Habari za Punde

Vikundi Vya Wanawake Vikoba Kisiwani Pemba Vyaimarisha Ndoa Kijiji Cha Vitongoji.

Na.Haji Nassor - Pemba.
WANAWAKE wa shehia ya Vitongoji wilaya ya Chakechake kisiwani Pemba, wamesema kujiunga kwao kwenye vikundi vya kuweka na kukopa, ‘hisa’ ni hatua muhimu kwao kuwasaidia waume zao huduma za kila siku, hasa kwa vile hutokezea siku wanakosa.

Walisema wanaume hawana mkataba na Muumba, kwamba kila siku watakuwa wanakamilisha hudua za ndani ya nyumba, hivyo kuingia kwao kwenye vikundi hivyo vya kuweka hisa, pamoja na mambo mengine, lakini pia ni kuwasaidia wenza wao huduma za lazima.

Wakizungumza na waandishi wa habari wa habari vyombo mbali mbali, wanawake hao walisema, wamegundua iwapo mwanamme ndani ya nyumba atapewa msaada kwa baadhi ya siku, hata ndoa zao hupata heshima na nidhamu.

Mwenyekiti wa kikundi cha kuweka na kukopa cha ‘wema hauozi’ Maryam Saleh Juma, alisema ni ukweli usiofichika yeye kabla ya kujiingiza kwenye vikundi hivyo, hakuona sana thamani ya ndoa yake.

Alisema wanaume wanaokuwa na wanawake wanaosubiri kila huduma kuletewa, hukosa furaha ya ndoa zao, jambo linalohatarisha usalama na uendelevu wa ndoa husika, ingawa iwapo mwanamke anamchango huwa tofauti.

“Mfano kama mimi sasa nahisi mume wangu ananielewa kwenye ndoa, na amekuwa akinishirikisha na kunishauri mambo ambayo kabla nikiona anafanya uamuzi tu peke yake”,alifafanua.

Nae Katibu wa kikundi hicho Zena Khamis Juma, alisema yeye kupitia uwanaharakati wake wa upandaji wa mboga mboga na kujiwekea akiba, sasa amefanikiwa kujenga nyumba ya pili kwa kushirikiana na mume wake.

Alieleza kuwa, ingawa kiwango kikubwa cha fedha alizokuwa akiziweka kwenye hisa akipewa na mume wake, lakini tayari nyumba hiyo imekamilika na sasa mume wake ameongeza mke wa pili.

“Mimi sijaona vibaya mume wangu kuongeza mke kwa kushirikiana nguvu zake na zangu, maana nilimruhusu na sasa nimepata nguvu zaidi ya kuendelea na ujasiriamali na yeye amenikubali”,alifafanua.

Alisema kwa sasa, wameshakamilisha ujenzi wa nyumba ya kisasa yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 30, na hana wasiwasi wa kuwahudumia watoto wake kwa vifaa vya madrassa na skuli.

Nae mume wa mjasiriamali huyo Juma Abrahaman Said, alikiri kuokolewa kimaisha na mke wake huyo kutokana na ujasiriamali wake anaoendelea nao.

Alifafanua kuwa msaada mkubwa anaoupata kwa mke wake huyo umemuwezesha kujenge nyumba ya pilia, ambayo anasema asilimia 40 ya gharama pamoja na nguvu kazi zilitokana na mke wake.

“Mimi hata nikiamua nyumba kutaka kuiza na tukikubaliana kuiuza kwa shilingi milioni 30, basi twazigawa sawa sawa, maana kama sio yeye mimi nisingepaya ujasiri wa kujenga nyumba”,alifafanua.

Hata hivyo amewakumbusha wanaume kuacha dhana potofu kuwa wanawake wanapojiingiza kwenye ujasiriamali ni uhuni na usema huko ndio wanakofikia ndoto zao.

Nae Mwenyekiti wa kikundi cha Tumain kinachojishughulisha na ukulima wa mboga mboga Mtuwa Ali Vue, alieleza kuwa lazima wanaume waache mzaha wa kuwafungia wake zao, na badala yake wawape uhuru wa kujiletea maendeleo.

“Wakati umefika sasa kwa wanawake kujiwezesha, kinachotakiwa ni kwa wanaume waliomo kwenye ndoa kuhakikisha, wanawaruhusu wake zao maana wakiwafungia watawazidisha umaskini”,alifafanua.

Hata hivyo Shamim Haji Makame, alisema bado wapo baadhi ya wanaume hawajaona umuhimu wa wanawake kuwa na chao, jambo linalopelekea ugumu, kwa baadhi ya wanawake kuijiingiza kwenye vikundi vya ujasiriamali.

Mkubwa Ali Mkubwa ambae ni mjasiriamali aliewaajiri wanawake watatu kwenye shamba lake la mboga mboga alisema, kama bado kuna wanaume wamekuwa wazito kuwaruhusu wake zao kuijiingiza kwenye umoja wa kujiletea maendeleo, wamechelewa kuamka.

“Hivi sasa tofauti ya mwanamke na mwanamme ni ile ya kimaumbile tu, lakini kwenye kusaka toke, watu wote wako sawa, maana maisha ya kuwa goli kipa hasa kwenye ndao yamekwisha”,alifafanua.

Omar Mjawiri Hamad yeye anasema, bado hajaamua mke wake kumpeleka shambani, kushughulikia kilimo kwa vile yeye mwenyewe anamudu kazi hiyo.

Sheha wa shehi ya Vitongoji Salum Ayoub Suleiman alisema, kwenye shehia yake, baada ya wanawake kupata elimu ya ujasiriamali, sasa hali za maisha yao hasa kwa waliomo ndani ya ndoa yamebadilika.

“Sasa mwanamke wa Vitongoji akiwa anahitaji fedha kwa ajili ya harusi, fedha za vifaa vya skuli, msiba au michango mengine ya familia, basi hukopa kwenye hisa au huuza mboga mboga”,alifafanua.

Hata hivyo wakulima hao wa mboga mboga shehiani humo, wamesema kwa sasa changamoto kubwa inayowarejesha nyuma ni ukosefu wa soko la uhakika.

Shehia ya Vitongoji wilaya ya Chakechake pekee, inajumla vikundi vya mboga mboga 15 na vya ufugaji 20, hisa 45 na vya ufugaji wa nyuki zaidi ya 10.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.