Habari za Punde

Miembeni yaendelea kuchezea kichapo mechi tatu mfululizo

 Kikosi cha timu yas JKU kilichoifunga Mimbeni City 1-0
Kikosi cha Miembeni City 

MIEMBENI CITY YAENDELEA KUCHAPWA MECHI TATU MFULULIZO, JKU WANAONGOZA LIGI KUU ZENJ KANDA YA UNGUJA

Na Abubakar Khatib Kisandu, Zanzibar.

Jinamizi bado linaendelea kuwatesa timu ya Miembeni City ambayo kwa mara ya kwanza inacheza ligi kuu soka ya Zanzibar Kanda ya Unguja baada ya kucheza michezo mitatu mfululizo ya awali na yote kupoteza kufuatia kipigo cha leo cha bao 1-0 kutoka kwa JKU.

Mchezo huo umepigwa jioni ya leo katika uwanja wa Amaan ambapo bao la JKU likifungwa na Amour Suleiman (Pwina) dakika ya 35. 
Kwa matokeo hayo JKU inaongoza ligi hiyo ikiwa na alama 9 kufuatia kushinda michezo yake yote mitatu ya awali baada ya kuichapa Mafunzo 1-0, kisha kuwafunga Chuoni 3-2 na leo kuwamaliza City 1-0.

Kwa upande wao Miembeni City hawana hata alama moja baada ya kupoteza michezo yote mitatu ya mwanzo kufuatia kufungwa na Polisi 1-0, kisha wakachapwa 1-0 na Mafunzo na leo kumalizwa 1-0 na JKU.

Saa 8 za mchana leo ulipigwa mchezo mwengine kiwanjani hapo ambapo Timu ya Taifa ya Jang’ombe (Wakombozi wa Ngambo) wametoka sare ya 1-1 na Mafunzo.

Kwa matokeo hayo Taifa amefikisha alama 2 baada ya kufungwa 1-0 na Zimamoto, kisha wakatoka sare ya 0-0 na Polisi na leo wakatoka sare ya 1-1 na Mafunzo.
Kwa upande wake Mafunzo wamefikisha alama 4 baada ya kucheza michezo mitatu kufuatia kufungwa 1-0 na JKU, kisha wakaichapa Miembeni City 1-0 na leo kutoka sare ya 1-1 na Taifa.

Ligi hiyo itaendelea tena kesho kwa kupigwa michezo miwili katika uwanja wa Amaan ambapo Saa 8:00 za mchana Black Sailors watakipiga na Kilimani City na saa 10:00 za jioni Charawe watacheza na KMKM.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.