Habari za Punde

Kocha Dedi Ajiunga na Timu ya RASKA ZONE

Na: Abubakar Khatib Kisandu, Zanzibar.
Kocha anaesifika kwa kuibuwa vipaji Mohammed Yussuf "Dedi" amejiunga kuifundisha klabu ya Raska Zone itakayoshiriki ligi daraja la Pili Taifa Unguja msimu huu mpya wa mwaka 2017-2018 akitokea Villa FC (Mpira Pesa).

Meneja wa Raska Zone Ali Mkanga amethibitisha kumteuwa kocha huyo ambae amefunga mkataba wa miaka miwili kuifundisha timu hiyo yenye maskani yake Michenzani Mjini Unguja.

"Ni kweli tumemteuwa kocha Mohammed Dedi au wengine wanamwita Babu Rigo, ameshatuambia anataka nini mahitaji yake na sisi tayari tumeshampa vilivyobakia vitu vidogo vidogo tu, tunategemea kufanya nae kazi katika msimu mpya kwenye ligi daraja la pili taifa, timu kashaiona na amekubali kufanya nayo kazi". Alisema Mkanga.

Kwa upande wake kocha huyo amefurahishwa sana kujiunga na Raska Zone huku akikiri kuwa timu kadhaa zilimfata kuhitaji huduma yake lakini mwenyewe akavutiwa na Raska Zone.

"Nimefurahi kuanza maisha mapya na Raska Zone, unajua timu nyingi zilinifata lakini mimi nikapendezwa sana na Raska Zone kwasababu uongozi wake upo imara sana na hata mazingira ya timu inavyoendeshwa ni mazuri sana, nawaambia wapenzi wote wangu Babu Rigo waendelee kuniunga mkono katika maisha yetu yote". Alisema Kocha Dedi.

Kocha huyo ana leseni C ya Ukocha inayotambuliwa na Shirikisho la Soka Barani Afrika "CAF". 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.