matendo hayo kuendelea.

“Mbakaji au mtu mwenye tabia ya kulawiti, akiona mzazi anapokea fedha baada ya tukio, basi baada ya muda anafanya tena tendo hilo, lazima sasa mubadilike na muache kuchukua fedha kama suluhu ya udhalilishaji huo”,alifafanua.

Kwa upande wake Afisa Mipango wa Kituo hicho Siti Habibu Mohamed, aliwataka wananchi hao kujenga utamaduni wa kuandikia kila wanapofanya mauziano.

Alisema wapo baadhi ya wananchi wamekuwa wakinunua maeneo ya ardhi, nyumba, vyombo vya usafiri bila ya kuwepo maandikiano jambo ambalo baade huzaa migogoro.
Sheha wa shehia ya Wingwi mapofu Ali Hamad Saleh, alisema nafasi waliopewa wananchi wake ni muhimu, maana wapo wanaohitaji msaada wa kisheri wakalazimika kutumia fedha nyingi.

Aidha alisema wakati umefika sasa kwa wananchi kuhakikisha wanajisomea sheria mbali mbali, kwa kuwatumia wasaidizi wa sheria waliopo majimboni ili kufahamu haki na wajibu wao.

Baadhi ya wananchi wa shehia hizo wamekipongeza Kituo hicho kwa kuwafuata na kuwapa msaada wa kisheria bila ya malipo, jambo ambalo limewapa mwanga wa kujua haki zao.

Salama Othaman Ramadhan mkaazi wa shehia ya Ukutini Jimbo kla Chambani alisema, sasa ameelewa njia za kufanya iwapo mwanawe atabakwa, jambo ambalo kabla hakuwa na taaluma.

“Mimi ilikuwa najua kuwa mwanangu akishabakwa, kama watakubali tumaliziane kwa suluhu, ilikuwa ndio dawa, lakini sasa kumbe hiyo ni kesi ya jinai, inatakiwa ifikishwe mahakamani”,alifafanua.

Nae Asia Saleh Salim alisema, ameshapata uwelewa juu ya njia za kufanya kisheria, anapotaka kununua mali, ikiwa ni pamoja na kuifanyia uhakiki iwapo haina migogoro.
Kwa upande wake mwananchi wa shehia ya Wingwi mapofu wilaya ya Micheweni, Ali Juma Hamad alisema jamii lazima iongezewe dozi ya elimu juu ya athari za kuzifanyia sulhu kesi hizo.

Nae Kombo Juma, amesema sasa anaelewa kuwa kumbe Halmashauri inayo mamlaka ya kumpandisha mtu kwenye mahakama zake, iwapo watakwenda kinyume na maagizo.

“Elimu ya ufafanuzi wa masuali yetu imenipa uwelewa na sasa kilichobakia nyinyi Kituo cha Huduma za Sheria endeleeni kutupia vijijini kwetu ili tujue haki na wajibu wetu kisheria”,alifafanu.

Akitoa ufafanuzi haki za mtoto Afisa Mipango wa Kituo hicho Mohamed Hassan Ali, alisema wakati umefika kwa jamii kuwa na malezi ya pamoa ili kukomesha mtendo maovu yanayofanywa na watoto.

“Njia mwafaka ambayo inaweza kuwatoa watoto wetu kwenye majanga yaliopo ni kuhakikisha tunasaidiana kimalezi badala ya utaratibu wa sasa wa kila mmoja kulea mwanawe”,alifafanua.


Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar ZLSC tawi la Pemba, tayari kimeshwatembelea waanchi wa shehia za Mbuyuni, Ukutini, Winwgwi mapofu, Wesha, Kiwani, Kengeja, Shengejuu, Kinowe. Mgogoni, na Kiungoni kuwapa msaada wa kisheri bila ya malipo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.